Surah: AL-AARAAF 

Ayah : 31

۞يَٰبَنِيٓ ءَادَمَ خُذُواْ زِينَتَكُمۡ عِندَ كُلِّ مَسۡجِدٖ وَكُلُواْ وَٱشۡرَبُواْ وَلَا تُسۡرِفُوٓاْۚ إِنَّهُۥ لَا يُحِبُّ ٱلۡمُسۡرِفِينَ

Enyi wanadamu, chukueni mapambo yenu kila muendapo msikitini (kila mnaposwali)[1] na kuleni na kunyweni na msifanye ubadhirifu. Hakika, yeye (Allah) hawapendi wabadhirifu


1- - Aya hii ndio iliyoweka sharti la Muislamu kujisitiri kwa kuvaa nguo za heshima na sitara katika Swala. Na sio kuvaa nguo tu, lakini kuvaa nguo ya sitara, safi na inayopendeza. Kwa msingi huu, sio vyema kwa Muislamu kuswali akiwa amevaa nguo chafu au zenye michoro, picha na mandishi yasiyokuwa na lazima.


Surah: AL-AARAAF 

Ayah : 32

قُلۡ مَنۡ حَرَّمَ زِينَةَ ٱللَّهِ ٱلَّتِيٓ أَخۡرَجَ لِعِبَادِهِۦ وَٱلطَّيِّبَٰتِ مِنَ ٱلرِّزۡقِۚ قُلۡ هِيَ لِلَّذِينَ ءَامَنُواْ فِي ٱلۡحَيَوٰةِ ٱلدُّنۡيَا خَالِصَةٗ يَوۡمَ ٱلۡقِيَٰمَةِۗ كَذَٰلِكَ نُفَصِّلُ ٱلۡأٓيَٰتِ لِقَوۡمٖ يَعۡلَمُونَ

Sema: Hivi ni nani aliyeharamisha mapambo ya Allah ambayo ameyatoa kwa waja wake na riziki nzuri? Sema: Hayo (mapambo na riziki nzuri) ni kwa ajili ya wale walioamini katika maisha (yao) ya dunia, yakiwa halisi (ya peke yao) Siku ya Kiyama. Kama hivyo tunazifafanua Aya (zetu) kwa watu wanaojua



Surah: AL-AARAAF 

Ayah : 33

قُلۡ إِنَّمَا حَرَّمَ رَبِّيَ ٱلۡفَوَٰحِشَ مَا ظَهَرَ مِنۡهَا وَمَا بَطَنَ وَٱلۡإِثۡمَ وَٱلۡبَغۡيَ بِغَيۡرِ ٱلۡحَقِّ وَأَن تُشۡرِكُواْ بِٱللَّهِ مَا لَمۡ يُنَزِّلۡ بِهِۦ سُلۡطَٰنٗا وَأَن تَقُولُواْ عَلَى ٱللَّهِ مَا لَا تَعۡلَمُونَ

Sema: Hakika, ilivyo ni kwamba, Mola wangu Mlezi ameharamisha (mambo) machafu; ya dhahiri katika hayo na ya siri na dhambi na dhuluma bila ya haki yoyote,[1] na kuvishirikisha na Allah vitu ambavyo hakuviteremshia dalili (hoja) yoyote na (pia Allah ameharamisha) kumsemea Allah msiyoyajua


1- - Dhuluma bila ya haki ni dhuluma isiyokuwa na msingi wa kisheria. Ama kutekeleza haki kwa msingi wa sheria sio dhuluma wala ukandamizaji, ila tu limetumika neno dhuluma kwa ulinganifu wa lugha. Inayo onekana kama ni dhuluma kwenye macho ya wapingaji wa sheria za Allah ni kama kuuawa kwa mtu aliyethibitika kuua, kukatwa mkono mtu aliyethibitika kuiba n.k. Lakini hii sio dhuluma ila ni haki kwa sababu ni utekelezaji wa sheria.


