Sura: ANNISAI 

Aya : 31

إِن تَجۡتَنِبُواْ كَبَآئِرَ مَا تُنۡهَوۡنَ عَنۡهُ نُكَفِّرۡ عَنكُمۡ سَيِّـَٔاتِكُمۡ وَنُدۡخِلۡكُم مُّدۡخَلٗا كَرِيمٗا

Kama mtayaepuka madhambi makubwa mnayokatazwa, tutakufutieni makosa yenu, na tutakuingizeni mahali pa heshima



Sura: ANNISAI 

Aya : 32

وَلَا تَتَمَنَّوۡاْ مَا فَضَّلَ ٱللَّهُ بِهِۦ بَعۡضَكُمۡ عَلَىٰ بَعۡضٖۚ لِّلرِّجَالِ نَصِيبٞ مِّمَّا ٱكۡتَسَبُواْۖ وَلِلنِّسَآءِ نَصِيبٞ مِّمَّا ٱكۡتَسَبۡنَۚ وَسۡـَٔلُواْ ٱللَّهَ مِن فَضۡلِهِۦٓۚ إِنَّ ٱللَّهَ كَانَ بِكُلِّ شَيۡءٍ عَلِيمٗا

Na msitamani (kwa husuda) vile ambavyo Allah amewazidishia baadhi yenu kuliko wengine (katika riziki na vipaji). Wanaume wana fungu katika vile walivyochuma na wanawake wana fungu katika vile walivyochuma. Na muombeni Allah (awape) katika fadhila zake. Hakika, Allah ni Mjuzi wa kila kitu



Sura: ANNISAI 

Aya : 33

وَلِكُلّٖ جَعَلۡنَا مَوَٰلِيَ مِمَّا تَرَكَ ٱلۡوَٰلِدَانِ وَٱلۡأَقۡرَبُونَۚ وَٱلَّذِينَ عَقَدَتۡ أَيۡمَٰنُكُمۡ فَـَٔاتُوهُمۡ نَصِيبَهُمۡۚ إِنَّ ٱللَّهَ كَانَ عَلَىٰ كُلِّ شَيۡءٖ شَهِيدًا

Na kila mtu tumemuwekea warithi katika vile ambavyo vimeachwa na wazazi na ndugu. Na wale mliofunga nao mikataba ya viapo (kuwa mtakuwa ndugu) wapeni sehemu yao (ya mirathi)[1]. Hakika, Allah ni Shahidi wa kila kitu


1- - Aya hii inazungumzia udugu wa kupanga (udugu wa Yamini). Udugu huu ulikuwepo mwanzo wa Uislamu, na ndugu wa udugu huu walikuwa wakirithiana. Urithi huu ulifutwa na Aya 11 - 12 za Sura hii.


Sura: ANNISAI 

Aya : 34

ٱلرِّجَالُ قَوَّـٰمُونَ عَلَى ٱلنِّسَآءِ بِمَا فَضَّلَ ٱللَّهُ بَعۡضَهُمۡ عَلَىٰ بَعۡضٖ وَبِمَآ أَنفَقُواْ مِنۡ أَمۡوَٰلِهِمۡۚ فَٱلصَّـٰلِحَٰتُ قَٰنِتَٰتٌ حَٰفِظَٰتٞ لِّلۡغَيۡبِ بِمَا حَفِظَ ٱللَّهُۚ وَٱلَّـٰتِي تَخَافُونَ نُشُوزَهُنَّ فَعِظُوهُنَّ وَٱهۡجُرُوهُنَّ فِي ٱلۡمَضَاجِعِ وَٱضۡرِبُوهُنَّۖ فَإِنۡ أَطَعۡنَكُمۡ فَلَا تَبۡغُواْ عَلَيۡهِنَّ سَبِيلًاۗ إِنَّ ٱللَّهَ كَانَ عَلِيّٗا كَبِيرٗا

