Sura: AL-AN’AAM 

Aya : 61

وَهُوَ ٱلۡقَاهِرُ فَوۡقَ عِبَادِهِۦۖ وَيُرۡسِلُ عَلَيۡكُمۡ حَفَظَةً حَتَّىٰٓ إِذَا جَآءَ أَحَدَكُمُ ٱلۡمَوۡتُ تَوَفَّتۡهُ رُسُلُنَا وَهُمۡ لَا يُفَرِّطُونَ

Na yeye tu ndiye Mwenye nguvu kubwa juu ya waja wake, na anatuma kwenu (Malaika) waangalizi (wanaowalinda binadamu na kutunza kumbukumbu za matendo yao)[1], mpaka kinapomfikia mmoja wenu kifo wajumbe wetu wanamfisha, na hawafanyi uzembe


1- - Rejea Aya ya 11, Sura Arraad (13).


Sura: AL-AN’AAM 

Aya : 62

ثُمَّ رُدُّوٓاْ إِلَى ٱللَّهِ مَوۡلَىٰهُمُ ٱلۡحَقِّۚ أَلَا لَهُ ٱلۡحُكۡمُ وَهُوَ أَسۡرَعُ ٱلۡحَٰسِبِينَ

Kisha watarudishwa kwa Allah, Mola wao wa haki. Ehee, elewa kwamba, hukumu ni yake yeye (Allah) tu, na yeye ni Mwepesi sana wa wanaohesabu



Sura: AL-AN’AAM 

Aya : 63

قُلۡ مَن يُنَجِّيكُم مِّن ظُلُمَٰتِ ٱلۡبَرِّ وَٱلۡبَحۡرِ تَدۡعُونَهُۥ تَضَرُّعٗا وَخُفۡيَةٗ لَّئِنۡ أَنجَىٰنَا مِنۡ هَٰذِهِۦ لَنَكُونَنَّ مِنَ ٱلشَّـٰكِرِينَ

Sema: Ni nani anayekuokoeni katika giza la bara na baharini? Mnamuomba kwa unyenyekevu na kwa siri, (mkisema kwamba:) Endapo (Allah) atatuokoa kwenye haya kwa hakika kabisa tutakuwa miongoni mwa wenye kushukuru



Sura: AL-AN’AAM 

Aya : 64

قُلِ ٱللَّهُ يُنَجِّيكُم مِّنۡهَا وَمِن كُلِّ كَرۡبٖ ثُمَّ أَنتُمۡ تُشۡرِكُونَ

Sema: Allah anakuokoeni kwenye hayo na kwenye kila janga, kisha nyinyi mnafanya ushirikina!



Sura: AL-AN’AAM 

Aya : 65

قُلۡ هُوَ ٱلۡقَادِرُ عَلَىٰٓ أَن يَبۡعَثَ عَلَيۡكُمۡ عَذَابٗا مِّن فَوۡقِكُمۡ أَوۡ مِن تَحۡتِ أَرۡجُلِكُمۡ أَوۡ يَلۡبِسَكُمۡ شِيَعٗا وَيُذِيقَ بَعۡضَكُم بَأۡسَ بَعۡضٍۗ ٱنظُرۡ كَيۡفَ نُصَرِّفُ ٱلۡأٓيَٰتِ لَعَلَّهُمۡ يَفۡقَهُونَ

Sema: Yeye tu ndiye Muweza wa kuleta kwenu adhabu itokayo juu yenu au chini ya miguu yenu, au kukuvalisheni nguo ya mfarakano wa makundi na kukuonjesheni mkong’oto wa (nguvu za) wengine. Ona, namna tunavyozifafanua Aya (hoja) ili wapate kufahamu



Sura: AL-AN’AAM 

Aya : 66

وَكَذَّبَ بِهِۦ قَوۡمُكَ وَهُوَ ٱلۡحَقُّۚ قُل لَّسۡتُ عَلَيۡكُم بِوَكِيلٖ

Na watu wako wameikanusha (Qur’ani), na ilhali ndio haki. Sema: Mimi sio mtetezi wenu (lakini mimi ni muonyaji)