Surah: AL-AARAAF 

Ayah : 34

وَلِكُلِّ أُمَّةٍ أَجَلٞۖ فَإِذَا جَآءَ أَجَلُهُمۡ لَا يَسۡتَأۡخِرُونَ سَاعَةٗ وَلَا يَسۡتَقۡدِمُونَ

Na kila umma una muda (wake); basi utakapofika muda wao hawatachelewesha hata saa moja wala hawatasogeza



Surah: AL-AARAAF 

Ayah : 35

يَٰبَنِيٓ ءَادَمَ إِمَّا يَأۡتِيَنَّكُمۡ رُسُلٞ مِّنكُمۡ يَقُصُّونَ عَلَيۡكُمۡ ءَايَٰتِي فَمَنِ ٱتَّقَىٰ وَأَصۡلَحَ فَلَا خَوۡفٌ عَلَيۡهِمۡ وَلَا هُمۡ يَحۡزَنُونَ

Enyi wanadamu, watakapo kufikieni Mitume watokanao na nyinyi wakikuhadithieni Aya zangu[1], basi yeyote atakayekuwa na uchaMungu na akafanya mema basi hawatakuwa na hofu yoyote, na hawatahuzunika


1- - Aya hii wanaitumia baadhi ya watu ili kupotosha. Wanadai kwamba, utume bado unaendelea. Itikadi ya Watu wa Sun ana Jama a ni kwamba, utume umekoma kwa Mtume Muhammad. Hakuna Mtume mwingine baada yake. Tujiulize swali la msingi. Aya hapa kama inasema kuwa Mitume wanaendelea kuja je, hizo Aya za Allah wanazotakiwa kutusomea ziko wapi? Rejea Aya ya 40, Sura Al-ahzab (33). Pia rejea Aya ya 158 ya Sura Al-aaraf (7).


Surah: AL-AARAAF 

Ayah : 36

وَٱلَّذِينَ كَذَّبُواْ بِـَٔايَٰتِنَا وَٱسۡتَكۡبَرُواْ عَنۡهَآ أُوْلَـٰٓئِكَ أَصۡحَٰبُ ٱلنَّارِۖ هُمۡ فِيهَا خَٰلِدُونَ

Na wale waliokadhibisha Aya zetu na kuzifanyia kiburi hao ni watu wa motoni, watakaa humo milele



Surah: AL-AARAAF 

Ayah : 37

فَمَنۡ أَظۡلَمُ مِمَّنِ ٱفۡتَرَىٰ عَلَى ٱللَّهِ كَذِبًا أَوۡ كَذَّبَ بِـَٔايَٰتِهِۦٓۚ أُوْلَـٰٓئِكَ يَنَالُهُمۡ نَصِيبُهُم مِّنَ ٱلۡكِتَٰبِۖ حَتَّىٰٓ إِذَا جَآءَتۡهُمۡ رُسُلُنَا يَتَوَفَّوۡنَهُمۡ قَالُوٓاْ أَيۡنَ مَا كُنتُمۡ تَدۡعُونَ مِن دُونِ ٱللَّهِۖ قَالُواْ ضَلُّواْ عَنَّا وَشَهِدُواْ عَلَىٰٓ أَنفُسِهِمۡ أَنَّهُمۡ كَانُواْ كَٰفِرِينَ

Basi, ni nani dhalimu zaidi kuliko yule aliyemzushia uwongo Allah au kuzikadhibisha Aya zake? Hao itawapata sehemu ya maandiko (aliyowaandikia Allah) mpaka watakapowafikia Wajumbe wetu wakiwatoa roho watasema: Wako wapi mliokuwa mkiwaomba (mukiwaabudu) badala ya Allah watasema: “Wametupotea” na wamejishuhudia wenyewe kwamba walikuwa makafiri



Surah: AL-AARAAF 

Ayah : 38

قَالَ ٱدۡخُلُواْ فِيٓ أُمَمٖ قَدۡ خَلَتۡ مِن قَبۡلِكُم مِّنَ ٱلۡجِنِّ وَٱلۡإِنسِ فِي ٱلنَّارِۖ كُلَّمَا دَخَلَتۡ أُمَّةٞ لَّعَنَتۡ أُخۡتَهَاۖ حَتَّىٰٓ إِذَا ٱدَّارَكُواْ فِيهَا جَمِيعٗا قَالَتۡ أُخۡرَىٰهُمۡ لِأُولَىٰهُمۡ رَبَّنَا هَـٰٓؤُلَآءِ أَضَلُّونَا فَـَٔاتِهِمۡ عَذَابٗا ضِعۡفٗا مِّنَ ٱلنَّارِۖ قَالَ لِكُلّٖ ضِعۡفٞ وَلَٰكِن لَّا تَعۡلَمُونَ

