Sura: ATTAUBA 

Aya : 1

بَرَآءَةٞ مِّنَ ٱللَّهِ وَرَسُولِهِۦٓ إِلَى ٱلَّذِينَ عَٰهَدتُّم مِّنَ ٱلۡمُشۡرِكِينَ

(Hili ni tangazo na angalizo la) Kujitoa (katika makubaliano) litokalo kwa Allah na Mtume wake kwenda kwa wale washirikina (makafiri) mlioingia nao makubaliano



Sura: ATTAUBA 

Aya : 2

فَسِيحُواْ فِي ٱلۡأَرۡضِ أَرۡبَعَةَ أَشۡهُرٖ وَٱعۡلَمُوٓاْ أَنَّكُمۡ غَيۡرُ مُعۡجِزِي ٱللَّهِ وَأَنَّ ٱللَّهَ مُخۡزِي ٱلۡكَٰفِرِينَ

Basi (enyi Washirikina) tembeeni katika ardhi (popote mpendapo kwa) muda wa miezi minne (bila kusumbuliwa), na jueni kwamba nyinyi hamuwezi kumshinda Allah (hamna pa kukimbilia), na kwamba Allah ni Mwenye kuwafedhehesha makafiri (Mwenye kuwaingiza katika hizaya)



Sura: ATTAUBA 

Aya : 3

وَأَذَٰنٞ مِّنَ ٱللَّهِ وَرَسُولِهِۦٓ إِلَى ٱلنَّاسِ يَوۡمَ ٱلۡحَجِّ ٱلۡأَكۡبَرِ أَنَّ ٱللَّهَ بَرِيٓءٞ مِّنَ ٱلۡمُشۡرِكِينَ وَرَسُولُهُۥۚ فَإِن تُبۡتُمۡ فَهُوَ خَيۡرٞ لَّكُمۡۖ وَإِن تَوَلَّيۡتُمۡ فَٱعۡلَمُوٓاْ أَنَّكُمۡ غَيۡرُ مُعۡجِزِي ٱللَّهِۗ وَبَشِّرِ ٱلَّذِينَ كَفَرُواْ بِعَذَابٍ أَلِيمٍ

Na (hili) ni tangazo kutoka kwa Allah na Mtume wake kwenda kwa watu (wote) Siku Kubwa ya Hija kwamba, Allah na Mtume wake, wamejiweka kando (kwenye makubaliano) na washirikina (makafiri). Basi iwapo (nyinyi makafiri) mtatubu hiyo itakuwa heri kwenu, na mkikengeuka (mkaipinga haki) basi jueni kuwa nyinyi hamuwezi kumshinda (kumtoroka) Allah. Na wabashirie (waonye) makafiri kuwa watapata adhabu iumizayo mno



Sura: ATTAUBA 

Aya : 4

إِلَّا ٱلَّذِينَ عَٰهَدتُّم مِّنَ ٱلۡمُشۡرِكِينَ ثُمَّ لَمۡ يَنقُصُوكُمۡ شَيۡـٔٗا وَلَمۡ يُظَٰهِرُواْ عَلَيۡكُمۡ أَحَدٗا فَأَتِمُّوٓاْ إِلَيۡهِمۡ عَهۡدَهُمۡ إِلَىٰ مُدَّتِهِمۡۚ إِنَّ ٱللَّهَ يُحِبُّ ٱلۡمُتَّقِينَ

Isipokuwa wale washirikina ambao mliahidiana nao kisha hawakuwapunguzieni chochote, wala hawakumsaidia (adui) yeyote dhidi yenu, basi hao watimizieni ahadi yao mpaka muda wao. Hakika Allah anawapenda wacha Mungu



