Sura: ANNISAI 

Aya : 91

سَتَجِدُونَ ءَاخَرِينَ يُرِيدُونَ أَن يَأۡمَنُوكُمۡ وَيَأۡمَنُواْ قَوۡمَهُمۡ كُلَّ مَا رُدُّوٓاْ إِلَى ٱلۡفِتۡنَةِ أُرۡكِسُواْ فِيهَاۚ فَإِن لَّمۡ يَعۡتَزِلُوكُمۡ وَيُلۡقُوٓاْ إِلَيۡكُمُ ٱلسَّلَمَ وَيَكُفُّوٓاْ أَيۡدِيَهُمۡ فَخُذُوهُمۡ وَٱقۡتُلُوهُمۡ حَيۡثُ ثَقِفۡتُمُوهُمۡۚ وَأُوْلَـٰٓئِكُمۡ جَعَلۡنَا لَكُمۡ عَلَيۡهِمۡ سُلۡطَٰنٗا مُّبِينٗا

Mtawakuta wengine wanataka kukaa nanyi kwa amani (kwa kuonesha kuwa nao wameamini) na kukaa kwa amani na watu wao (kwa kuwaonesha kuwa bado wao ni makafiri). Kila wanaporudishwa kwenye fitina (ukafiri) wanaporomoshwa (wanaburuzwa na kurudi kwa kasi kubwa) kwenye ukafiri huo. Basi kama hawakukuacheni na hawakukutangazieni amani na hawakuizuia mikono yao (wakaacha kukupigeni), basi wakamateni na waueni popote mtakapowakuta, na hao tumekupeni hoja ya wazi (ya kuwashambulia, kuwapiga, kuwaua na kuwakamata mateka)



Sura: ANNISAI 

Aya : 92

وَمَا كَانَ لِمُؤۡمِنٍ أَن يَقۡتُلَ مُؤۡمِنًا إِلَّا خَطَـٔٗاۚ وَمَن قَتَلَ مُؤۡمِنًا خَطَـٔٗا فَتَحۡرِيرُ رَقَبَةٖ مُّؤۡمِنَةٖ وَدِيَةٞ مُّسَلَّمَةٌ إِلَىٰٓ أَهۡلِهِۦٓ إِلَّآ أَن يَصَّدَّقُواْۚ فَإِن كَانَ مِن قَوۡمٍ عَدُوّٖ لَّكُمۡ وَهُوَ مُؤۡمِنٞ فَتَحۡرِيرُ رَقَبَةٖ مُّؤۡمِنَةٖۖ وَإِن كَانَ مِن قَوۡمِۭ بَيۡنَكُمۡ وَبَيۡنَهُم مِّيثَٰقٞ فَدِيَةٞ مُّسَلَّمَةٌ إِلَىٰٓ أَهۡلِهِۦ وَتَحۡرِيرُ رَقَبَةٖ مُّؤۡمِنَةٖۖ فَمَن لَّمۡ يَجِدۡ فَصِيَامُ شَهۡرَيۡنِ مُتَتَابِعَيۡنِ تَوۡبَةٗ مِّنَ ٱللَّهِۗ وَكَانَ ٱللَّهُ عَلِيمًا حَكِيمٗا

Na haiwi kwa Muumini (Muis-lamu) yeyote kumuua Muumini (mwingine) isipokuwa tu kwa kukosea. Na yeyote aliyemuua Muumini kwa kukosea, basi (adhabu yake) ni kuacha huru mtumwa Muumini (Muislamu) na Dia (fidia)[1] itakayokabidhiwa kwa ndugu zake (warithi wake), isipokuwa tu kama (ndugu hao) watafanya Dia hiyo sadaka (kwa kusamehe). Na kama (aliyeuliwa) ni kutoka kwa watu maadui wenu (makafiri), na yeye (marehemu) ni Mumini (Muislamu), basi (adhabu ya muuaji) ni kuacha huru mtumwa Muislamu tu.[2] Na kama (aliyeuliwa) ni kutoka kwa watu (makafiri) ambao kuna mkataba kati yenu na wao (wa kuishi kwa amani) basi (adhabu ya muuaji) ni Dia (fidia) itakayokabidhiwa kwa ndugu zake na kuacha huru mtumwa Muislamu[3]. Basi ambaye hakupata (mtumwa wa kumuacha huru adhabu yake) ni kufunga miezi miwili mfululizo. (Hii) Ndio toba kutoka kwa Allah, na Allah ni Mjuzi sana, Mwenye hekima nyingi