Sura: AL-AN’AAM 

Aya : 67

لِّكُلِّ نَبَإٖ مُّسۡتَقَرّٞۚ وَسَوۡفَ تَعۡلَمُونَ

Kila habari ina sehemu yake (maalumu), na punde tu mtajua



Sura: AL-AN’AAM 

Aya : 68

وَإِذَا رَأَيۡتَ ٱلَّذِينَ يَخُوضُونَ فِيٓ ءَايَٰتِنَا فَأَعۡرِضۡ عَنۡهُمۡ حَتَّىٰ يَخُوضُواْ فِي حَدِيثٍ غَيۡرِهِۦۚ وَإِمَّا يُنسِيَنَّكَ ٱلشَّيۡطَٰنُ فَلَا تَقۡعُدۡ بَعۡدَ ٱلذِّكۡرَىٰ مَعَ ٱلۡقَوۡمِ ٱلظَّـٰلِمِينَ

Na utakapowaona wanaozizungumza vibaya Aya zetu, basi wapuuze (na jitenge nao) hadi waingie katika mazungumzo mengine. Na kama shetani atakusahaulisha, basi baada ya kukumbushwa usikae pamoja na watu madhalimu.[1]


1- - Aya hii inawataka Waislamu wahakikishe kuwa maandiko ya dini yao yanaheshimiwa. Pale watakapo ona yanakejiliwa, yanachezewa, yanabezwa au kupotoshwa wasikae kimya bali wakemee na ikibidi waondoke sehemu inapofanyika kejeli hiyo.


Sura: AL-AN’AAM 

Aya : 69

وَمَا عَلَى ٱلَّذِينَ يَتَّقُونَ مِنۡ حِسَابِهِم مِّن شَيۡءٖ وَلَٰكِن ذِكۡرَىٰ لَعَلَّهُمۡ يَتَّقُونَ

Na wale wanaomcha Allah hawana dhambi yoyote katika dhambi zao (watapojitenga nao), lakini (huu) ni ukumbusho tu, ili waogope



Sura: AL-AN’AAM 

Aya : 70

وَذَرِ ٱلَّذِينَ ٱتَّخَذُواْ دِينَهُمۡ لَعِبٗا وَلَهۡوٗا وَغَرَّتۡهُمُ ٱلۡحَيَوٰةُ ٱلدُّنۡيَاۚ وَذَكِّرۡ بِهِۦٓ أَن تُبۡسَلَ نَفۡسُۢ بِمَا كَسَبَتۡ لَيۡسَ لَهَا مِن دُونِ ٱللَّهِ وَلِيّٞ وَلَا شَفِيعٞ وَإِن تَعۡدِلۡ كُلَّ عَدۡلٖ لَّا يُؤۡخَذۡ مِنۡهَآۗ أُوْلَـٰٓئِكَ ٱلَّذِينَ أُبۡسِلُواْ بِمَا كَسَبُواْۖ لَهُمۡ شَرَابٞ مِّنۡ حَمِيمٖ وَعَذَابٌ أَلِيمُۢ بِمَا كَانُواْ يَكۡفُرُونَ

Na waache wale walioifanya dini yao mchezo na pumbao, na yamewahadaa maisha ya dunia. Na kumbusha kwayo (Qur’ani ili), isije nafsi ikaangamizwa kwasababu ya (madhambi) waliyoyachuma, haina mlinzi yeyote wala muombezi yeyote. Na hata kama (nafsi hiyo) itatoa fidia ya aina yoyote (ili isiadhibiwe) haitachukuliwa. Hao ndio wale walioangamizwa kwa (sababu ya madhambi) waliyoyachuma. Watapata kinywaji cha maji ya moto na adhabu iumizayo sana kwa (sababu) ya walivyokuwa wanakufuru