Sura: ATTAUBA 

Aya : 5

فَإِذَا ٱنسَلَخَ ٱلۡأَشۡهُرُ ٱلۡحُرُمُ فَٱقۡتُلُواْ ٱلۡمُشۡرِكِينَ حَيۡثُ وَجَدتُّمُوهُمۡ وَخُذُوهُمۡ وَٱحۡصُرُوهُمۡ وَٱقۡعُدُواْ لَهُمۡ كُلَّ مَرۡصَدٖۚ فَإِن تَابُواْ وَأَقَامُواْ ٱلصَّلَوٰةَ وَءَاتَوُاْ ٱلزَّكَوٰةَ فَخَلُّواْ سَبِيلَهُمۡۚ إِنَّ ٱللَّهَ غَفُورٞ رَّحِيمٞ

Basi inapokwisha Miezi (minne) Mitukufu (ambayo mliwapa amani makafiri) basi (tengueni ahadi na) waueni washirikina popote mnapowakuta, na washikeni (watieni mbaroni) na wazingireni, na wakalieni (wadhibitini) katika kila njia (kila kona). Basi iwapo watatubu (wataacha ukafiri) nawakasimamisha Swala na wakatoa Zaka, basi waachieni (kwakuwa wameshakuwa ndugu zenu katika imani). Hakika Allah ni Mwenye kusamehe mno, Mwenye kurehemu



Sura: ATTAUBA 

Aya : 6

وَإِنۡ أَحَدٞ مِّنَ ٱلۡمُشۡرِكِينَ ٱسۡتَجَارَكَ فَأَجِرۡهُ حَتَّىٰ يَسۡمَعَ كَلَٰمَ ٱللَّهِ ثُمَّ أَبۡلِغۡهُ مَأۡمَنَهُۥۚ ذَٰلِكَ بِأَنَّهُمۡ قَوۡمٞ لَّا يَعۡلَمُونَ

Na iwapo yeyote katika washirikina (makafiri) wakikuomba ujirani (na ulinzi na amani kwenye himaya yako), basi mpe ujirani (ukae naye) ili apate kuyasikia maneno ya Allah. Kisha mfikishe mahali pake pa amani (sehemu atakayokuwa salama). Hiyo ni kwa kuwa hao ni watu wasiojua (Uislamu)



Sura: ATTAUBA 

Aya : 7

كَيۡفَ يَكُونُ لِلۡمُشۡرِكِينَ عَهۡدٌ عِندَ ٱللَّهِ وَعِندَ رَسُولِهِۦٓ إِلَّا ٱلَّذِينَ عَٰهَدتُّمۡ عِندَ ٱلۡمَسۡجِدِ ٱلۡحَرَامِۖ فَمَا ٱسۡتَقَٰمُواْ لَكُمۡ فَٱسۡتَقِيمُواْ لَهُمۡۚ إِنَّ ٱللَّهَ يُحِبُّ ٱلۡمُتَّقِينَ

Vipi washirikina (makafiri waliovunja makubaliano) wawe na makubaliano mbele ya Allah na mbele ya Mtume wake ukiwatoa wale mlioafikiana nao kwenye Msikiti Mtukufu? Basi nendeni nao sawa madamu nao wanakwenda nanyi. Hakika Allah anawapenda wachaMungu



Sura: ATTAUBA 

Aya : 8

كَيۡفَ وَإِن يَظۡهَرُواْ عَلَيۡكُمۡ لَا يَرۡقُبُواْ فِيكُمۡ إِلّٗا وَلَا ذِمَّةٗۚ يُرۡضُونَكُم بِأَفۡوَٰهِهِمۡ وَتَأۡبَىٰ قُلُوبُهُمۡ وَأَكۡثَرُهُمۡ فَٰسِقُونَ

Vipi (makafiri) waheshimu ahadi na makubaliano) na ilhali wakikushindeni hawatazami (hawajali) kwenu udugu wala ahadi[1]. Wanawafurahisheni kwa vinywa vyao tu (kwa maneno matamu), na ilhali nyoyo zao zinakataa. Na wengi wao ni waovu


1- - Aya hii inatuelekeza kwamba, siku zote tabia za makafiri ni kuangalia mvumo wa upepo unakoelekea. Pale pasipobudi hujilazimisha kuingia kwenye maafikiano, maridhiano au kuonesha utii wa kimaslahi iwapo tu ushindi au mamlaka yamewatoka na yameshikwa na wasiokuwa wao. Lakini kila wanapojihisi wao ndio wenye mamlaka au hatamu, wanawatenga Waislamu na kuwapumbaza kwa kuwapiga porojo mbalimbali. Makafiri ni wabinafsi, hawaheshimu utu, haki wala makubaliano.