1- - Dia au fidia ya kuua ni ngamia mia moja (100) kama alivyoainisha Mtume, Allah amshushie rehema na amani, katika waraka alioutuma kwa watu wa Yemen. Ameyanukuu haya Imamu Malik katika kitabu chake cha Muwattwai.


2- - Hapa aya inamaanisha kuwa aliyeuliwa ni Muislamu lakini ndugu zake ni makafiri. Hivyo hakuna fidia itakayotolewa isipokuwa tu kuacha huru Mtumwa Muislamu. Kwa nini fidia hapa haipo? Ni kwa sababu fidia kama itatolewa itakwenda kwa makafiri wenye uadui na Uislamu. Kuwapa fidia makafiri maadui ni kuwapa nguvu dhidi ya Waislamu.


3- - Pamoja na kwamba ndugu wa Muislamu aliyeuliwa ni makafiri lakini hapa Uislamu unawapa fidia kwa sababu fidia hiyo haitarajiwi kutumika katika kuwadhuru Waislamu kwa sababu makafiri hawa wamo katika mkataba wa kuishi kwa amani. Hapa tunajifunza namna Uislamu unavyothamini amani na utulivu katika jamii. Ndugu wa marehemu kama ni makafiri wasioingia mkataba wa amani na Waislamu hawapewi Dia. Ama kama ni makafiri walioingia mkataba wa amani na Waislamu wanapewa Dia kwa kuzingatia amani.


Sura: ANNISAI 

Aya : 93

وَمَن يَقۡتُلۡ مُؤۡمِنٗا مُّتَعَمِّدٗا فَجَزَآؤُهُۥ جَهَنَّمُ خَٰلِدٗا فِيهَا وَغَضِبَ ٱللَّهُ عَلَيۡهِ وَلَعَنَهُۥ وَأَعَدَّ لَهُۥ عَذَابًا عَظِيمٗا

Na yeyote anayemuua Muumini (Muislamu) kwa kukusudia basi malipo yake ni Jahanamu, ataishi humo milele na Allah amemghadhibikia na amemlaani na amemuandalia adhabu kubwa kabisa



Sura: ANNISAI 

Aya : 94

يَـٰٓأَيُّهَا ٱلَّذِينَ ءَامَنُوٓاْ إِذَا ضَرَبۡتُمۡ فِي سَبِيلِ ٱللَّهِ فَتَبَيَّنُواْ وَلَا تَقُولُواْ لِمَنۡ أَلۡقَىٰٓ إِلَيۡكُمُ ٱلسَّلَٰمَ لَسۡتَ مُؤۡمِنٗا تَبۡتَغُونَ عَرَضَ ٱلۡحَيَوٰةِ ٱلدُّنۡيَا فَعِندَ ٱللَّهِ مَغَانِمُ كَثِيرَةٞۚ كَذَٰلِكَ كُنتُم مِّن قَبۡلُ فَمَنَّ ٱللَّهُ عَلَيۡكُمۡ فَتَبَيَّنُوٓاْۚ إِنَّ ٱللَّهَ كَانَ بِمَا تَعۡمَلُونَ خَبِيرٗا

Enyi mlioamini, mnaposafiri katika njia ya Allah (Jihadi), basi kuweni waangalifu. Na msimwambie yeyote aliyekusalimieni (kwa maamkizi ya Kiislamu[1]) kwamba: “Wewe sio Muumini”, kwa kutaka manufaa ya maisha ya dunia hii. Basi kwa Allah ziko ngawira (kheri) nyingi. Hivyo ndivyo mlivyo kuwa nyinyi zamani (kwa kutamka tu na Uislamu wenu ukakubalika), na Allah akakuneemesheni, basi zindukeni. Hakika Allah ni Mjuzi wa yote mnayoyatenda


1- - Waislamu, wanapokuwa vitani, wanakatazwa kumdhuru mtu ambaye ameonesha alama za kwamba ameukubali Uislamu, ikiwa ni pamoja na kutumia maamkizi ya Kiislamu yenye kuashiria amani.


