Surah: ATTAUBA 

Ayah : 31

ٱتَّخَذُوٓاْ أَحۡبَارَهُمۡ وَرُهۡبَٰنَهُمۡ أَرۡبَابٗا مِّن دُونِ ٱللَّهِ وَٱلۡمَسِيحَ ٱبۡنَ مَرۡيَمَ وَمَآ أُمِرُوٓاْ إِلَّا لِيَعۡبُدُوٓاْ إِلَٰهٗا وَٰحِدٗاۖ لَّآ إِلَٰهَ إِلَّا هُوَۚ سُبۡحَٰنَهُۥ عَمَّا يُشۡرِكُونَ

(Wayahudi na Wanaswara) Wamewafanya watawa wao na makuhani wao Miungu (kwa kuwaabudu) badala ya Allah, na pia Masihi bin Mariamu (wamemfanya Mungu)[1]. Na hawakuamrishwa isipokuwa wamuabudu Mola mmoja tu. Hakuna muabudiwa (wa haki) ila Yeye tu. Ametakasika na hayo wanayomshirikisha nayo


1- - Wayahudi na Wanaswara wamewafanya watawa na wanazuoni wao Miungu badala ya Allah kwa sababu ya kuwatii katika kila jambo, hata katika yale mambo ambayo yapo tofauti na maandiko na mafundisho sahihi ya dini. Utiifu wa aina hii na utayari wa aina hii wa kutii katika kamusi ya Kiislamu unahisabika kwamba ni ibada. Hii ni tahadhari kwa Waislamu ya kuacha kuiga mwenendo huu wa kuwatii viongozi katika mambo ambayo yanapingana na maandiko na maelekezo sahihi ya dini. Utiifu usiokuwa na mipaka kwa mujibu wa Uislamu ni ibada na unatakiwa afanyiwe Allah tu.


Surah: ATTAUBA 

Ayah : 32

يُرِيدُونَ أَن يُطۡفِـُٔواْ نُورَ ٱللَّهِ بِأَفۡوَٰهِهِمۡ وَيَأۡبَى ٱللَّهُ إِلَّآ أَن يُتِمَّ نُورَهُۥ وَلَوۡ كَرِهَ ٱلۡكَٰفِرُونَ

(Makafiri) Wanataka kuizima Nuru ya Allah (Uislamu) kwa vinywa vyao, na Allah anakataa ila (ni lazima) aitimize Nuru yake (Dini yake na kumnusuru Nabii wake) na hata kama makafiri watachukia



Surah: ATTAUBA 

Ayah : 33

هُوَ ٱلَّذِيٓ أَرۡسَلَ رَسُولَهُۥ بِٱلۡهُدَىٰ وَدِينِ ٱلۡحَقِّ لِيُظۡهِرَهُۥ عَلَى ٱلدِّينِ كُلِّهِۦ وَلَوۡ كَرِهَ ٱلۡمُشۡرِكُونَ

Yeye (Allah) ndiye aliyemtuma Mtume wake kwa uwongofu (Qur’an) na Dini ya Haki ili ipate kuzishinda dini zote, na hata kama washirikina watachukia



Surah: ATTAUBA 

Ayah : 34

۞يَـٰٓأَيُّهَا ٱلَّذِينَ ءَامَنُوٓاْ إِنَّ كَثِيرٗا مِّنَ ٱلۡأَحۡبَارِ وَٱلرُّهۡبَانِ لَيَأۡكُلُونَ أَمۡوَٰلَ ٱلنَّاسِ بِٱلۡبَٰطِلِ وَيَصُدُّونَ عَن سَبِيلِ ٱللَّهِۗ وَٱلَّذِينَ يَكۡنِزُونَ ٱلذَّهَبَ وَٱلۡفِضَّةَ وَلَا يُنفِقُونَهَا فِي سَبِيلِ ٱللَّهِ فَبَشِّرۡهُم بِعَذَابٍ أَلِيمٖ

Enyi mlioamini, kwa hakika kabisa watawa na makuhani wengi wanakula mali za watu kwa batili na wanazuia (watu kufuata) Njia ya Allah (Uislamu). Na wale wanaolimbikiza dhahabu na fedha na hawazitumii katika Njia ya Allah, wabashirie (waonye) adhabu iumizayo mno