Sura: AL-AN’AAM 

Aya : 71

قُلۡ أَنَدۡعُواْ مِن دُونِ ٱللَّهِ مَا لَا يَنفَعُنَا وَلَا يَضُرُّنَا وَنُرَدُّ عَلَىٰٓ أَعۡقَابِنَا بَعۡدَ إِذۡ هَدَىٰنَا ٱللَّهُ كَٱلَّذِي ٱسۡتَهۡوَتۡهُ ٱلشَّيَٰطِينُ فِي ٱلۡأَرۡضِ حَيۡرَانَ لَهُۥٓ أَصۡحَٰبٞ يَدۡعُونَهُۥٓ إِلَى ٱلۡهُدَى ٱئۡتِنَاۗ قُلۡ إِنَّ هُدَى ٱللَّهِ هُوَ ٱلۡهُدَىٰۖ وَأُمِرۡنَا لِنُسۡلِمَ لِرَبِّ ٱلۡعَٰلَمِينَ

Sema: Hivi tuwaombe (tuwaa-budu) badala ya Allah (Miungu) ambao hawatunufaishi na hawatudhuru na turudishwe nyuma (kwenye itikadi potofu tulizokwisha ziacha) baada ya Allah kutuongoa kama yule ambaye mashetani wamempagawisha katika ardhi, akiduwaa, akiwa na marafiki wanaomuita aende katika uongofu (wakimwambia): Njoo kwetu?[1] Sema: Hakika, muongozo wa Allah ndio uongofu, na tumeamrishwa tujisalimishe kwa Mola Mlezi wa walimwengu wote


1- - Aya hapa inamtaka Muumini kuwa na msimamo imara na thabiti katika Imani na itikadi yake. Hatakiwi kuyumba au kuyumbishwa. Sio kila analolisikia au kuliona au kushawishiwa alifuate.


Sura: AL-AN’AAM 

Aya : 72

وَأَنۡ أَقِيمُواْ ٱلصَّلَوٰةَ وَٱتَّقُوهُۚ وَهُوَ ٱلَّذِيٓ إِلَيۡهِ تُحۡشَرُونَ

Na (tumeamrishwa kwamba): Simamisheni Swala, na mumche yeye (Allah), na yeye ndiye ambaye kwake tu ndiko mtakapokusanywa



Sura: AL-AN’AAM 

Aya : 73

وَهُوَ ٱلَّذِي خَلَقَ ٱلسَّمَٰوَٰتِ وَٱلۡأَرۡضَ بِٱلۡحَقِّۖ وَيَوۡمَ يَقُولُ كُن فَيَكُونُۚ قَوۡلُهُ ٱلۡحَقُّۚ وَلَهُ ٱلۡمُلۡكُ يَوۡمَ يُنفَخُ فِي ٱلصُّورِۚ عَٰلِمُ ٱلۡغَيۡبِ وَٱلشَّهَٰدَةِۚ وَهُوَ ٱلۡحَكِيمُ ٱلۡخَبِيرُ

Na yeye ndiye aliyeumba mbingu na ardhi kwa haki. Na (kumbuka) siku (Allah) anaposema (kuliambia jambo): Kuwa, basi linakuwa. Kauli yake ni haki. Ni wake yeye tu ufalme siku litakapopulizwa baragumu. Ni mjuzi wa Ghaibu (yaliyofichika) na yaliyo bayana. Na yeye ni Mwenye hekima, Mjuzi wa habari (zote)



Sura: AL-AN’AAM 

Aya : 74

۞وَإِذۡ قَالَ إِبۡرَٰهِيمُ لِأَبِيهِ ءَازَرَ أَتَتَّخِذُ أَصۡنَامًا ءَالِهَةً إِنِّيٓ أَرَىٰكَ وَقَوۡمَكَ فِي ضَلَٰلٖ مُّبِينٖ

Na (kumbuka Mtume) Ibrahimu alipomwambia baba yake Azar (kwamba): Hivi unayafanya masanamu Miungu? Hakika, mimi ninakuona wewe na watu wako kwamba mmo katika upotevu ulio wazi