Sura: ANNISAI 

Aya : 95

لَّا يَسۡتَوِي ٱلۡقَٰعِدُونَ مِنَ ٱلۡمُؤۡمِنِينَ غَيۡرُ أُوْلِي ٱلضَّرَرِ وَٱلۡمُجَٰهِدُونَ فِي سَبِيلِ ٱللَّهِ بِأَمۡوَٰلِهِمۡ وَأَنفُسِهِمۡۚ فَضَّلَ ٱللَّهُ ٱلۡمُجَٰهِدِينَ بِأَمۡوَٰلِهِمۡ وَأَنفُسِهِمۡ عَلَى ٱلۡقَٰعِدِينَ دَرَجَةٗۚ وَكُلّٗا وَعَدَ ٱللَّهُ ٱلۡحُسۡنَىٰۚ وَفَضَّلَ ٱللَّهُ ٱلۡمُجَٰهِدِينَ عَلَى ٱلۡقَٰعِدِينَ أَجۡرًا عَظِيمٗا

Waumini wasiokuwa na udhuru wowote waliokaa (kwa kuacha kwenda vitani) hawawi sawa na wale wanaopigana Jihadi katika njia ya Allah kwa mali zao na nafsi zao. Allah amewafanya bora zaidi kwa daraja wanaopigana Jihadi kwa mali zao na nafsi zao kuliko wanaokaa. Na wote Allah amewaahidi mazuri (Pepo)[1]. Na Allah amewafanya bora zaidi wanaopigana Jihadi kuliko wanaokaa kwa ujira mkubwa kabisa


1- - Kwa mujibu wa Aya hii ni kwamba, waumini walioshiriki Jihadi na ambao hawakushiriki wote Allah amewaahidi Pepo. Huu ni ushahidi kwamba, wale wanaodai kuwa Swahaba wengi waliritadi na kukufuru kwa kutoshiriki Jihadi isipokuwa wachache tu madai hayo ni ya uongo na itikadi yao hii sio sahihi.


Sura: ANNISAI 

Aya : 96

دَرَجَٰتٖ مِّنۡهُ وَمَغۡفِرَةٗ وَرَحۡمَةٗۚ وَكَانَ ٱللَّهُ غَفُورٗا رَّحِيمًا

Ni daraja nyingi kutoka kwake na msamaha na rehema. Na Allah amekuwa Mwingi wa kusamehe, Mwenye kurehemu



Sura: ANNISAI 

Aya : 97

إِنَّ ٱلَّذِينَ تَوَفَّىٰهُمُ ٱلۡمَلَـٰٓئِكَةُ ظَالِمِيٓ أَنفُسِهِمۡ قَالُواْ فِيمَ كُنتُمۡۖ قَالُواْ كُنَّا مُسۡتَضۡعَفِينَ فِي ٱلۡأَرۡضِۚ قَالُوٓاْ أَلَمۡ تَكُنۡ أَرۡضُ ٱللَّهِ وَٰسِعَةٗ فَتُهَاجِرُواْ فِيهَاۚ فَأُوْلَـٰٓئِكَ مَأۡوَىٰهُمۡ جَهَنَّمُۖ وَسَآءَتۡ مَصِيرًا

Hakika, wale ambao Malaika wamewafisha (wamewatoa roho) ilhali wamezidhulumu nafsi zao, (Malaika) watawauliza: Je, mlikuwa na nini nyinyi? Watasema: Tulikuwa wayonge katika ardhi (duniani). (Malaika) Watawaambia: Hivi Ardhi ya Allah haikuwa yenye wasaa mkahama humo? Basi hao makazi yao ni Jahanamu, na marejeo mabaya mno ni hayo.[1]


1- - Aya hii inawataka Waislamu kutoridhika na mazingira ambayo sio rafiki katika kutekeleza majukumu ya dini yao na pia mambo yao ya kimaendeleo. Wanatakiwa kupambana na ikishindikana wahame na kwenda eneo jingine lenye mazingira rafiki.