Sura: ATTAUBA 

Aya : 9

ٱشۡتَرَوۡاْ بِـَٔايَٰتِ ٱللَّهِ ثَمَنٗا قَلِيلٗا فَصَدُّواْ عَن سَبِيلِهِۦٓۚ إِنَّهُمۡ سَآءَ مَا كَانُواْ يَعۡمَلُونَ

Wamezibadilisha Aya za Allah kwa thamani duni mno, na wakaizuia Njia yake (kwa kuiwekea vikwazo ili watu wasiifuate). Hakika ni jambo ovu sana walilokuwa wanalifanya



Sura: ATTAUBA 

Aya : 10

لَا يَرۡقُبُونَ فِي مُؤۡمِنٍ إِلّٗا وَلَا ذِمَّةٗۚ وَأُوْلَـٰٓئِكَ هُمُ ٱلۡمُعۡتَدُونَ

(Makafiri wapo kwenye vita dhidi ya Uislamu na Waislamu muda wote) Hawatazami (hawajali) kwa Muumini udugu wala ahadi, na hao ndio wavukao mipaka



Sura: ATTAUBA 

Aya : 11

فَإِن تَابُواْ وَأَقَامُواْ ٱلصَّلَوٰةَ وَءَاتَوُاْ ٱلزَّكَوٰةَ فَإِخۡوَٰنُكُمۡ فِي ٱلدِّينِۗ وَنُفَصِّلُ ٱلۡأٓيَٰتِ لِقَوۡمٖ يَعۡلَمُونَ

Basi (Makafiri) wakitubu (wakiacha ukafiri na kuingia katika Uislamu) na wakasimamisha Swala na wakatoa Zaka, basi ni ndugu zenu katika Dini. Na tunazifafanua Aya kwa watu wanaojua



Sura: ATTAUBA 

Aya : 12

وَإِن نَّكَثُوٓاْ أَيۡمَٰنَهُم مِّنۢ بَعۡدِ عَهۡدِهِمۡ وَطَعَنُواْ فِي دِينِكُمۡ فَقَٰتِلُوٓاْ أَئِمَّةَ ٱلۡكُفۡرِ إِنَّهُمۡ لَآ أَيۡمَٰنَ لَهُمۡ لَعَلَّهُمۡ يَنتَهُونَ

Na iwapo Makafiri) watavunja viapo vyao baada ya ahadi zao, na wakaitukana Dini yenu, basi waueni viongozi wa ukafiri. Hakika, hao hawana muamana (hawaheshimu viapo vyao). (Washirikina wakiona wanauawa au wanapigwa) huenda wakaacha[1]


1- - Aya hizi za 11 na 12 zinawahiyarisha washirikishaji mambo mawili; ima watubu au waingie vitani.


Sura: ATTAUBA 

Aya : 13

أَلَا تُقَٰتِلُونَ قَوۡمٗا نَّكَثُوٓاْ أَيۡمَٰنَهُمۡ وَهَمُّواْ بِإِخۡرَاجِ ٱلرَّسُولِ وَهُم بَدَءُوكُمۡ أَوَّلَ مَرَّةٍۚ أَتَخۡشَوۡنَهُمۡۚ فَٱللَّهُ أَحَقُّ أَن تَخۡشَوۡهُ إِن كُنتُم مُّؤۡمِنِينَ

Hivi kwa nini hampigani na watu waliokiuka viapo vyao na kudhamiria kumfukuza Mtume, na hao ndio waliokuanzeni (kukuchozeni) mara ya kwanza?[1] Je, mnawaogopa? Basi Allah anastahiki zaidi kuogopwa, ikiwa nyinyi ni Waumini (wa kweli)


1- - Allah katika Aya hizi tatu 11,12 na13 anawahimiza Waislamu kuingia kwenye mapambano na makafiri kwa sababu kuu tatu. Mosi, Pale dini yao inapotukanwa na kudhalilishwa. Pili, Ahadi zinapokiukwa, na Tatu wanapodhamiria kumfukuza (au kumdhuru) Mtume (au kiongozi yeyote wa dini yao).