(Allah) Atasema: Ingieni Motoni (nyinyi) pamoja na mataifa yaliyopita kabla yenu, ambao ni majini na watu. Kila umma unapoingia utawalaani (umma) ndugu yake (mwenzake) mpaka watakapokusanyika humo wote kwa pamoja, watasema wa mwisho wao (kuwashitaki) wa mwanzo wao (kwamba): “Ewe Mola wetu Mlezi, hawa ndio waliotupoteza, basi wape adhabu ya moto maradufu”. (Allah) Atasema: Kila mmoja wenu ana (adhabu) mara dufu na lakini hamjui



Surah: AL-AARAAF 

Ayah : 39

وَقَالَتۡ أُولَىٰهُمۡ لِأُخۡرَىٰهُمۡ فَمَا كَانَ لَكُمۡ عَلَيۡنَا مِن فَضۡلٖ فَذُوقُواْ ٱلۡعَذَابَ بِمَا كُنتُمۡ تَكۡسِبُونَ

Na watasema wa mwanzo wao kuwaambia wa mwisho wao (kwamba): Nyinyi hamkuwa na fadhila yoyote kwetu, basi onjeni adhabu kwa sababu ya yale mliyokuwa mkiyachuma



Surah: AL-AARAAF 

Ayah : 40

إِنَّ ٱلَّذِينَ كَذَّبُواْ بِـَٔايَٰتِنَا وَٱسۡتَكۡبَرُواْ عَنۡهَا لَا تُفَتَّحُ لَهُمۡ أَبۡوَٰبُ ٱلسَّمَآءِ وَلَا يَدۡخُلُونَ ٱلۡجَنَّةَ حَتَّىٰ يَلِجَ ٱلۡجَمَلُ فِي سَمِّ ٱلۡخِيَاطِۚ وَكَذَٰلِكَ نَجۡزِي ٱلۡمُجۡرِمِينَ

Hakika, wale wanaozikadhibisha aya zetu na kuzifanyia kiburi, hawatafunguliwa milango ya mbinguni na hawataingia Peponi isipokuwa kama ngamia ataingia (atapenya) katika tundu ya sindano. Na kama hivyo tunawalipa waovu



Surah: AL-AARAAF 

Ayah : 41

لَهُم مِّن جَهَنَّمَ مِهَادٞ وَمِن فَوۡقِهِمۡ غَوَاشٖۚ وَكَذَٰلِكَ نَجۡزِي ٱلظَّـٰلِمِينَ

(Waovu) Jahanamu itakua kitanda chao na juu yao nguo za moto za kujifunika. Na hivyo ndivyo tunavowalipa madhalimu



Surah: AL-AARAAF 

Ayah : 42

وَٱلَّذِينَ ءَامَنُواْ وَعَمِلُواْ ٱلصَّـٰلِحَٰتِ لَا نُكَلِّفُ نَفۡسًا إِلَّا وُسۡعَهَآ أُوْلَـٰٓئِكَ أَصۡحَٰبُ ٱلۡجَنَّةِۖ هُمۡ فِيهَا خَٰلِدُونَ

Na wale walioamini na wakatenda yaliyo mema hatutamkalifisha mtu yeyote (kufanya) isipokuwa tu aliwezalo. Hao ndio watu wa Peponi, wao humo watakaa milele



Surah: AL-AARAAF 

Ayah : 43

وَنَزَعۡنَا مَا فِي صُدُورِهِم مِّنۡ غِلّٖ تَجۡرِي مِن تَحۡتِهِمُ ٱلۡأَنۡهَٰرُۖ وَقَالُواْ ٱلۡحَمۡدُ لِلَّهِ ٱلَّذِي هَدَىٰنَا لِهَٰذَا وَمَا كُنَّا لِنَهۡتَدِيَ لَوۡلَآ أَنۡ هَدَىٰنَا ٱللَّهُۖ لَقَدۡ جَآءَتۡ رُسُلُ رَبِّنَا بِٱلۡحَقِّۖ وَنُودُوٓاْ أَن تِلۡكُمُ ٱلۡجَنَّةُ أُورِثۡتُمُوهَا بِمَا كُنتُمۡ تَعۡمَلُونَ

Na tutaondoa husuda vifuani mwao, ikipita mito chini yao na watasema: “Kila sifa njema anaistahiki Allah ambaye ametuongoza kwenye hili na tusingeweza kuongoka kama Allah asingetuongoza”. Hakika kabisa, Mitume ya Allah imekuja kwa haki. Na (waumini huko peponi) wataitwa (na kuambiwa kwamba): Hii ndio pepo mliorithishwa kwa sababu ya yale mliyokuwa mkiyafanya