Sura: ANNISAI 

Aya : 98

إِلَّا ٱلۡمُسۡتَضۡعَفِينَ مِنَ ٱلرِّجَالِ وَٱلنِّسَآءِ وَٱلۡوِلۡدَٰنِ لَا يَسۡتَطِيعُونَ حِيلَةٗ وَلَا يَهۡتَدُونَ سَبِيلٗا

Isipokuwa (wanaosameheka na dhambi hii ni) wale wanyonge ikiwa ni pamoja na wanaume na wanawake na watoto ambao hawawezi (kufanya) mbinu yoyote (ya kujihami) na hawajui njia (ya kukimbilia)[1]


1- - Kusameheka kwa mwanaume ni kwa sababu ya uzee, ugonjwa n.k. Kwa mwanamke ni kwa sababu ya jinsia yake, na kwa mtoto ni kwa sababu ya umri.


Sura: ANNISAI 

Aya : 99

فَأُوْلَـٰٓئِكَ عَسَى ٱللَّهُ أَن يَعۡفُوَ عَنۡهُمۡۚ وَكَانَ ٱللَّهُ عَفُوًّا غَفُورٗا

Basi hao huenda Allah akawasamehe, na Allah ni Msamehevu sana, Mwingi wa kufuta dhambi



Sura: ANNISAI 

Aya : 100

۞وَمَن يُهَاجِرۡ فِي سَبِيلِ ٱللَّهِ يَجِدۡ فِي ٱلۡأَرۡضِ مُرَٰغَمٗا كَثِيرٗا وَسَعَةٗۚ وَمَن يَخۡرُجۡ مِنۢ بَيۡتِهِۦ مُهَاجِرًا إِلَى ٱللَّهِ وَرَسُولِهِۦ ثُمَّ يُدۡرِكۡهُ ٱلۡمَوۡتُ فَقَدۡ وَقَعَ أَجۡرُهُۥ عَلَى ٱللَّهِۗ وَكَانَ ٱللَّهُ غَفُورٗا رَّحِيمٗا

Na yeyote anayehama katika njia ya Allah atapata faida nyingi ardhini na ukunjufu. Na yeyote anayetoka nyumbani kwake akahama kwa ajili ya Allah na Mtume wake, kisha kifo kikamfika, hakika ujira wake umeshathibiti kwa Allah. Na Allah ni Mwingi wa kusamehe, Mwenye kurehemu



Sura: ANNISAI 

Aya : 101

وَإِذَا ضَرَبۡتُمۡ فِي ٱلۡأَرۡضِ فَلَيۡسَ عَلَيۡكُمۡ جُنَاحٌ أَن تَقۡصُرُواْ مِنَ ٱلصَّلَوٰةِ إِنۡ خِفۡتُمۡ أَن يَفۡتِنَكُمُ ٱلَّذِينَ كَفَرُوٓاْۚ إِنَّ ٱلۡكَٰفِرِينَ كَانُواْ لَكُمۡ عَدُوّٗا مُّبِينٗا

Na mnaposafiri ardhini[1], basi hakuna ubaya wowote kwenu kupunguza Swala[2] ikiwa mtahofia kupata mitihani ya makafiri (kwa kukudhuruni). Hakika makafiri wamekuwa maadui wa dhahiri kwenu


1- - Hapa imetajwa kusafiri ardhini kwa sababu sehemu kubwa ya usafiri kwa wakati Qur’ani inashuka ilikuwa kwa njia ya ardhini na majini. Ama ruhusa hii inahusu pia usafiri wa anga abao umeshamiri hivi sasa.