Sura: ATTAUBA 

Aya : 14

قَٰتِلُوهُمۡ يُعَذِّبۡهُمُ ٱللَّهُ بِأَيۡدِيكُمۡ وَيُخۡزِهِمۡ وَيَنصُرۡكُمۡ عَلَيۡهِمۡ وَيَشۡفِ صُدُورَ قَوۡمٖ مُّؤۡمِنِينَ

Piganeni nao, Allah atawaadhibu kwa mikono yenu, na atawafedhehesha na atakunusuruni dhidi yao, na ataviponya vifua vya watu waumini



Sura: ATTAUBA 

Aya : 15

وَيُذۡهِبۡ غَيۡظَ قُلُوبِهِمۡۗ وَيَتُوبُ ٱللَّهُ عَلَىٰ مَن يَشَآءُۗ وَٱللَّهُ عَلِيمٌ حَكِيمٌ

Na ataondoa hasira ya nyoyo zao (hao waumini). Na Allah humkubalia toba amtakaye. Na Allah ni Mwenye kujua sana, Mwenye hekima nyingi



Sura: ATTAUBA 

Aya : 16

أَمۡ حَسِبۡتُمۡ أَن تُتۡرَكُواْ وَلَمَّا يَعۡلَمِ ٱللَّهُ ٱلَّذِينَ جَٰهَدُواْ مِنكُمۡ وَلَمۡ يَتَّخِذُواْ مِن دُونِ ٱللَّهِ وَلَا رَسُولِهِۦ وَلَا ٱلۡمُؤۡمِنِينَ وَلِيجَةٗۚ وَٱللَّهُ خَبِيرُۢ بِمَا تَعۡمَلُونَ

Hivi mlidhani (enyi waumini) kuwa mtaachwa tu bila ya Allah kuwajua wale waliopigana Jihadi kati yenu, na wala hawakumfanya mwandani wao isipokuwa Allah na Mtume wake na Waumini wenzao? Na Allah ana habari nyingi za yote mnayoyatenda



Sura: ATTAUBA 

Aya : 17

مَا كَانَ لِلۡمُشۡرِكِينَ أَن يَعۡمُرُواْ مَسَٰجِدَ ٱللَّهِ شَٰهِدِينَ عَلَىٰٓ أَنفُسِهِم بِٱلۡكُفۡرِۚ أُوْلَـٰٓئِكَ حَبِطَتۡ أَعۡمَٰلُهُمۡ وَفِي ٱلنَّارِ هُمۡ خَٰلِدُونَ

Hawawezekani kwa Washirikina (makafiri) kuiamirisha misikiti ya Allah, ilhali wanajishuhudishia wao wenyewe ukafiri. Hao ndio ambao vitendo vyao vimepomoka (vimeharibika), na katika moto watadumu milele



Sura: ATTAUBA 

Aya : 18

إِنَّمَا يَعۡمُرُ مَسَٰجِدَ ٱللَّهِ مَنۡ ءَامَنَ بِٱللَّهِ وَٱلۡيَوۡمِ ٱلۡأٓخِرِ وَأَقَامَ ٱلصَّلَوٰةَ وَءَاتَى ٱلزَّكَوٰةَ وَلَمۡ يَخۡشَ إِلَّا ٱللَّهَۖ فَعَسَىٰٓ أُوْلَـٰٓئِكَ أَن يَكُونُواْ مِنَ ٱلۡمُهۡتَدِينَ

Hakika ilivyo ni kwamba, wanaoamirisha misikiti ya Allah ni wale wanaomuamini Allah na Siku ya Mwisho na wakasimamisha Swala na wakatoa Zaka na wala hawamuogopi (yeyote) ila Allah tu. Basi huwenda hao wakawa miongoni mwa walioongoka