Wanaume ni wasimamizi wakuu wa wanawake; kwasababu ya vile Allah alivyowazidishia baadhi yao kwa wengine, na kwa sababu ya mali zao walizozitoa (mahari, makazi, mavazi, chakula na matumizi yote ya msingi kwa jumla). Basi wanawake wema ni wale wenye kutii, na wanaojihifadhi hata katika siri kwasababu Allah ameamrisha wajihifadhi. Na wale mnaochelea uasi wao, basi waonyeni na wahameni vitandani na wapigeni.[1] Na kama watakutiini msiwatafutie njia (sababu ya kuwaadhibu na kuwaonea). Hakika Allah ndiye aliye juu na Mkuu


1- - Hizi ni hatua za kumuadabisha mke aliye asi: (a) Kumnasihi (b) Kumuhama kitandani (c) Kumpiga pigo lisilodhuru.


Sura: ANNISAI 

Aya : 35

وَإِنۡ خِفۡتُمۡ شِقَاقَ بَيۡنِهِمَا فَٱبۡعَثُواْ حَكَمٗا مِّنۡ أَهۡلِهِۦ وَحَكَمٗا مِّنۡ أَهۡلِهَآ إِن يُرِيدَآ إِصۡلَٰحٗا يُوَفِّقِ ٱللَّهُ بَيۡنَهُمَآۗ إِنَّ ٱللَّهَ كَانَ عَلِيمًا خَبِيرٗا

Na kama mkihofia ugomvi baina yao (mke na mume), basi tumenimuamuzi mmoja kutoka familia ya mume na muamuzi mmoja kutoka familia ya mke. Kama (wasuluhishi hao) watakusudia kusuluhisha, Allah atawapa Taufiki (Mwafaka). Hakika, Allah ni Mjuzi, Mwenye habari nyingi (za yanayojiri)



Sura: ANNISAI 

Aya : 36

۞وَٱعۡبُدُواْ ٱللَّهَ وَلَا تُشۡرِكُواْ بِهِۦ شَيۡـٔٗاۖ وَبِٱلۡوَٰلِدَيۡنِ إِحۡسَٰنٗا وَبِذِي ٱلۡقُرۡبَىٰ وَٱلۡيَتَٰمَىٰ وَٱلۡمَسَٰكِينِ وَٱلۡجَارِ ذِي ٱلۡقُرۡبَىٰ وَٱلۡجَارِ ٱلۡجُنُبِ وَٱلصَّاحِبِ بِٱلۡجَنۢبِ وَٱبۡنِ ٱلسَّبِيلِ وَمَا مَلَكَتۡ أَيۡمَٰنُكُمۡۗ إِنَّ ٱللَّهَ لَا يُحِبُّ مَن كَانَ مُخۡتَالٗا فَخُورًا

Na mwabuduni Allah na msikishirikishe naye kitu chochote. Na wazazi wawili wafanyieni mazuri, na ndugu wa karibu (wa nasaba), na Yatima na maskini na jirani wa karibu (mwenye udugu wa nasaba) na jirani wa mbali (kwa makazi au udugu) na rafiki aliyeko ubavuni (rafiki mwenye usuhuba wa karibu na pia mke) na msafiri (aliyeharibikiwa) na wale walio chini ya mikono yenu ya kuume (watumwa waliopo chini ya miliki yenu). Hakika, Allah hawapendi wenye kiburi, wenye majivuno mengi



Sura: ANNISAI 

Aya : 37

ٱلَّذِينَ يَبۡخَلُونَ وَيَأۡمُرُونَ ٱلنَّاسَ بِٱلۡبُخۡلِ وَيَكۡتُمُونَ مَآ ءَاتَىٰهُمُ ٱللَّهُ مِن فَضۡلِهِۦۗ وَأَعۡتَدۡنَا لِلۡكَٰفِرِينَ عَذَابٗا مُّهِينٗا