2- - Swala zinazokusudiwa kupunguzwa hapa ni zile zenye rakaa nne. Zinapunguzwa na kuswaliwa rakaa mbili. Swala hizo ni Adhuhuri, Alasiri na Isha.


Sura: ANNISAI 

Aya : 102

وَإِذَا كُنتَ فِيهِمۡ فَأَقَمۡتَ لَهُمُ ٱلصَّلَوٰةَ فَلۡتَقُمۡ طَآئِفَةٞ مِّنۡهُم مَّعَكَ وَلۡيَأۡخُذُوٓاْ أَسۡلِحَتَهُمۡۖ فَإِذَا سَجَدُواْ فَلۡيَكُونُواْ مِن وَرَآئِكُمۡ وَلۡتَأۡتِ طَآئِفَةٌ أُخۡرَىٰ لَمۡ يُصَلُّواْ فَلۡيُصَلُّواْ مَعَكَ وَلۡيَأۡخُذُواْ حِذۡرَهُمۡ وَأَسۡلِحَتَهُمۡۗ وَدَّ ٱلَّذِينَ كَفَرُواْ لَوۡ تَغۡفُلُونَ عَنۡ أَسۡلِحَتِكُمۡ وَأَمۡتِعَتِكُمۡ فَيَمِيلُونَ عَلَيۡكُم مَّيۡلَةٗ وَٰحِدَةٗۚ وَلَا جُنَاحَ عَلَيۡكُمۡ إِن كَانَ بِكُمۡ أَذٗى مِّن مَّطَرٍ أَوۡ كُنتُم مَّرۡضَىٰٓ أَن تَضَعُوٓاْ أَسۡلِحَتَكُمۡۖ وَخُذُواْ حِذۡرَكُمۡۗ إِنَّ ٱللَّهَ أَعَدَّ لِلۡكَٰفِرِينَ عَذَابٗا مُّهِينٗا

Na unapokuwa nao ukawa-simamishia Swala, basi lisimame kundi miongoni mwao pamoja nawe, na washike silaha zao. Wanaposujudu, (walioshika silaha) wawe nyuma yenu. Na (likimaliza kundi hili) lije kundi jingine ambalo halijaswali liswali pamoja na wewe na wachukue tahadhari zao na silaha zao. Waliokufuru wanapenda lau mngesahau silaha zenu na mizigo yenu ili wakushukieni (wakushambulieni kwa) shambulio moja tu (na kukumalizeni). Na hakuna ubaya wowote kwenu, kama mtakuwa katika hali ya udhia utokanao na mvua au mkiwa wagonjwa kutochukua silaha zenu. Na chukueni tahadhari zenu. Hakika Allah amewaandalia makafiri adhabu yenye kudhalilisha



Sura: ANNISAI 

Aya : 103

فَإِذَا قَضَيۡتُمُ ٱلصَّلَوٰةَ فَٱذۡكُرُواْ ٱللَّهَ قِيَٰمٗا وَقُعُودٗا وَعَلَىٰ جُنُوبِكُمۡۚ فَإِذَا ٱطۡمَأۡنَنتُمۡ فَأَقِيمُواْ ٱلصَّلَوٰةَۚ إِنَّ ٱلصَّلَوٰةَ كَانَتۡ عَلَى ٱلۡمُؤۡمِنِينَ كِتَٰبٗا مَّوۡقُوتٗا

Mmalizapo kuswali basi mtajeni Allah mkiwa mmesimama na mkiwa mmekaa na mkiwa mmejilaza ubavu. Mnapokuwa katika utulivu (amani), basi simamisheni Swala (kwa ukamilifu na bila ya kupunguza). Kwa hakika, Swala kwa Waislamu ni jambo liliofaradhishwa, lililowekewa wakati maaulumu



Sura: ANNISAI 

Aya : 104

وَلَا تَهِنُواْ فِي ٱبۡتِغَآءِ ٱلۡقَوۡمِۖ إِن تَكُونُواْ تَأۡلَمُونَ فَإِنَّهُمۡ يَأۡلَمُونَ كَمَا تَأۡلَمُونَۖ وَتَرۡجُونَ مِنَ ٱللَّهِ مَا لَا يَرۡجُونَۗ وَكَانَ ٱللَّهُ عَلِيمًا حَكِيمًا