Sura: ATTAUBA 

Aya : 19

۞أَجَعَلۡتُمۡ سِقَايَةَ ٱلۡحَآجِّ وَعِمَارَةَ ٱلۡمَسۡجِدِ ٱلۡحَرَامِ كَمَنۡ ءَامَنَ بِٱللَّهِ وَٱلۡيَوۡمِ ٱلۡأٓخِرِ وَجَٰهَدَ فِي سَبِيلِ ٱللَّهِۚ لَا يَسۡتَوُۥنَ عِندَ ٱللَّهِۗ وَٱللَّهُ لَا يَهۡدِي ٱلۡقَوۡمَ ٱلظَّـٰلِمِينَ

Je, mnafanya (jambo la) kuwapa maji Mahujaji na kuimarisha Msikiti Mtukufu (kwa huduma) ni sawa na mwenye kumuamini Allah na Siku ya Mwisho na akapigana Jihadi katika Njia ya Allah? Hawawi sawa mbele ya Allah. Na Allah hawaongozi watu madhalimu



Sura: ATTAUBA 

Aya : 20

ٱلَّذِينَ ءَامَنُواْ وَهَاجَرُواْ وَجَٰهَدُواْ فِي سَبِيلِ ٱللَّهِ بِأَمۡوَٰلِهِمۡ وَأَنفُسِهِمۡ أَعۡظَمُ دَرَجَةً عِندَ ٱللَّهِۚ وَأُوْلَـٰٓئِكَ هُمُ ٱلۡفَآئِزُونَ

Wale walioamini na wakahama na wakapigana Jihadi katika Njia ya Allah kwa mali zao na nafsi zao, hao wana hadhi kubwa zaidi mbele ya Allah na hao tu ndio wenye kufuzu



Sura: ATTAUBA 

Aya : 21

يُبَشِّرُهُمۡ رَبُّهُم بِرَحۡمَةٖ مِّنۡهُ وَرِضۡوَٰنٖ وَجَنَّـٰتٖ لَّهُمۡ فِيهَا نَعِيمٞ مُّقِيمٌ

Mola wao Mlezi anawabashiria rehema zitokazo kwake na radhi na Pepo (mbalimbali) ambazo humo watapata neema za kudumu



Sura: ATTAUBA 

Aya : 22

خَٰلِدِينَ فِيهَآ أَبَدًاۚ إِنَّ ٱللَّهَ عِندَهُۥٓ أَجۡرٌ عَظِيمٞ

Watadumu humo milele. Hakika kwa Allah yapo malipo (ya aina mbalimbali tena) makubwa mno



Sura: ATTAUBA 

Aya : 23

يَـٰٓأَيُّهَا ٱلَّذِينَ ءَامَنُواْ لَا تَتَّخِذُوٓاْ ءَابَآءَكُمۡ وَإِخۡوَٰنَكُمۡ أَوۡلِيَآءَ إِنِ ٱسۡتَحَبُّواْ ٱلۡكُفۡرَ عَلَى ٱلۡإِيمَٰنِۚ وَمَن يَتَوَلَّهُم مِّنكُمۡ فَأُوْلَـٰٓئِكَ هُمُ ٱلظَّـٰلِمُونَ

Enyi mlioamini, msiwafanye baba zenu na ndugu zenu kuwa marafiki (wa ndani wa kuwategemea) ikiwa watapenda kuchagua ukafiri kuliko Imani (Uislamu). Na yeyote katika nyinyi atakayewafanya marafiki (na kuwaibia siri za Waislamu), basi hao ndio madhalimu hasa