Surah: ATTAUBA 

Ayah : 35

يَوۡمَ يُحۡمَىٰ عَلَيۡهَا فِي نَارِ جَهَنَّمَ فَتُكۡوَىٰ بِهَا جِبَاهُهُمۡ وَجُنُوبُهُمۡ وَظُهُورُهُمۡۖ هَٰذَا مَا كَنَزۡتُمۡ لِأَنفُسِكُمۡ فَذُوقُواْ مَا كُنتُمۡ تَكۡنِزُونَ

Siku zitapounguzwa (mali zao) katika Moto wa Jahanamu, na kwazo yatachomwa mapaji ya nyuso zao na (zitachomwa) mbavu zao na (itachomwa) migongo yao, (na wataambiwa kwa kusimangwa): “Haya ndiyo mliojilimbikizia. Basi onjeni mliyokuwa mnayalimbikiza



Surah: ATTAUBA 

Ayah : 36

إِنَّ عِدَّةَ ٱلشُّهُورِ عِندَ ٱللَّهِ ٱثۡنَا عَشَرَ شَهۡرٗا فِي كِتَٰبِ ٱللَّهِ يَوۡمَ خَلَقَ ٱلسَّمَٰوَٰتِ وَٱلۡأَرۡضَ مِنۡهَآ أَرۡبَعَةٌ حُرُمٞۚ ذَٰلِكَ ٱلدِّينُ ٱلۡقَيِّمُۚ فَلَا تَظۡلِمُواْ فِيهِنَّ أَنفُسَكُمۡۚ وَقَٰتِلُواْ ٱلۡمُشۡرِكِينَ كَآفَّةٗ كَمَا يُقَٰتِلُونَكُمۡ كَآفَّةٗۚ وَٱعۡلَمُوٓاْ أَنَّ ٱللَّهَ مَعَ ٱلۡمُتَّقِينَ

Hakika, idadi ya miezi kwa Allah ni miezi kumi na miwili katika kitabu cha Allah[1] tangu alipoumba mbingu na ardhi. Katika hiyo ipo (miezi) minne mitukufu[2]. Hiyo ndio Dini iliyo sawa. Basi msidhulumu nafsi zenu humo (ndani ya hiyo miezi minne kwa kufanya mambo yasiyomridhisha Allah). Na piganeni na washirikina (makafiri) wote kama wao wanavyopigana nanyi nyote. Na jueni kuwa Allah yupo pamoja na wenye takwa (uchaMungu)


1- - Hiki ni kitabu kiitwacho Allauhul-Mahfuudh na kinachotunza mambo yote. Kitabu hiki kimetajwa katika Aya ya 22 ya Sura Alburuuj (85).


2- - Miezi hiyo mine mitukufu ni Dhul-qa’adah (Mfungopili), Dhul-hijja (Mfungotatu), Muharram (Mfungonne) na Rajabu (mfungokumi).


Surah: ATTAUBA 

Ayah : 37

إِنَّمَا ٱلنَّسِيٓءُ زِيَادَةٞ فِي ٱلۡكُفۡرِۖ يُضَلُّ بِهِ ٱلَّذِينَ كَفَرُواْ يُحِلُّونَهُۥ عَامٗا وَيُحَرِّمُونَهُۥ عَامٗا لِّيُوَاطِـُٔواْ عِدَّةَ مَا حَرَّمَ ٱللَّهُ فَيُحِلُّواْ مَا حَرَّمَ ٱللَّهُۚ زُيِّنَ لَهُمۡ سُوٓءُ أَعۡمَٰلِهِمۡۗ وَٱللَّهُ لَا يَهۡدِي ٱلۡقَوۡمَ ٱلۡكَٰفِرِينَ

Bila ya shaka yoyote, ubadili-shwaji (ucheleweshwaji) wa miezi mitukufu[1]) ni ukafiri ulio zidi walio kufuru wanautumia kuwapoteza watu wasijuwe miezi mitukufu; wanahalalisha mwaka mmoja na kuharamisha mwaka mwingine, ili wafanye kuwa sawa idadi ya ile (miezi) aliyoitukuza Allah. Kwa hivyo watahalalisha alivyo viharimisha Allah. Wamepambiwa vitendo vyao viovu. Na Allah hawa-ongozi watu makafiri