Sura: AL-AN’AAM 

Aya : 75

وَكَذَٰلِكَ نُرِيٓ إِبۡرَٰهِيمَ مَلَكُوتَ ٱلسَّمَٰوَٰتِ وَٱلۡأَرۡضِ وَلِيَكُونَ مِنَ ٱلۡمُوقِنِينَ

Na kama hivyo tunamuonyesha Ibrahimu ufalme wa mbinguni na ardhini, na ili awe miongoni mwa wenye yakini



Sura: AL-AN’AAM 

Aya : 76

فَلَمَّا جَنَّ عَلَيۡهِ ٱلَّيۡلُ رَءَا كَوۡكَبٗاۖ قَالَ هَٰذَا رَبِّيۖ فَلَمَّآ أَفَلَ قَالَ لَآ أُحِبُّ ٱلۡأٓفِلِينَ

Basi (Mtume Ibrahimu) ulipomjia usiku aliona nyota (na) akasema: Huyu ni Mola wangu Mlezi. (Nyota) Ilipozama alisema: Siwapendi wanaopotea



Sura: AL-AN’AAM 

Aya : 77

فَلَمَّا رَءَا ٱلۡقَمَرَ بَازِغٗا قَالَ هَٰذَا رَبِّيۖ فَلَمَّآ أَفَلَ قَالَ لَئِن لَّمۡ يَهۡدِنِي رَبِّي لَأَكُونَنَّ مِنَ ٱلۡقَوۡمِ ٱلضَّآلِّينَ

Na alipoona mwezi umechomoza alisema: Huyu ni Mola wangu Mlezi. Na (mwezi) ulipozama alisema: Kama Mola wangu hataniongoza, kwa hakika kabisa nitakuwa miongoni mwa watu waliopotea



Sura: AL-AN’AAM 

Aya : 78

فَلَمَّا رَءَا ٱلشَّمۡسَ بَازِغَةٗ قَالَ هَٰذَا رَبِّي هَٰذَآ أَكۡبَرُۖ فَلَمَّآ أَفَلَتۡ قَالَ يَٰقَوۡمِ إِنِّي بَرِيٓءٞ مِّمَّا تُشۡرِكُونَ

Na alipoliona jua limechomoza alisema: Huyu ni Mola wangu. Huyu ni mkubwa zaidi (kuliko wote). Basi (jua) lilipozama, alisema: Enyi watu wangu, mimi najitenga mbali na (Miungu yote) mnayoshirikisha (na Allah).[1]


1- - Nabii Ibrahimu katika mdahalo huu aliofanya na watu wake hakumaanisha kwamba na yeye aliamini kuwa nyota, mwezi na jua ni Miungu kama walivyoamini. Alichofanya ni maelekezo aliyopewa na Allah kama ilivyoelezwa katika Aya ya 83 ya Sura hii. Pia hiyo ni aina fulani ya mbinu za ufundishaji ya kujifanya unayemfundisha uko pamoja naye ili ufike naye kwenye ukweli na autambue kwa kutumia hoja, akili na mazingira. Nabii Ibrahimu hakuwa Mshirikishaji bali alikuwa Muumini safi anayemuamini na kumuabudu Allah tu. Rejea Aya 120-123 ya Sura Annahli (16).


Sura: AL-AN’AAM 

Aya : 79

إِنِّي وَجَّهۡتُ وَجۡهِيَ لِلَّذِي فَطَرَ ٱلسَّمَٰوَٰتِ وَٱلۡأَرۡضَ حَنِيفٗاۖ وَمَآ أَنَا۠ مِنَ ٱلۡمُشۡرِكِينَ

Hakika, mimi nimeelekeza uso wangu kwa (Allah) aliyeumba mbingu na ardhi, nikiacha itikadi zote potofu, na mimi si miongoni mwa washirikina