Surah: AL-AARAAF 

Ayah : 44

وَنَادَىٰٓ أَصۡحَٰبُ ٱلۡجَنَّةِ أَصۡحَٰبَ ٱلنَّارِ أَن قَدۡ وَجَدۡنَا مَا وَعَدَنَا رَبُّنَا حَقّٗا فَهَلۡ وَجَدتُّم مَّا وَعَدَ رَبُّكُمۡ حَقّٗاۖ قَالُواْ نَعَمۡۚ فَأَذَّنَ مُؤَذِّنُۢ بَيۡنَهُمۡ أَن لَّعۡنَةُ ٱللَّهِ عَلَى ٱلظَّـٰلِمِينَ

Na watu wa Peponi watawaita watu wa motoni (na kuwaambia): “Sisi kwa hakika tumekuta aliyotuahidi Mola wetu Mlezi ni kweli kabisa. Je, nyinyi mmekuta aliyowahidini Mola wenu ni kweli? (Watu wa Motoni) Watasema: Ndio. Basi atatangaza mtangazaji baina yao kwamba, laana ya Allah iwashukie madhalimu



Surah: AL-AARAAF 

Ayah : 45

ٱلَّذِينَ يَصُدُّونَ عَن سَبِيلِ ٱللَّهِ وَيَبۡغُونَهَا عِوَجٗا وَهُم بِٱلۡأٓخِرَةِ كَٰفِرُونَ

(Madhalimu) Ambao wanazuia (watu kufuata) njia ya Allah, na wanaitaka ipinde (iende vile wanavyotaka wao), na wao wanaikufuru Akhera



Surah: AL-AARAAF 

Ayah : 46

وَبَيۡنَهُمَا حِجَابٞۚ وَعَلَى ٱلۡأَعۡرَافِ رِجَالٞ يَعۡرِفُونَ كُلَّۢا بِسِيمَىٰهُمۡۚ وَنَادَوۡاْ أَصۡحَٰبَ ٱلۡجَنَّةِ أَن سَلَٰمٌ عَلَيۡكُمۡۚ لَمۡ يَدۡخُلُوهَا وَهُمۡ يَطۡمَعُونَ

Na baina yao (baina ya watu wa Peponi na watu wa Motoni) kuna kizuizi (cha muinuko/ukuta). Na juu ya muinuko (huo) kuna watu wanaowafahamu wote (watu wa Peponi na wa Motoni) kwa alama zao. Na watu wa muinuko (huo) watawaita watu wa Peponi (na kuwaambia): “Amani iwe kwenu” huku hawajaingia humo na wana tamaa (ya kuingia)



Surah: AL-AARAAF 

Ayah : 47

۞وَإِذَا صُرِفَتۡ أَبۡصَٰرُهُمۡ تِلۡقَآءَ أَصۡحَٰبِ ٱلنَّارِ قَالُواْ رَبَّنَا لَا تَجۡعَلۡنَا مَعَ ٱلۡقَوۡمِ ٱلظَّـٰلِمِينَ

Na (watu walioko kwenye muinuko) macho yao yatakapogeuzwa yatazame upande wa watu wa Motoni, watasema: “Ewe Mola wetu, usituweke pamoja na watu madhalimu”



Surah: AL-AARAAF 

Ayah : 48

وَنَادَىٰٓ أَصۡحَٰبُ ٱلۡأَعۡرَافِ رِجَالٗا يَعۡرِفُونَهُم بِسِيمَىٰهُمۡ قَالُواْ مَآ أَغۡنَىٰ عَنكُمۡ جَمۡعُكُمۡ وَمَا كُنتُمۡ تَسۡتَكۡبِرُونَ

Na watu wa muinuko watawaita watu (wa Motoni) wanaowafahamu kwa alama zao na kuwaambia: “Haukukusaidieni wingi wenu wala hicho mlichokuwa mnafanyia kiburi



Surah: AL-AARAAF 

Ayah : 49

أَهَـٰٓؤُلَآءِ ٱلَّذِينَ أَقۡسَمۡتُمۡ لَا يَنَالُهُمُ ٱللَّهُ بِرَحۡمَةٍۚ ٱدۡخُلُواْ ٱلۡجَنَّةَ لَا خَوۡفٌ عَلَيۡكُمۡ وَلَآ أَنتُمۡ تَحۡزَنُونَ