1- - Allah katika Aya iliyotangulia kabla ya hii ametaja kuwa katika miezi kumi na miwili ya mwaka ameteua miezi mine na kuifanya mitukufu. Ndani ya miezi hiyo mitukufu ameharamisha mambo mengi ikiwemo kupigana vita. Makafiri, kwa ukafiri wao, walikuwa wanaufanyia ukarabati utaratibu huu uliowekwa na Allah na kufanya mabadiliko ya miezi mitukufu kwa kuipa majina ya miezi mitukufu miezi mingine ili wapate fursa ya kufanya yale yaliyokatazwa katika miezi mitukufu. Allah anahesabu kitengo hiki ni ukafiri juu ya ukafiri.


Surah: ATTAUBA 

Ayah : 38

يَـٰٓأَيُّهَا ٱلَّذِينَ ءَامَنُواْ مَا لَكُمۡ إِذَا قِيلَ لَكُمُ ٱنفِرُواْ فِي سَبِيلِ ٱللَّهِ ٱثَّاقَلۡتُمۡ إِلَى ٱلۡأَرۡضِۚ أَرَضِيتُم بِٱلۡحَيَوٰةِ ٱلدُّنۡيَا مِنَ ٱلۡأٓخِرَةِۚ فَمَا مَتَٰعُ ٱلۡحَيَوٰةِ ٱلدُّنۡيَا فِي ٱلۡأٓخِرَةِ إِلَّا قَلِيلٌ

Enyi mlioamini, mna nini wakati mnapoambiwa: Nendeni haraka katika Njia ya Allah (Jihadi), mnajitia uzito katika ardhi (kwa kubaki majumbani na kuwa wazito katika kuitikia wito wa Jihadi)? Je, mmeyaridhia maisha ya dunia kuliko ya Akhera? Basi hazikuwa starehe za maisha ya dunia ukizilinganisha na za Akhera isipokuwa ni chache mno



Surah: ATTAUBA 

Ayah : 39

إِلَّا تَنفِرُواْ يُعَذِّبۡكُمۡ عَذَابًا أَلِيمٗا وَيَسۡتَبۡدِلۡ قَوۡمًا غَيۡرَكُمۡ وَلَا تَضُرُّوهُ شَيۡـٔٗاۗ وَٱللَّهُ عَلَىٰ كُلِّ شَيۡءٖ قَدِيرٌ

Kama hamtatoka (kwenda kupambana kwenye Jihadi basi Allah) atakuadhibuni adhabu inayoumiza mno, na atabadilisha (na kuleta) watu wengine wasiokuwa nyinyi (wenye utayari wa kwenda Jihadi) na nyinyi hamtamdhuru chochote Allah (kwa kuikimbia kwenu Jihadi). Na Allah ni Muweza wa kila kitu



Surah: ATTAUBA 

Ayah : 40

إِلَّا تَنصُرُوهُ فَقَدۡ نَصَرَهُ ٱللَّهُ إِذۡ أَخۡرَجَهُ ٱلَّذِينَ كَفَرُواْ ثَانِيَ ٱثۡنَيۡنِ إِذۡ هُمَا فِي ٱلۡغَارِ إِذۡ يَقُولُ لِصَٰحِبِهِۦ لَا تَحۡزَنۡ إِنَّ ٱللَّهَ مَعَنَاۖ فَأَنزَلَ ٱللَّهُ سَكِينَتَهُۥ عَلَيۡهِ وَأَيَّدَهُۥ بِجُنُودٖ لَّمۡ تَرَوۡهَا وَجَعَلَ كَلِمَةَ ٱلَّذِينَ كَفَرُواْ ٱلسُّفۡلَىٰۗ وَكَلِمَةُ ٱللَّهِ هِيَ ٱلۡعُلۡيَاۗ وَٱللَّهُ عَزِيزٌ حَكِيمٌ

Ikiwa nyinyi hamtamnusuru Mtume (Muhammad), basi Allah alikwishamnusuru pale waliokufuru walipomtoa (walipomfukuza) akiwa mmoja kati ya wawili wakati walipokuwa kwenye pango (la mlima Thaur), wakati akimwambia Swahibawake[1]: “Usihuzunike. Hakika, Allah yupo pamoja nasi”. Allah alimteremshia utulivu wake, na akampa nguvu kwa majeshi ambayo hamkuyaona, na akalifanya neno la waliokufuru kuwa chini sana, na Neno la Allah ndilo lililo juu zaidi. Na Allah ndiye Mwenye nguvu mno, Mwenye hekima sana[2]


1- - Alikuwa Swahaba Abubakar, Allah amuwie radhi.