Sura: AL-AN’AAM 

Aya : 80

وَحَآجَّهُۥ قَوۡمُهُۥۚ قَالَ أَتُحَـٰٓجُّوٓنِّي فِي ٱللَّهِ وَقَدۡ هَدَىٰنِۚ وَلَآ أَخَافُ مَا تُشۡرِكُونَ بِهِۦٓ إِلَّآ أَن يَشَآءَ رَبِّي شَيۡـٔٗاۚ وَسِعَ رَبِّي كُلَّ شَيۡءٍ عِلۡمًاۚ أَفَلَا تَتَذَكَّرُونَ

Na watu wake wakamuwekea mdahalo. Alisema: Hivi, mnanihoji kuhusu Allah, na ilhali ameniongoa? Na siwaogopi hao mnaowashirikisha naye, isipokuwa kama Mola wangu atapenda jambo lolote (linipate). Mola wangu anajua kila kitu kwa mapana na marefu. Hivi hamuonyeki (na haya ninayokuambieni)?



Sura: AL-AN’AAM 

Aya : 81

وَكَيۡفَ أَخَافُ مَآ أَشۡرَكۡتُمۡ وَلَا تَخَافُونَ أَنَّكُمۡ أَشۡرَكۡتُم بِٱللَّهِ مَا لَمۡ يُنَزِّلۡ بِهِۦ عَلَيۡكُمۡ سُلۡطَٰنٗاۚ فَأَيُّ ٱلۡفَرِيقَيۡنِ أَحَقُّ بِٱلۡأَمۡنِۖ إِن كُنتُمۡ تَعۡلَمُونَ

Na vipi niwaogope wale (Miungu bandia) mliowashirikisha (na Allah) na ilhali nyinyi hamuogopi kwamba mmemshirikisha Allah na vitu ambavyo hakukuteremshieni hoja (yoyote)? Basi ni kundi lipi lililo na haki zaidi ya kuwa katika amani kati ya makundi mawili (ya mimi na nyinyi) ikiwa (kweli) mnajua?



Sura: AL-AN’AAM 

Aya : 82

ٱلَّذِينَ ءَامَنُواْ وَلَمۡ يَلۡبِسُوٓاْ إِيمَٰنَهُم بِظُلۡمٍ أُوْلَـٰٓئِكَ لَهُمُ ٱلۡأَمۡنُ وَهُم مُّهۡتَدُونَ

Wale walioamini na imani zao hawakuzichanganya na dhuluma (ushirikina), hao ndio wenye amani na hao ndio waongofu



Sura: AL-AN’AAM 

Aya : 83

وَتِلۡكَ حُجَّتُنَآ ءَاتَيۡنَٰهَآ إِبۡرَٰهِيمَ عَلَىٰ قَوۡمِهِۦۚ نَرۡفَعُ دَرَجَٰتٖ مَّن نَّشَآءُۗ إِنَّ رَبَّكَ حَكِيمٌ عَلِيمٞ

Na hizo ndio hoja zetu tulizompa (Mtume) Ibrahimu ajadiliane na watu wake[1]. Tunampandisha vyeo tumtakae. Hakika, Mola wako ni Mwenye hekima sana, Mjuzi mno


1- - Hapa Aya inathibitisha kuwa, mdahalo wa Nabii Ibrahimu na watu ni maelekezo ya Allah na hoja zote na mpangilio mzima ameelekezwa na Mola wake.


Sura: AL-AN’AAM 

Aya : 84

وَوَهَبۡنَا لَهُۥٓ إِسۡحَٰقَ وَيَعۡقُوبَۚ كُلًّا هَدَيۡنَاۚ وَنُوحًا هَدَيۡنَا مِن قَبۡلُۖ وَمِن ذُرِّيَّتِهِۦ دَاوُۥدَ وَسُلَيۡمَٰنَ وَأَيُّوبَ وَيُوسُفَ وَمُوسَىٰ وَهَٰرُونَۚ وَكَذَٰلِكَ نَجۡزِي ٱلۡمُحۡسِنِينَ