Ambao wanaofanya ubahili na wanawaamuru watu wawe mabahili, na wanaficha fadhila alizowapa Allah. Na tumewaandalia makafiri adhabu inayodhalilisha



Sura: ANNISAI 

Aya : 38

وَٱلَّذِينَ يُنفِقُونَ أَمۡوَٰلَهُمۡ رِئَآءَ ٱلنَّاسِ وَلَا يُؤۡمِنُونَ بِٱللَّهِ وَلَا بِٱلۡيَوۡمِ ٱلۡأٓخِرِۗ وَمَن يَكُنِ ٱلشَّيۡطَٰنُ لَهُۥ قَرِينٗا فَسَآءَ قَرِينٗا

Na ambao wanatoa mali zao kwa kujionesha (na kujitangaza) kwa watu, na hawamuamini Allah na Siku ya Mwisho. Na yeyote atakayemfanya shetani kuwa rafiki yake, basi (ajue kuwa huyo ni) rafiki mbaya sana



Sura: ANNISAI 

Aya : 39

وَمَاذَا عَلَيۡهِمۡ لَوۡ ءَامَنُواْ بِٱللَّهِ وَٱلۡيَوۡمِ ٱلۡأٓخِرِ وَأَنفَقُواْ مِمَّا رَزَقَهُمُ ٱللَّهُۚ وَكَانَ ٱللَّهُ بِهِمۡ عَلِيمًا

Na wangepata tatizo gani kama wangemuamini Allah na Siku ya Mwisho na wakatoa katika vile Allah alivyowapa? Na Allah anawajua vizuri sana



Sura: ANNISAI 

Aya : 40

إِنَّ ٱللَّهَ لَا يَظۡلِمُ مِثۡقَالَ ذَرَّةٖۖ وَإِن تَكُ حَسَنَةٗ يُضَٰعِفۡهَا وَيُؤۡتِ مِن لَّدُنۡهُ أَجۡرًا عَظِيمٗا

Hakika, Allah Hadhulumu uzito wa punje. Na kama (uzito huo wa punje) ni jambo zuri analizidisha na anatoa ujira mkubwa kabisa kutoka kwake



Sura: ANNISAI 

Aya : 41

فَكَيۡفَ إِذَا جِئۡنَا مِن كُلِّ أُمَّةِۭ بِشَهِيدٖ وَجِئۡنَا بِكَ عَلَىٰ هَـٰٓؤُلَآءِ شَهِيدٗا

Basi itakuaje (Siku) tutakapoleta shahidi wa kila umma, na tukakuleta wewe kuwa shahidi wa hawa?



Sura: ANNISAI 

Aya : 42

يَوۡمَئِذٖ يَوَدُّ ٱلَّذِينَ كَفَرُواْ وَعَصَوُاْ ٱلرَّسُولَ لَوۡ تُسَوَّىٰ بِهِمُ ٱلۡأَرۡضُ وَلَا يَكۡتُمُونَ ٱللَّهَ حَدِيثٗا

Siku hiyo watatamani wale waliokufuru na kumuasi Mtume, kuwa wawe sawa na ardhi[1] na hawataweza kumficha Allah mazungumzo yoyote


1- - Makafiri watatamani Siku ya Kiama wabadilishwe wawe mchanga. Rejea Aya ya 40 ya Sura Annabai (78).


Sura: ANNISAI 

Aya : 43

يَـٰٓأَيُّهَا ٱلَّذِينَ ءَامَنُواْ لَا تَقۡرَبُواْ ٱلصَّلَوٰةَ وَأَنتُمۡ سُكَٰرَىٰ حَتَّىٰ تَعۡلَمُواْ مَا تَقُولُونَ وَلَا جُنُبًا إِلَّا عَابِرِي سَبِيلٍ حَتَّىٰ تَغۡتَسِلُواْۚ وَإِن كُنتُم مَّرۡضَىٰٓ أَوۡ عَلَىٰ سَفَرٍ أَوۡ جَآءَ أَحَدٞ مِّنكُم مِّنَ ٱلۡغَآئِطِ أَوۡ لَٰمَسۡتُمُ ٱلنِّسَآءَ فَلَمۡ تَجِدُواْ مَآءٗ فَتَيَمَّمُواْ صَعِيدٗا طَيِّبٗا فَٱمۡسَحُواْ بِوُجُوهِكُمۡ وَأَيۡدِيكُمۡۗ إِنَّ ٱللَّهَ كَانَ عَفُوًّا غَفُورًا