Sura: ATTAUBA 

Aya : 24

قُلۡ إِن كَانَ ءَابَآؤُكُمۡ وَأَبۡنَآؤُكُمۡ وَإِخۡوَٰنُكُمۡ وَأَزۡوَٰجُكُمۡ وَعَشِيرَتُكُمۡ وَأَمۡوَٰلٌ ٱقۡتَرَفۡتُمُوهَا وَتِجَٰرَةٞ تَخۡشَوۡنَ كَسَادَهَا وَمَسَٰكِنُ تَرۡضَوۡنَهَآ أَحَبَّ إِلَيۡكُم مِّنَ ٱللَّهِ وَرَسُولِهِۦ وَجِهَادٖ فِي سَبِيلِهِۦ فَتَرَبَّصُواْ حَتَّىٰ يَأۡتِيَ ٱللَّهُ بِأَمۡرِهِۦۗ وَٱللَّهُ لَا يَهۡدِي ٱلۡقَوۡمَ ٱلۡفَٰسِقِينَ

Sema: Ikiwa baba zenu na watoto wenu na ndugu zenu na wake zenu na jamaa zenu na mali mlizochuma na biashara mnazoogopa kuharibika kwake (kwa kukosa soko) na majumba mnayoyapenda ni vipendwa zaidi kwenu kuliko Allah na Mtume wake na kupigana Jihadi katika Njia yake, basi ngojeni mpaka Allah alete amri yake (adhabu yake). Na Allah hawaongozi watu waovu



Sura: ATTAUBA 

Aya : 25

لَقَدۡ نَصَرَكُمُ ٱللَّهُ فِي مَوَاطِنَ كَثِيرَةٖ وَيَوۡمَ حُنَيۡنٍ إِذۡ أَعۡجَبَتۡكُمۡ كَثۡرَتُكُمۡ فَلَمۡ تُغۡنِ عَنكُمۡ شَيۡـٔٗا وَضَاقَتۡ عَلَيۡكُمُ ٱلۡأَرۡضُ بِمَا رَحُبَتۡ ثُمَّ وَلَّيۡتُم مُّدۡبِرِينَ

Kwa hakika kabisa, Allah (pamoja na uchache na udhaifu wenu) amekunusuruni katika maeneo mengi na (pia) siku ya Hunaini ambapo wingi wenu ulikufurahisheni (ulikuvimbisheni vichwa)[1] na (lakini wingi huo) haukukusaidieni kitu na ardhi, pamoja na wasaa wake, ikawa finyu kwenu. Kisha mkageuka nyuma (mkamuacha Mtume) mkikimbia


1- - Nyinyi mlikuwa elfu kumi na mbili na maadui wenu walikuwa elfu nne.


Sura: ATTAUBA 

Aya : 26

ثُمَّ أَنزَلَ ٱللَّهُ سَكِينَتَهُۥ عَلَىٰ رَسُولِهِۦ وَعَلَى ٱلۡمُؤۡمِنِينَ وَأَنزَلَ جُنُودٗا لَّمۡ تَرَوۡهَا وَعَذَّبَ ٱلَّذِينَ كَفَرُواْۚ وَذَٰلِكَ جَزَآءُ ٱلۡكَٰفِرِينَ

Kisha Allah akateremsha utulivu wake kwa Mtume wake na kwa Waumini, na akateremsha majeshi ambayo hamkuyaona na akawaadhibu wale waliokufuru. Na hiyo ndio malipo ya makafiri



Sura: ATTAUBA 

Aya : 27

ثُمَّ يَتُوبُ ٱللَّهُ مِنۢ بَعۡدِ ذَٰلِكَ عَلَىٰ مَن يَشَآءُۗ وَٱللَّهُ غَفُورٞ رَّحِيمٞ

Kisha baada ya hayo Allah anamsamehe amtakaye. Na Allah ni Mwenye kusamehe sana, Mwenye kuhurumia mno



Sura: ATTAUBA 

Aya : 28

يَـٰٓأَيُّهَا ٱلَّذِينَ ءَامَنُوٓاْ إِنَّمَا ٱلۡمُشۡرِكُونَ نَجَسٞ فَلَا يَقۡرَبُواْ ٱلۡمَسۡجِدَ ٱلۡحَرَامَ بَعۡدَ عَامِهِمۡ هَٰذَاۚ وَإِنۡ خِفۡتُمۡ عَيۡلَةٗ فَسَوۡفَ يُغۡنِيكُمُ ٱللَّهُ مِن فَضۡلِهِۦٓ إِن شَآءَۚ إِنَّ ٱللَّهَ عَلِيمٌ حَكِيمٞ