Hivi hawa ndio wale (waumini waliokuwa wanyonge) mliokuwa mkiwaapia kwamba Allah hatawafikishia rehema? Ingieni Peponi, hamna hofu wala hamtahuzunika



Surah: AL-AARAAF 

Ayah : 50

وَنَادَىٰٓ أَصۡحَٰبُ ٱلنَّارِ أَصۡحَٰبَ ٱلۡجَنَّةِ أَنۡ أَفِيضُواْ عَلَيۡنَا مِنَ ٱلۡمَآءِ أَوۡ مِمَّا رَزَقَكُمُ ٱللَّهُۚ قَالُوٓاْ إِنَّ ٱللَّهَ حَرَّمَهُمَا عَلَى ٱلۡكَٰفِرِينَ

Na watu motoni watawaita watu wa Peponi (na kuwaambia): Tumiminieni (kiasi japo kidogo cha) maji au katika vile (vitu vizuri) ambavyo Allah amekuruzukuni. (Watu wa Peponi) Watasema: Hakika, Allah ameviharamisha viwili hivyo kwa makafiri



Surah: AL-AARAAF 

Ayah : 51

ٱلَّذِينَ ٱتَّخَذُواْ دِينَهُمۡ لَهۡوٗا وَلَعِبٗا وَغَرَّتۡهُمُ ٱلۡحَيَوٰةُ ٱلدُّنۡيَاۚ فَٱلۡيَوۡمَ نَنسَىٰهُمۡ كَمَا نَسُواْ لِقَآءَ يَوۡمِهِمۡ هَٰذَا وَمَا كَانُواْ بِـَٔايَٰتِنَا يَجۡحَدُونَ

Ambao wameifanya dini yao pumbao na mchezo, na maisha ya dunia yakawadanganya. Basi leo tunawasahau kama walivyosahau kukutana na siku yao hii, na kwa sababu walikuwa wanazipinga Aya zetu



Surah: AL-AARAAF 

Ayah : 52

وَلَقَدۡ جِئۡنَٰهُم بِكِتَٰبٖ فَصَّلۡنَٰهُ عَلَىٰ عِلۡمٍ هُدٗى وَرَحۡمَةٗ لِّقَوۡمٖ يُؤۡمِنُونَ

Na kwa hakika kabisa tumewa-letea kitabu tulichokifafanua kwa elimu, kikiwa ni muongozo na rehema kwa watu wanaoamini



Surah: AL-AARAAF 

Ayah : 53

هَلۡ يَنظُرُونَ إِلَّا تَأۡوِيلَهُۥۚ يَوۡمَ يَأۡتِي تَأۡوِيلُهُۥ يَقُولُ ٱلَّذِينَ نَسُوهُ مِن قَبۡلُ قَدۡ جَآءَتۡ رُسُلُ رَبِّنَا بِٱلۡحَقِّ فَهَل لَّنَا مِن شُفَعَآءَ فَيَشۡفَعُواْ لَنَآ أَوۡ نُرَدُّ فَنَعۡمَلَ غَيۡرَ ٱلَّذِي كُنَّا نَعۡمَلُۚ قَدۡ خَسِرُوٓاْ أَنفُسَهُمۡ وَضَلَّ عَنۡهُم مَّا كَانُواْ يَفۡتَرُونَ

Hawana wanachongoja isipokuwa tu matokeo yake. Siku yatakapokuja matokeo yake watasema wale waliokisahau (kitabu walicholetewa) kabla ya hapo kwamba: “Hakika, walikuja Mitume wa Mola wetu kwa haki. Basi je, kuna waombezi watuombee au turudishwe (duniani) na tufanye tofauti ya yale tuliyokuwa tunayafanya? Kwa hakika, wamezitia hasara nafsi zao, na yamewapotea yote waliyokuwa wakiyazusha



Surah: AL-AARAAF 

Ayah : 54

إِنَّ رَبَّكُمُ ٱللَّهُ ٱلَّذِي خَلَقَ ٱلسَّمَٰوَٰتِ وَٱلۡأَرۡضَ فِي سِتَّةِ أَيَّامٖ ثُمَّ ٱسۡتَوَىٰ عَلَى ٱلۡعَرۡشِۖ يُغۡشِي ٱلَّيۡلَ ٱلنَّهَارَ يَطۡلُبُهُۥ حَثِيثٗا وَٱلشَّمۡسَ وَٱلۡقَمَرَ وَٱلنُّجُومَ مُسَخَّرَٰتِۭ بِأَمۡرِهِۦٓۗ أَلَا لَهُ ٱلۡخَلۡقُ وَٱلۡأَمۡرُۗ تَبَارَكَ ٱللَّهُ رَبُّ ٱلۡعَٰلَمِينَ