Enyi mlioamini, msiisogelee swala (msiswali) ilhali mmelewa, hadi mjue mnachosema.[1] Na (msiingie msikitini kwa ajili ya kuswali) mnapokuwa na janaba isipokuwa tu kama mtapita njia (kutoka upande mmoja kwenda upande mwingine) hadi muoge. Na kama mkiwa wagonjwa (na hamuwezi kutawadha au kuoga kwa maji) au mkiwa safarini au mmoja wenu ametoka chooni (kukidhi haja) au mkigusana (mkiingiliana) na wake zenu na mkakosa maji, basi tayamamuni mchanga mzuri (safi); basi pakeni nyuso zenu na mikono yenu. Hakika, Allah amekuwa Msamehevu sana, Mfutaji dhambi


1- - Hapa ilikuwa pombe haijaharamishwa. Ama baada ya pombe kuharamishwa kabisa kwa aya ya 90 ya Sura Almaida (5), suala la mtu kuswali akiwa amelewa halipo, hata kama atakuwa anaelewa anachokisema na anachokifanya.


Sura: ANNISAI 

Aya : 44

أَلَمۡ تَرَ إِلَى ٱلَّذِينَ أُوتُواْ نَصِيبٗا مِّنَ ٱلۡكِتَٰبِ يَشۡتَرُونَ ٱلضَّلَٰلَةَ وَيُرِيدُونَ أَن تَضِلُّواْ ٱلسَّبِيلَ

Hivi huwaoni waliopewa sehemu ya kitabu (Taurati) wananunua (wanabadilisha) upotevu, na wanataka mpotee njia (ya haki)



Sura: ANNISAI 

Aya : 45

وَٱللَّهُ أَعۡلَمُ بِأَعۡدَآئِكُمۡۚ وَكَفَىٰ بِٱللَّهِ وَلِيّٗا وَكَفَىٰ بِٱللَّهِ نَصِيرٗا

Na Allah anawajua zaidi maadui wenu, na Allah anatosha kuwa Mlinzi, na Allah anatosha kuwa Muokozi



Sura: ANNISAI 

Aya : 46

مِّنَ ٱلَّذِينَ هَادُواْ يُحَرِّفُونَ ٱلۡكَلِمَ عَن مَّوَاضِعِهِۦ وَيَقُولُونَ سَمِعۡنَا وَعَصَيۡنَا وَٱسۡمَعۡ غَيۡرَ مُسۡمَعٖ وَرَٰعِنَا لَيَّۢا بِأَلۡسِنَتِهِمۡ وَطَعۡنٗا فِي ٱلدِّينِۚ وَلَوۡ أَنَّهُمۡ قَالُواْ سَمِعۡنَا وَأَطَعۡنَا وَٱسۡمَعۡ وَٱنظُرۡنَا لَكَانَ خَيۡرٗا لَّهُمۡ وَأَقۡوَمَ وَلَٰكِن لَّعَنَهُمُ ٱللَّهُ بِكُفۡرِهِمۡ فَلَا يُؤۡمِنُونَ إِلَّا قَلِيلٗا