Na msiwe dhaifu katika kuwasaka jamaa (ambao ni maadui wenu). Ikiwa nyinyi mnaumia (katika mapambano) kwa hakika wao pia wanaumia kama mnavyoumia nyinyi, na nyinyi mnataraji kwa Allah kitu ambacho wao hawakitaraji, na Allah ni Mjuzi sana, Mwenye hekima nyingi



Sura: ANNISAI 

Aya : 105

إِنَّآ أَنزَلۡنَآ إِلَيۡكَ ٱلۡكِتَٰبَ بِٱلۡحَقِّ لِتَحۡكُمَ بَيۡنَ ٱلنَّاسِ بِمَآ أَرَىٰكَ ٱللَّهُۚ وَلَا تَكُن لِّلۡخَآئِنِينَ خَصِيمٗا

Hakika, sisi tumekuteremshia kitabu kwa haki ili uhukumu baina ya watu kwa kile ambacho Allah amekuonyesha (amekuelimisha). Na usiwe mtetezi wa wanaofanya khiana



Sura: ANNISAI 

Aya : 106

وَٱسۡتَغۡفِرِ ٱللَّهَۖ إِنَّ ٱللَّهَ كَانَ غَفُورٗا رَّحِيمٗا

Na muombe msamaha Allah. Hakika Allah ni Msamehevu sana, Mwenye kurehem



Sura: ANNISAI 

Aya : 107

وَلَا تُجَٰدِلۡ عَنِ ٱلَّذِينَ يَخۡتَانُونَ أَنفُسَهُمۡۚ إِنَّ ٱللَّهَ لَا يُحِبُّ مَن كَانَ خَوَّانًا أَثِيمٗا

Na usiwatetee wale wanaozi-fanyia khiana nafsi zao (kwa kutenda dhambi na makosa mbali mbali). Hakika Allah hampendi (mtu) mwenye khiana, mwenye dhambi



Sura: ANNISAI 

Aya : 108

يَسۡتَخۡفُونَ مِنَ ٱلنَّاسِ وَلَا يَسۡتَخۡفُونَ مِنَ ٱللَّهِ وَهُوَ مَعَهُمۡ إِذۡ يُبَيِّتُونَ مَا لَا يَرۡضَىٰ مِنَ ٱلۡقَوۡلِۚ وَكَانَ ٱللَّهُ بِمَا يَعۡمَلُونَ مُحِيطًا

Wanajificha wasionekane na watu na wala hawamstahi Allah kuwaona (wanapofanya dhambi) ilhali yeye yuko pamoja nao wakati wanapopanga njama usiku za (kusema) kauli zisizoridhiwa (na Allah). Na Allah anayajua vilivyo yote wayafanyayo



Sura: ANNISAI 

Aya : 109

هَـٰٓأَنتُمۡ هَـٰٓؤُلَآءِ جَٰدَلۡتُمۡ عَنۡهُمۡ فِي ٱلۡحَيَوٰةِ ٱلدُّنۡيَا فَمَن يُجَٰدِلُ ٱللَّهَ عَنۡهُمۡ يَوۡمَ ٱلۡقِيَٰمَةِ أَم مَّن يَكُونُ عَلَيۡهِمۡ وَكِيلٗا

Ee! Nyinyi hawa mmewatetea katika maisha ya kidunia. Basi ni nani atakayejadiliana na Allah Siku ya Kiama akiwatetea au ni nani atakayekuwa wakili wao?