2- - Aya hii inatutajia tukio adhimu la kuhama kwa Nabii Muhammad (Allah amshushie rehema na amani)
kutoka kwenye mji Mtukufu wa Makkah na kwenda kujificha kwenye pango (Ghari Thaur) kwa muda wa
siku tatu, na hatimae kuelekea uhamishoni kwenye Mji wa Madina. Aidha, Allah kupitia Aya hii
ametudhihirishia wazi utukufu wa Nabii wake na utukufu wa Swahaba Abubakar Allah amridhie ambaye
Alifuatana na Nabii kwenye msafara huo.


Surah: ATTAUBA 

Ayah : 41

ٱنفِرُواْ خِفَافٗا وَثِقَالٗا وَجَٰهِدُواْ بِأَمۡوَٰلِكُمۡ وَأَنفُسِكُمۡ فِي سَبِيلِ ٱللَّهِۚ ذَٰلِكُمۡ خَيۡرٞ لَّكُمۡ إِن كُنتُمۡ تَعۡلَمُونَ

Tokeni haraka (kwenda kwenye Jihadi katika mazingira yoyote) mkiwa wepesi (wa hali, mali, maandalizi n.k.) na wazito (wa hali, mali, maandalizi n.k.) na piganeni Jihadi kwa mali zenu na nafsi zenu katika Njia ya Allah. Hiyo ni heri kwenu iwapo mnajua



Surah: ATTAUBA 

Ayah : 42

لَوۡ كَانَ عَرَضٗا قَرِيبٗا وَسَفَرٗا قَاصِدٗا لَّٱتَّبَعُوكَ وَلَٰكِنۢ بَعُدَتۡ عَلَيۡهِمُ ٱلشُّقَّةُۚ وَسَيَحۡلِفُونَ بِٱللَّهِ لَوِ ٱسۡتَطَعۡنَا لَخَرَجۡنَا مَعَكُمۡ يُهۡلِكُونَ أَنفُسَهُمۡ وَٱللَّهُ يَعۡلَمُ إِنَّهُمۡ لَكَٰذِبُونَ

Lau kama ingekuwa (hilo wanaloitiwa) ni faida ya papo kwa papo na safari fupi, kwa yakini kabisa wangelikufuata (ili nao wapate ngawira), na lakini kipande (cha safari ya eneo la vita la Tabuk) kimekuwa cha mbali (ndio maana wamekuwa wazito). Na wataapia Allah (mtakaporejea) kwamba: Lau kama tungeweza, bila ya shaka tungelitoka pamoja nanyi. Wanaziangamiza nafsi zao, na Allah anajua fika kuwa wao ni waongo



Surah: ATTAUBA 

Ayah : 43

عَفَا ٱللَّهُ عَنكَ لِمَ أَذِنتَ لَهُمۡ حَتَّىٰ يَتَبَيَّنَ لَكَ ٱلَّذِينَ صَدَقُواْ وَتَعۡلَمَ ٱلۡكَٰذِبِينَ

Allah alishakusamehe. Kwa nini uliwaruhusu (wasiende kwenye vita vya Tabuki) kabla ya kukubainikia wasemao kweli, na ukawajua waongo?



Surah: ATTAUBA 

Ayah : 44

لَا يَسۡتَـٔۡذِنُكَ ٱلَّذِينَ يُؤۡمِنُونَ بِٱللَّهِ وَٱلۡيَوۡمِ ٱلۡأٓخِرِ أَن يُجَٰهِدُواْ بِأَمۡوَٰلِهِمۡ وَأَنفُسِهِمۡۗ وَٱللَّهُ عَلِيمُۢ بِٱلۡمُتَّقِينَ

Hawakuombi ruhusa wale wanaomuamini Allah na Siku ya Mwisho, wasiende kupigana Jihadi kwa mali zao na nafsi zao. Na Allah ni Mwenye kuwajua mno wachaMungu