Miongoni mwa Wayahudi wapo wanaobadilisha maneno kutoka katika sehemu zake, na wanasema: Tumesikia (kauli yako) na tumeasi (amri yako), na sikiliza (kutoka kwetu na wewe) husikilizwi (unachotaka). Na (wanasema): “Raainaa”[1] kwa kuzipotosha ndimi zao na kuitukana dini. Na kama wangesema: Tumesikia na tumetii na usikie na utuangalie ingekuwa kheri kwao na jambo linalojenga zaidi, lakini Allah amewalaani kwa ukafiri wao, na hawaamini isipokuwa wachache tu


1- - Neno Raaina katika lugha ya Kiarabu lina maana nzuri ya tulee, tuchunge, tuvumilie. Lakini katika lugha ya Kiyahudi neno hili lina maana mbaya ya kejeli, kashfa na utusi. Wayahudi walikuwa wakilitumia neno hili kumzuga Mtume kwamba aone kuwa wanamrai awavumilie, awaongoze na kuwalea kumbe wanakusudia maana mbaya ya Kiyahudi. Rejea maelezo yetu pia katika Aya ya 104 ya Sura Albaqara (2).


Sura: ANNISAI 

Aya : 47

يَـٰٓأَيُّهَا ٱلَّذِينَ أُوتُواْ ٱلۡكِتَٰبَ ءَامِنُواْ بِمَا نَزَّلۡنَا مُصَدِّقٗا لِّمَا مَعَكُم مِّن قَبۡلِ أَن نَّطۡمِسَ وُجُوهٗا فَنَرُدَّهَا عَلَىٰٓ أَدۡبَارِهَآ أَوۡ نَلۡعَنَهُمۡ كَمَا لَعَنَّآ أَصۡحَٰبَ ٱلسَّبۡتِۚ وَكَانَ أَمۡرُ ٱللَّهِ مَفۡعُولًا

Enyi mliopewa kitabu, aminini tuliyoyateremsha yakisadikisha yale mliyo nayo, kabla hatujazifuta nyuso tukazirudisha kisogoni, au (kabla ya) kuwalaani kama tulivyowalaani Watu wa (siku ya) Jumamosi (Wasabato). Na amri ya Allah ni yenye kutekelezwa



Sura: ANNISAI 

Aya : 48

إِنَّ ٱللَّهَ لَا يَغۡفِرُ أَن يُشۡرَكَ بِهِۦ وَيَغۡفِرُ مَا دُونَ ذَٰلِكَ لِمَن يَشَآءُۚ وَمَن يُشۡرِكۡ بِٱللَّهِ فَقَدِ ٱفۡتَرَىٰٓ إِثۡمًا عَظِيمًا

Hakika, Allah hatoi msamaha (wa dhambi ya) kushirikishwa na anasamehe (dhambi) isiyokuwa hiyo kwa amtakaye. Na yeyote amshirikishaye Allah basi hakika amezua dhambi kubwa kabisa



Sura: ANNISAI 

Aya : 49

أَلَمۡ تَرَ إِلَى ٱلَّذِينَ يُزَكُّونَ أَنفُسَهُمۚ بَلِ ٱللَّهُ يُزَكِّي مَن يَشَآءُ وَلَا يُظۡلَمُونَ فَتِيلًا

Hivi huwaoni wale wanaozitakasa nafsi zao? Bali Allah humtakasa amtakaye. Na (waja) hawatadhulumiwa hata kitu chenye uzito wa uzi wa kokwa ya tende



Sura: ANNISAI 

Aya : 50

ٱنظُرۡ كَيۡفَ يَفۡتَرُونَ عَلَى ٱللَّهِ ٱلۡكَذِبَۖ وَكَفَىٰ بِهِۦٓ إِثۡمٗا مُّبِينًا

Tazama jinsi wanavyomtungia Allah uongo. Na hayo yanatosha kuwa dhambi zilizo dhahiri