Na tulimtunuku (Mtume Ibrahimu) Isihaka na Yakubu. Wote tuliwaongoa. Na Nuhu tulimuongoa kabla (yao). Na katika kizazi chake tulimongoa Daudi na Suleimani na Ayubu na Yusufu na Mussa na Haruna. Na kama hivyo tunawalipa wafanyao mazuri



Sura: AL-AN’AAM 

Aya : 85

وَزَكَرِيَّا وَيَحۡيَىٰ وَعِيسَىٰ وَإِلۡيَاسَۖ كُلّٞ مِّنَ ٱلصَّـٰلِحِينَ

Na Zakaria na Yahaya na Issa na Iliasa. Wote ni miongoni mwa watu wema



Sura: AL-AN’AAM 

Aya : 86

وَإِسۡمَٰعِيلَ وَٱلۡيَسَعَ وَيُونُسَ وَلُوطٗاۚ وَكُلّٗا فَضَّلۡنَا عَلَى ٱلۡعَٰلَمِينَ

Na Ismaili na Alyasaa na Yunus na Lutwi. Na wote (hao) tumewafanya bora kuliko walimwengu (wengine wa zama zao)



Sura: AL-AN’AAM 

Aya : 87

وَمِنۡ ءَابَآئِهِمۡ وَذُرِّيَّـٰتِهِمۡ وَإِخۡوَٰنِهِمۡۖ وَٱجۡتَبَيۡنَٰهُمۡ وَهَدَيۡنَٰهُمۡ إِلَىٰ صِرَٰطٖ مُّسۡتَقِيمٖ

Na katika baba zao na watoto wao na ndugu zao. Na tuliwateua na tuliwaongoza njia iliyo nyooka



Sura: AL-AN’AAM 

Aya : 88

ذَٰلِكَ هُدَى ٱللَّهِ يَهۡدِي بِهِۦ مَن يَشَآءُ مِنۡ عِبَادِهِۦۚ وَلَوۡ أَشۡرَكُواْ لَحَبِطَ عَنۡهُم مَّا كَانُواْ يَعۡمَلُونَ

Huo ndio muongozo wa Allah, anamuongoa amtakaye katika waja wake. Na lau kama (Mitume) wangefanya ushirikina (wa kumshi-rikisha Allah na vitu vingine), yangewaharibikia (matendo) waliyokuwa wanayafanya



Sura: AL-AN’AAM 

Aya : 89

أُوْلَـٰٓئِكَ ٱلَّذِينَ ءَاتَيۡنَٰهُمُ ٱلۡكِتَٰبَ وَٱلۡحُكۡمَ وَٱلنُّبُوَّةَۚ فَإِن يَكۡفُرۡ بِهَا هَـٰٓؤُلَآءِ فَقَدۡ وَكَّلۡنَا بِهَا قَوۡمٗا لَّيۡسُواْ بِهَا بِكَٰفِرِينَ

Hao ndio tuliowapa vitabu na utawala na Utume. Endepo hawa (watu wa Makkah) watayakataa hayo, basi tumesha yawakilisha kwa watu (wengine) wasioyakataa (ambao ni Muhajirina na Answari)



Sura: AL-AN’AAM 

Aya : 90

أُوْلَـٰٓئِكَ ٱلَّذِينَ هَدَى ٱللَّهُۖ فَبِهُدَىٰهُمُ ٱقۡتَدِهۡۗ قُل لَّآ أَسۡـَٔلُكُمۡ عَلَيۡهِ أَجۡرًاۖ إِنۡ هُوَ إِلَّا ذِكۡرَىٰ لِلۡعَٰلَمِينَ

Hao ndio wale ambao Allah amewaongoa. Basi fuata muongozo wao[1]. Sema (uwaambie): Sikuombeni ujira wowote katika hilo (la kukufikishieni ujumbe wa Allah). Hayakuwa hayo (ninayokufikishieni) isipokuwa tu ni mawaidha kwa walimwengu wote


1- - Aya hapa inawaongoza Waumini kufuata muongozo wa viongozi wao. Iwapo kiongozi atakapotoka, utaachwa upotofu wake.