Surah: ATTAUBA 

Ayah : 45

إِنَّمَا يَسۡتَـٔۡذِنُكَ ٱلَّذِينَ لَا يُؤۡمِنُونَ بِٱللَّهِ وَٱلۡيَوۡمِ ٱلۡأٓخِرِ وَٱرۡتَابَتۡ قُلُوبُهُمۡ فَهُمۡ فِي رَيۡبِهِمۡ يَتَرَدَّدُونَ

Hakika wanaokuomba ruhusa ni wale wasiomuamini Allah na Siku ya Mwisho na nyoyo zao zina shaka (Wanafiki). Basi hao wanataradadi katika shaka zao



Surah: ATTAUBA 

Ayah : 46

۞وَلَوۡ أَرَادُواْ ٱلۡخُرُوجَ لَأَعَدُّواْ لَهُۥ عُدَّةٗ وَلَٰكِن كَرِهَ ٱللَّهُ ٱنۢبِعَاثَهُمۡ فَثَبَّطَهُمۡ وَقِيلَ ٱقۡعُدُواْ مَعَ ٱلۡقَٰعِدِينَ

Na kama ingelikuwa kweli walitaka kutoka, bila ya shaka wangeliandalia hilo maandalizi, na lakini Allah amechukia kutoka kwao, na kwa hiyo akawakwaza na ikasemwa: Kaeni pamoja na wanaokaa



Surah: ATTAUBA 

Ayah : 47

لَوۡ خَرَجُواْ فِيكُم مَّا زَادُوكُمۡ إِلَّا خَبَالٗا وَلَأَوۡضَعُواْ خِلَٰلَكُمۡ يَبۡغُونَكُمُ ٱلۡفِتۡنَةَ وَفِيكُمۡ سَمَّـٰعُونَ لَهُمۡۗ وَٱللَّهُ عَلِيمُۢ بِٱلظَّـٰلِمِينَ

Lau kama (wanafiki) wangetoka (kwenda Jihadi) pamoja nanyi wasingekuzidishieni isipokuwa mchafuko (mvurugano) tu, na wangekwenda mbio kati yenu wakikutilieni fitina. Na miongoni mwenu wapo (wapelelezi) wanaosikiliza sana (habari kwenu) na kuzipeleka kwao. Na Allah anawajua mno madhalimu



Surah: ATTAUBA 

Ayah : 48

لَقَدِ ٱبۡتَغَوُاْ ٱلۡفِتۡنَةَ مِن قَبۡلُ وَقَلَّبُواْ لَكَ ٱلۡأُمُورَ حَتَّىٰ جَآءَ ٱلۡحَقُّ وَظَهَرَ أَمۡرُ ٱللَّهِ وَهُمۡ كَٰرِهُونَ

Kwa hakika kabisa, (wanafiki) hapo awali (kabla ya vita vya Tabuki) walitaka fitina, na wakakupindulia pindulia mambo (kihila ili ukubaliane nao), mpaka ilipokuja haki na likadhihiri jambo la Allah (Dini yake), na ilhali wao ni wenye kuchukia



Surah: ATTAUBA 

Ayah : 49

وَمِنۡهُم مَّن يَقُولُ ٱئۡذَن لِّي وَلَا تَفۡتِنِّيٓۚ أَلَا فِي ٱلۡفِتۡنَةِ سَقَطُواْۗ وَإِنَّ جَهَنَّمَ لَمُحِيطَةُۢ بِٱلۡكَٰفِرِينَ

Na miongoni mwao (hao wanafiki) wapo wanaosema: Niruhusu (nisiende Jihadi) wala usinitie katika fitina. Zinduka! Wameshatumbukia katika fitina (kwa kuhalifu Jihadi na kutoa udhuru wa uongo). Na hakika kabisa, Jahanamu ni yenye kuwazingira makafiri



Surah: ATTAUBA 

Ayah : 50

إِن تُصِبۡكَ حَسَنَةٞ تَسُؤۡهُمۡۖ وَإِن تُصِبۡكَ مُصِيبَةٞ يَقُولُواْ قَدۡ أَخَذۡنَآ أَمۡرَنَا مِن قَبۡلُ وَيَتَوَلَّواْ وَّهُمۡ فَرِحُونَ