Sura: ANNISAI 

Aya : 51

أَلَمۡ تَرَ إِلَى ٱلَّذِينَ أُوتُواْ نَصِيبٗا مِّنَ ٱلۡكِتَٰبِ يُؤۡمِنُونَ بِٱلۡجِبۡتِ وَٱلطَّـٰغُوتِ وَيَقُولُونَ لِلَّذِينَ كَفَرُواْ هَـٰٓؤُلَآءِ أَهۡدَىٰ مِنَ ٱلَّذِينَ ءَامَنُواْ سَبِيلًا

Je, huwaoni waliopewa sehemu ya kitabu wanaamini Jibti (masanamu, mashetani na mizimu) na Twaghuti (kila kinachoabudiwa badala ya Allah na kikawa radhi), na wanawaambia wale waliokufuru kwamba hawa wameongoka zaidi katika njia kuliko wale walioamini



Sura: ANNISAI 

Aya : 52

أُوْلَـٰٓئِكَ ٱلَّذِينَ لَعَنَهُمُ ٱللَّهُۖ وَمَن يَلۡعَنِ ٱللَّهُ فَلَن تَجِدَ لَهُۥ نَصِيرًا

Hao ndio ambao Allah amewa-laani. Na ambaye Allah amemlaani basi katu hutampata wa kumnusuru



Sura: ANNISAI 

Aya : 53

أَمۡ لَهُمۡ نَصِيبٞ مِّنَ ٱلۡمُلۡكِ فَإِذٗا لَّا يُؤۡتُونَ ٱلنَّاسَ نَقِيرًا

Au wanayo sehemu ya ufalme? Basi hapo wasingeliwapa watu (chochote) hata utando wa kokwa ya tende



Sura: ANNISAI 

Aya : 54

أَمۡ يَحۡسُدُونَ ٱلنَّاسَ عَلَىٰ مَآ ءَاتَىٰهُمُ ٱللَّهُ مِن فَضۡلِهِۦۖ فَقَدۡ ءَاتَيۡنَآ ءَالَ إِبۡرَٰهِيمَ ٱلۡكِتَٰبَ وَٱلۡحِكۡمَةَ وَءَاتَيۡنَٰهُم مُّلۡكًا عَظِيمٗا

Au wanawafayia watu husuda kwa sababu ya fadhila walizopewa na Allah? Hakika tuliipa familia ya Ibrahimu kitabu na hekima na tuliwapa ufalme mkubwa



Sura: ANNISAI 

Aya : 55

فَمِنۡهُم مَّنۡ ءَامَنَ بِهِۦ وَمِنۡهُم مَّن صَدَّ عَنۡهُۚ وَكَفَىٰ بِجَهَنَّمَ سَعِيرًا

Basi miongoni mwao kuna walioyaamini haya, na wapo miongoni mwao walioyapinga. Na Jahanamu inatosha kuwa moto mkali wa kuunguza



Sura: ANNISAI 

Aya : 56

إِنَّ ٱلَّذِينَ كَفَرُواْ بِـَٔايَٰتِنَا سَوۡفَ نُصۡلِيهِمۡ نَارٗا كُلَّمَا نَضِجَتۡ جُلُودُهُم بَدَّلۡنَٰهُمۡ جُلُودًا غَيۡرَهَا لِيَذُوقُواْ ٱلۡعَذَابَۗ إِنَّ ٱللَّهَ كَانَ عَزِيزًا حَكِيمٗا

Hakika, wale waliozipinga Aya zetu, tutawaingiza Motoni. Kila zinapoiva ngozi zao tutawabadilishia ngozi nyingine, ili waonje adhabu. Hakika, Allah amekuwa Mwenye nguvu kubwa, Mwenye hekima



Sura: ANNISAI 

Aya : 57

وَٱلَّذِينَ ءَامَنُواْ وَعَمِلُواْ ٱلصَّـٰلِحَٰتِ سَنُدۡخِلُهُمۡ جَنَّـٰتٖ تَجۡرِي مِن تَحۡتِهَا ٱلۡأَنۡهَٰرُ خَٰلِدِينَ فِيهَآ أَبَدٗاۖ لَّهُمۡ فِيهَآ أَزۡوَٰجٞ مُّطَهَّرَةٞۖ وَنُدۡخِلُهُمۡ ظِلّٗا ظَلِيلًا