Sura: ANNISAI 

Aya : 110

وَمَن يَعۡمَلۡ سُوٓءًا أَوۡ يَظۡلِمۡ نَفۡسَهُۥ ثُمَّ يَسۡتَغۡفِرِ ٱللَّهَ يَجِدِ ٱللَّهَ غَفُورٗا رَّحِيمٗا

Na yeyote mwenye kutenda baya au kudhulumu nafsi yake, kisha akamuomba msamaha Allah, atamkuta Allah ni Msamehevu sana, Mwenye kurehem



Sura: ANNISAI 

Aya : 111

وَمَن يَكۡسِبۡ إِثۡمٗا فَإِنَّمَا يَكۡسِبُهُۥ عَلَىٰ نَفۡسِهِۦۚ وَكَانَ ٱللَّهُ عَلِيمًا حَكِيمٗا

Na yeyote anayechuma dhambi, basi hakika anazichuma kwa (kuidhuru) nafsi yake. Na Allah ni Mjuzi mno, Mwenye hekima nyingi



Sura: ANNISAI 

Aya : 112

وَمَن يَكۡسِبۡ خَطِيٓـَٔةً أَوۡ إِثۡمٗا ثُمَّ يَرۡمِ بِهِۦ بَرِيٓـٔٗا فَقَدِ ٱحۡتَمَلَ بُهۡتَٰنٗا وَإِثۡمٗا مُّبِينٗا

Na yeyote anayetenda kosa au dhambi kisha akamsingizia asiyekuwa na hatia, basi hakika amebeba uzushi na dhambi inayobainisha (uovu wake)



Sura: ANNISAI 

Aya : 113

وَلَوۡلَا فَضۡلُ ٱللَّهِ عَلَيۡكَ وَرَحۡمَتُهُۥ لَهَمَّت طَّآئِفَةٞ مِّنۡهُمۡ أَن يُضِلُّوكَ وَمَا يُضِلُّونَ إِلَّآ أَنفُسَهُمۡۖ وَمَا يَضُرُّونَكَ مِن شَيۡءٖۚ وَأَنزَلَ ٱللَّهُ عَلَيۡكَ ٱلۡكِتَٰبَ وَٱلۡحِكۡمَةَ وَعَلَّمَكَ مَا لَمۡ تَكُن تَعۡلَمُۚ وَكَانَ فَضۡلُ ٱللَّهِ عَلَيۡكَ عَظِيمٗا

Na lau kama si hisani ya Allah na rehema zake kwako basi kwa yakini kabisa kundi miongoni mwao lilikusudia kukupotosha. Na hawapotoshi ispokuwa nafsi zao tu na hawatakudhuru chochote. Na Allah amekuteremshia kitabu (Qur’an) na hekima, na amekufundisha uliyokuwa huyajui. Na hisani ya Allah kwako ni kubwa sana



Sura: ANNISAI 

Aya : 114

۞لَّا خَيۡرَ فِي كَثِيرٖ مِّن نَّجۡوَىٰهُمۡ إِلَّا مَنۡ أَمَرَ بِصَدَقَةٍ أَوۡ مَعۡرُوفٍ أَوۡ إِصۡلَٰحِۭ بَيۡنَ ٱلنَّاسِۚ وَمَن يَفۡعَلۡ ذَٰلِكَ ٱبۡتِغَآءَ مَرۡضَاتِ ٱللَّهِ فَسَوۡفَ نُؤۡتِيهِ أَجۡرًا عَظِيمٗا

Hakuna kheri yoyote katika minong’ono yao mingi isipokuwa tu kwa yule anayeamrisha (kutoa) sadaka au (kutenda) jema au kupatanisha watu. Na yeyote atakayefanya hayo kwa kutaka radhi za Allah basi tutampa malipo makubwa kabisa



Sura: ANNISAI 

Aya : 115

وَمَن يُشَاقِقِ ٱلرَّسُولَ مِنۢ بَعۡدِ مَا تَبَيَّنَ لَهُ ٱلۡهُدَىٰ وَيَتَّبِعۡ غَيۡرَ سَبِيلِ ٱلۡمُؤۡمِنِينَ نُوَلِّهِۦ مَا تَوَلَّىٰ وَنُصۡلِهِۦ جَهَنَّمَۖ وَسَآءَتۡ مَصِيرًا

Na yeyote anayempinga Mtume baada ya kumdhihirikia uongofu na akafuata njia isiyokuwa ya Waumini, basi tutamuelekeza huko alikoelekea, na tutamuingiza katika Jahanamu, na hayo ndio marejeo mabaya kabisa