Enyi mlioamini, hakika washiri-kina (makafiri) ni Najisi.[1] Kwa hivyo, wasiusogelee Msikiti Mtukufu (wa Makka) baada ya mwaka wao huu[2]. Na ikiwa mnachelea umasikini (kwa kukatikiwa na misaada au biashara zitokazo kwao), basi Allah atakutajirisheni kutoka katika fadhila zake akitaka. Hakika, Allah ni Mwenye kujua mno, Mwenye hekima nyingi


1- - Najisi inayokusudiwa hapa ni Najisi na uchafu wa itikadi, na sio kwamba ni uchafu wa mwili wa kutofaa kukaa pamoja, kula pamoja au kupeana mikono.


2- - Zuio na marufuku hii ilianza mwaka wa tisa wa Hijiria kwa Kalenda ya Kiislamu. Zuio hili linahusu Msikiti Mtukufu wa Makka tu. Ama misikiti mingine, kafiri anaweza kuingia ikiwa kuna sababu ya kufanya hivyo kama Mtume (Allah amshushie rehema na amani, alivyoruhusu makafiri kadhaa kuingia katika msikiti wa Madina kwa sababu mbali mbali.


Sura: ATTAUBA 

Aya : 29

قَٰتِلُواْ ٱلَّذِينَ لَا يُؤۡمِنُونَ بِٱللَّهِ وَلَا بِٱلۡيَوۡمِ ٱلۡأٓخِرِ وَلَا يُحَرِّمُونَ مَا حَرَّمَ ٱللَّهُ وَرَسُولُهُۥ وَلَا يَدِينُونَ دِينَ ٱلۡحَقِّ مِنَ ٱلَّذِينَ أُوتُواْ ٱلۡكِتَٰبَ حَتَّىٰ يُعۡطُواْ ٱلۡجِزۡيَةَ عَن يَدٖ وَهُمۡ صَٰغِرُونَ

(Enyi Waislamu) Piganeni na wasiomuamini Allah wala Siku ya Mwisho na hawaharamishi alivyoviharimisha Allah na Mtume wake na hawafuati Dini ya Haki, miongoni mwa waliopewa Kitabu, mpaka watoe kodi[1] kwa hiari yao na wao wakiwa dhalili.[2]


1- - Jizia ni kodi maalumu anayoitoa kafiri mwenye uwezo wa kuitoa katika serikali ya Kiislamu kwa sababu ya huduma anazozipata ikiwemo ulinzi na usalama wa maisha yake, mwili wake, mali yake, dini yake, hadhi na heshima yake.


2- - Maana ya Aya hii ni maelekezo kwa mamlaka ya serikali ya Kiislamu ambayo imeshika hatamu. Sio maelekezo kwa mtu mmoja mmoja au kikundi kisichokuwa na mamlaka ya kisheria.


Sura: ATTAUBA 

Aya : 30

وَقَالَتِ ٱلۡيَهُودُ عُزَيۡرٌ ٱبۡنُ ٱللَّهِ وَقَالَتِ ٱلنَّصَٰرَى ٱلۡمَسِيحُ ٱبۡنُ ٱللَّهِۖ ذَٰلِكَ قَوۡلُهُم بِأَفۡوَٰهِهِمۡۖ يُضَٰهِـُٔونَ قَوۡلَ ٱلَّذِينَ كَفَرُواْ مِن قَبۡلُۚ قَٰتَلَهُمُ ٱللَّهُۖ أَنَّىٰ يُؤۡفَكُونَ

Na Wayahudi walisema: Uzeri ni Mwana wa Allah. Na Wanaswara walisema: Masihi ni Mwana wa Allah (Mwana wa Mungu). Hiyo ni kauli yao (waisemayo) kwa vinywa vyao. Wanayaiga maneno ya waliokufuru kabla yao. Allah amewalaani. Inakuwaje wanapotoshwa?