Na walioamini na wakatenda mema tutawaingiza katika Pepo zipitazo mito chini yake, wakibaki humo milele. Katika Pepo hizo watakuwa na wake waliotakaswa, na tutawaingiza katika vivuli vinavyofunika daima



Sura: ANNISAI 

Aya : 58

۞إِنَّ ٱللَّهَ يَأۡمُرُكُمۡ أَن تُؤَدُّواْ ٱلۡأَمَٰنَٰتِ إِلَىٰٓ أَهۡلِهَا وَإِذَا حَكَمۡتُم بَيۡنَ ٱلنَّاسِ أَن تَحۡكُمُواْ بِٱلۡعَدۡلِۚ إِنَّ ٱللَّهَ نِعِمَّا يَعِظُكُم بِهِۦٓۗ إِنَّ ٱللَّهَ كَانَ سَمِيعَۢا بَصِيرٗا

Hakika, Allah anakuamrisheni kurudisha amana kwa wenyewe, na mnapo hukumu baina ya watu mhukumu kwa uadilifu. Hakika, mazuri mno anayokuwaidhini Allah ni hayo. HakikaAllah ndiye Mwenye kusikia, Mwenye kuona



Sura: ANNISAI 

Aya : 59

يَـٰٓأَيُّهَا ٱلَّذِينَ ءَامَنُوٓاْ أَطِيعُواْ ٱللَّهَ وَأَطِيعُواْ ٱلرَّسُولَ وَأُوْلِي ٱلۡأَمۡرِ مِنكُمۡۖ فَإِن تَنَٰزَعۡتُمۡ فِي شَيۡءٖ فَرُدُّوهُ إِلَى ٱللَّهِ وَٱلرَّسُولِ إِن كُنتُمۡ تُؤۡمِنُونَ بِٱللَّهِ وَٱلۡيَوۡمِ ٱلۡأٓخِرِۚ ذَٰلِكَ خَيۡرٞ وَأَحۡسَنُ تَأۡوِيلًا

Enyi mlioamini, mtiini Allah na mtiini Mtume, na wenye mamlaka katika nyinyi. Basi iwapo mtavutana[1] katika jambo lolote, lirudisheni kwa Allah na (kwa) Mtume, ikiwa mnamuamini Allah na Siku ya Mwisho. Hilo ni bora zaidi na ni mwisho mzuri sana


1- - Kuvutana ni kubishana kuhusu jambo fulani kati ya pande mbili au zaidi na kila upande huvutia kwake.


Sura: ANNISAI 

Aya : 60

أَلَمۡ تَرَ إِلَى ٱلَّذِينَ يَزۡعُمُونَ أَنَّهُمۡ ءَامَنُواْ بِمَآ أُنزِلَ إِلَيۡكَ وَمَآ أُنزِلَ مِن قَبۡلِكَ يُرِيدُونَ أَن يَتَحَاكَمُوٓاْ إِلَى ٱلطَّـٰغُوتِ وَقَدۡ أُمِرُوٓاْ أَن يَكۡفُرُواْ بِهِۦۖ وَيُرِيدُ ٱلشَّيۡطَٰنُ أَن يُضِلَّهُمۡ ضَلَٰلَۢا بَعِيدٗا

Je, hukuwaona wanaodai kuwa wameamini yaliyoteremshwa kwako na yaliyoteremshwa kabla yako wanataka wakahukumiane kwa Twaghuti[1], na ilhali wameamrishwa wamkatae? Na shetani anataka kuwapoteza upotevu wa mbali


1- - Twaghuti ni kila kinachoabudiwa na kutiiwa badala ya Allah ikiwa ni pamoja na shetani, sanamu, mzimu n.k.