Likikupata jambo zuri (mafanikio, wema, nusura au ngawira) linawachukiza, na yakikusibu maafa, wanasema: Sisi tulilichukulia (tahadhari) jambo letu tokea awali (kwa kujiweka mbali) na wanageuka (kwenda zao) na ilhali wakifurahia sana (kilichowasibu Waislamu)



Surah: ATTAUBA 

Ayah : 51

قُل لَّن يُصِيبَنَآ إِلَّا مَا كَتَبَ ٱللَّهُ لَنَا هُوَ مَوۡلَىٰنَاۚ وَعَلَى ٱللَّهِ فَلۡيَتَوَكَّلِ ٱلۡمُؤۡمِنُونَ

Sema: Katu halitusibu ila tu alilotuandikia Allah. Yeye ndiye Mola wetu Mlinzi. Na waumini (wa kweli) wamtegemee Allah tu



Surah: ATTAUBA 

Ayah : 52

قُلۡ هَلۡ تَرَبَّصُونَ بِنَآ إِلَّآ إِحۡدَى ٱلۡحُسۡنَيَيۡنِۖ وَنَحۡنُ نَتَرَبَّصُ بِكُمۡ أَن يُصِيبَكُمُ ٱللَّهُ بِعَذَابٖ مِّنۡ عِندِهِۦٓ أَوۡ بِأَيۡدِينَاۖ فَتَرَبَّصُوٓاْ إِنَّا مَعَكُم مُّتَرَبِّصُونَ

Sema (ewe Nabii Muhammad uwaambie wanafiki kuwa): Hivi mnatutazamia litupate moja ya mema mawili (kufa mashahidi au kupata ushindi)? Nasi tunakutazamieni Allah akufikishieni adhabu kutoka kwake au kwa (kupitia) mikono yetu. Basi ngojeni, nasi pamoja nanyi tunangoja



Surah: ATTAUBA 

Ayah : 53

قُلۡ أَنفِقُواْ طَوۡعًا أَوۡ كَرۡهٗا لَّن يُتَقَبَّلَ مِنكُمۡ إِنَّكُمۡ كُنتُمۡ قَوۡمٗا فَٰسِقِينَ

Sema (uwaambie wanafiki kuwa): Toeni mkipenda au msipende. Katu hakitopokelewa kitu kwenu. Hakika, nyinyi mmekuwa watu waovu



Surah: ATTAUBA 

Ayah : 54

وَمَا مَنَعَهُمۡ أَن تُقۡبَلَ مِنۡهُمۡ نَفَقَٰتُهُمۡ إِلَّآ أَنَّهُمۡ كَفَرُواْ بِٱللَّهِ وَبِرَسُولِهِۦ وَلَا يَأۡتُونَ ٱلصَّلَوٰةَ إِلَّا وَهُمۡ كُسَالَىٰ وَلَا يُنفِقُونَ إِلَّا وَهُمۡ كَٰرِهُونَ

Na hakuna kilichowazuia kukubaliwa michango yao ila tu kwamba, walimkufuru Allah na Mtume wake na hawaendikuswali ila wakiwa wavivu, na wala hawatoi (michango kwenye Jihadi n.k.) ila wakiwa wamechukia



Surah: ATTAUBA 

Ayah : 55

فَلَا تُعۡجِبۡكَ أَمۡوَٰلُهُمۡ وَلَآ أَوۡلَٰدُهُمۡۚ إِنَّمَا يُرِيدُ ٱللَّهُ لِيُعَذِّبَهُم بِهَا فِي ٱلۡحَيَوٰةِ ٱلدُّنۡيَا وَتَزۡهَقَ أَنفُسُهُمۡ وَهُمۡ كَٰفِرُونَ

Zisikupendeze (zisikushangaze) mali zao wala watoto wao. Hakika ilivyo ni kwamba, Allah anataka kuwaadhibu kwazo hapa duniani[1], na roho zao zitoke (kwa uchungu) na wao wakiwa makafiri


1- - Adhabu inayotajwa hapa kwa wanafiki na makafiri kwa jumla wanaojikusanyia mali na kukataa kumuamini Allah ni tabu wanayoipata katika kutafuta mali, tabu wanayoipata katika kuilinda na tabu wanayoipata katika kukosa amani.