Sura: ANNISAI 

Aya : 116

إِنَّ ٱللَّهَ لَا يَغۡفِرُ أَن يُشۡرَكَ بِهِۦ وَيَغۡفِرُ مَا دُونَ ذَٰلِكَ لِمَن يَشَآءُۚ وَمَن يُشۡرِكۡ بِٱللَّهِ فَقَدۡ ضَلَّ ضَلَٰلَۢا بَعِيدًا

Hakika, Allah hatoi msamaha (wa dhambi ya) kushirikishwa, na anasamehe (dhambi) zilizo chini ya hiyo kwa amtakaye. Na yeyote anayemfanyia ushirika Allah kwa hakika amepotea upotevu ulio mbali kabisa (na haki)



Sura: ANNISAI 

Aya : 117

إِن يَدۡعُونَ مِن دُونِهِۦٓ إِلَّآ إِنَٰثٗا وَإِن يَدۡعُونَ إِلَّا شَيۡطَٰنٗا مَّرِيدٗا

Hawaombi (hawaabudu) badala yake isipokuwa tu wanawake (masanamu)[1], na hawamuombi isipokuwa shetani (Ibilisi) aliyechupa mipaka (katika uasi)


1- - Masanamu hapa yameitwa wanawake sio kwa lengo la kudhalilisha wanawake lakini ni kunukuu hali halisi ya masanamu hayo kwa mujibu wa makafiri wenyewe waliyoyatengeneza. Wanachuoni wametoa ufafanuzi kwamba, masanamu hapa yameitwa wanawake kwa tafsiri mbili.
1. Tafsiri ya kwanza ni kwamba makafiri waliyapa masanamu yao majina ya kike, kama vile Lata, Uza, Manata n.k.
2. Tafsiri ya pili ni kwamba masanamu yameitwa wanawake kwa sababu ya udhaifu wake wa kutoweza kujihami kama ilivyo kwa wanawake.


Sura: ANNISAI 

Aya : 118

لَّعَنَهُ ٱللَّهُۘ وَقَالَ لَأَتَّخِذَنَّ مِنۡ عِبَادِكَ نَصِيبٗا مَّفۡرُوضٗا

Allah amemlaani (shetani). Na amesema (baada ya kulaaniwa): Kwa yakini kabisa, nitachukua katika waja wako fungu lililokadiriwa



Sura: ANNISAI 

Aya : 119

وَلَأُضِلَّنَّهُمۡ وَلَأُمَنِّيَنَّهُمۡ وَلَأٓمُرَنَّهُمۡ فَلَيُبَتِّكُنَّ ءَاذَانَ ٱلۡأَنۡعَٰمِ وَلَأٓمُرَنَّهُمۡ فَلَيُغَيِّرُنَّ خَلۡقَ ٱللَّهِۚ وَمَن يَتَّخِذِ ٱلشَّيۡطَٰنَ وَلِيّٗا مِّن دُونِ ٱللَّهِ فَقَدۡ خَسِرَ خُسۡرَانٗا مُّبِينٗا

Na kwa hakika kabisa, nitawa-poteza na nitawatia matumaini na nitawaamrisha wakate masikio ya wanyama[1], na nitawaamrisha (na) watabadilisha maumbile aliyoyaumba Allah. Na yeyote atakayemfanya shetani mlinzi (wake) badala ya Allah hakika amehasirika hasara inayodhihirisha (uovu wao)


1- - Ukataji wa masikio ya wanyama unaokatazwa hapa ni ule unaombatana na uharibifu na itikadi potofu. Ama utoboaji au upasuaji wa uwekaji wa alama za utambuzi haukatazwi.


Sura: ANNISAI 

Aya : 120

يَعِدُهُمۡ وَيُمَنِّيهِمۡۖ وَمَا يَعِدُهُمُ ٱلشَّيۡطَٰنُ إِلَّا غُرُورًا

(Shetani) Anawaahidi na anawatumainisha. Na hakuna anachowaahidi shetani isipokuwa hadaa tu