Surah: ATTAUBA 

Ayah : 56

وَيَحۡلِفُونَ بِٱللَّهِ إِنَّهُمۡ لَمِنكُمۡ وَمَا هُم مِّنكُمۡ وَلَٰكِنَّهُمۡ قَوۡمٞ يَفۡرَقُونَ

Na wanaapa kwa Allah (kwa uongo) kwamba wao ni katika nyinyi, na wala wao si katika nyinyi. Lakini wao ni watu wanaoishi kwa hofu



Surah: ATTAUBA 

Ayah : 57

لَوۡ يَجِدُونَ مَلۡجَـًٔا أَوۡ مَغَٰرَٰتٍ أَوۡ مُدَّخَلٗا لَّوَلَّوۡاْ إِلَيۡهِ وَهُمۡ يَجۡمَحُونَ

Laiti kama (hawa wanafiki) wangepata mahali pa kukimbilia au ngome au pango la kuingia (ili wasiende Jihadi) basi wangekwenda huko na huku wakikimbilia



Surah: ATTAUBA 

Ayah : 58

وَمِنۡهُم مَّن يَلۡمِزُكَ فِي ٱلصَّدَقَٰتِ فَإِنۡ أُعۡطُواْ مِنۡهَا رَضُواْ وَإِن لَّمۡ يُعۡطَوۡاْ مِنۡهَآ إِذَا هُمۡ يَسۡخَطُونَ

Na miongoni mwao wapo (wanafiki) wanaokubeua (wanaokubeza) katika (kugawa) sadaka. Wanapopewa sadaka katika sadaka hizo (kama walivyotarajia) wanaridhika. Na wasipopewa katika sadaka hizo (kama walivyotarajia) haraka wanakasirika



Surah: ATTAUBA 

Ayah : 59

وَلَوۡ أَنَّهُمۡ رَضُواْ مَآ ءَاتَىٰهُمُ ٱللَّهُ وَرَسُولُهُۥ وَقَالُواْ حَسۡبُنَا ٱللَّهُ سَيُؤۡتِينَا ٱللَّهُ مِن فَضۡلِهِۦ وَرَسُولُهُۥٓ إِنَّآ إِلَى ٱللَّهِ رَٰغِبُونَ

Na laiti kama (wanafiki) wangeridhia kile walichopewa na Allah na Mtume wake na wakasema: “Allah anatutosha, Allah atatupa (vingi) katika fadhila zake na pia Mtume wake (atatupa zaidi ya alivyotupa), (ingekuwa bora zaidi kwao). Hakika sisi ni wenye kumtaraji Allah tu (atupe fadhila zake)”



Surah: ATTAUBA 

Ayah : 60

۞إِنَّمَا ٱلصَّدَقَٰتُ لِلۡفُقَرَآءِ وَٱلۡمَسَٰكِينِ وَٱلۡعَٰمِلِينَ عَلَيۡهَا وَٱلۡمُؤَلَّفَةِ قُلُوبُهُمۡ وَفِي ٱلرِّقَابِ وَٱلۡغَٰرِمِينَ وَفِي سَبِيلِ ٱللَّهِ وَٱبۡنِ ٱلسَّبِيلِۖ فَرِيضَةٗ مِّنَ ٱللَّهِۗ وَٱللَّهُ عَلِيمٌ حَكِيمٞ

Kwa hakika kabisa, sadaka (Zaka) ni za mafakiri[1] na maskini[2] na watumishi[3], na mnaowazoesha nyoyo zao[4] na katika kukomboa watumwa na wenye madeni na katika Njia ya Allah na msafiri. Huu ni wajibu uliofaradhishwa na Allah. Na Allah ni Mwenye kujua, Mwenye hekima sana


1- - Fakiri au fukara ni mtu ambaye hana kabisa uwezo wa kipato kinachoweza kukidhi mahitaji yake ya kila siku.


2- - Maskini ni mtu ambaye anacho kipato lakini hakikidhi kwa asilimia mia moja mahitaji yake ya kila siku.


3- - Ni wale watumishi walioajiriwa kwa kazi ya ukusanyaji wa Zaka.


4- - Hawa ni watu wanaopewa Zaka ili kuzilainisha na kuzivuta nyoyo zao ziukubali na kuupenda Uislamu.