Hakika, Mola wenu Mlezi ni Allah ambaye ameziumba mbingu na ardhi katika siku sita, kisha akastawi juu ya Arshi. Anaufunika usiku kwa kuleta mchana, ukiufuata kwa haraka, na (ameumba) jua na mwezi na nyota vikiwa vimetiishwa (vimefanywa vitiifu kwa mwana-damu) kwa amri yake. Elewa (kwamba): kuumba na kuamrisha Ni kwake yeye tu. Ametukuka Allah, Mola Mlezi wa walimwengu wote



Surah: AL-AARAAF 

Ayah : 55

ٱدۡعُواْ رَبَّكُمۡ تَضَرُّعٗا وَخُفۡيَةًۚ إِنَّهُۥ لَا يُحِبُّ ٱلۡمُعۡتَدِينَ

Muombeni Mola wenu Mlezi kwa unyenyekevu na kificho (kimya kimya). Hakika, yeye (Allah) hawapendi wavukao mipaka (ya sheria zake)



Surah: AL-AARAAF 

Ayah : 56

وَلَا تُفۡسِدُواْ فِي ٱلۡأَرۡضِ بَعۡدَ إِصۡلَٰحِهَا وَٱدۡعُوهُ خَوۡفٗا وَطَمَعًاۚ إِنَّ رَحۡمَتَ ٱللَّهِ قَرِيبٞ مِّنَ ٱلۡمُحۡسِنِينَ

Na msifanye uharibifu katika ardhi baada ya (ya Allah) kutengeneza na muombeni yeye (tu) kwa kuogopa (adhabu yake) na kutumai (rehema zake). Hakika, rehema za Allah zipo karibu na wenye kufanya mazuri



Surah: AL-AARAAF 

Ayah : 57

وَهُوَ ٱلَّذِي يُرۡسِلُ ٱلرِّيَٰحَ بُشۡرَۢا بَيۡنَ يَدَيۡ رَحۡمَتِهِۦۖ حَتَّىٰٓ إِذَآ أَقَلَّتۡ سَحَابٗا ثِقَالٗا سُقۡنَٰهُ لِبَلَدٖ مَّيِّتٖ فَأَنزَلۡنَا بِهِ ٱلۡمَآءَ فَأَخۡرَجۡنَا بِهِۦ مِن كُلِّ ٱلثَّمَرَٰتِۚ كَذَٰلِكَ نُخۡرِجُ ٱلۡمَوۡتَىٰ لَعَلَّكُمۡ تَذَكَّرُونَ

Na Yeye ndiye apelekae pepo zikiwa bishara ya kufika kwa rehema zake, hadi (pepo hizo) zinapobeba mawingu mazito tunayachunga (na kuyapeleka) kwenye mji uliokufa (kwa ukame) na tunateremsha hapo maji (mvua). Basi tukaotesha kwa mvua hizo kila aina ya matunda. Kama hivyo tunawafufua waliokufa, ili mpate kuonyeka



Surah: AL-AARAAF 

Ayah : 58

وَٱلۡبَلَدُ ٱلطَّيِّبُ يَخۡرُجُ نَبَاتُهُۥ بِإِذۡنِ رَبِّهِۦۖ وَٱلَّذِي خَبُثَ لَا يَخۡرُجُ إِلَّا نَكِدٗاۚ كَذَٰلِكَ نُصَرِّفُ ٱلۡأٓيَٰتِ لِقَوۡمٖ يَشۡكُرُونَ

Na nchi (ardhi) nzuri hutoa mimea yake kwa idhini ya Mola wake na nchi (ardhi) iliyokuwa mbaya haitoki (mimeya yake) ila kwa taabu mno. Kama hivyo tunazifafanua aya kwa watu wanaoshukuru



Surah: AL-AARAAF 

Ayah : 59

لَقَدۡ أَرۡسَلۡنَا نُوحًا إِلَىٰ قَوۡمِهِۦ فَقَالَ يَٰقَوۡمِ ٱعۡبُدُواْ ٱللَّهَ مَا لَكُم مِّنۡ إِلَٰهٍ غَيۡرُهُۥٓ إِنِّيٓ أَخَافُ عَلَيۡكُمۡ عَذَابَ يَوۡمٍ عَظِيمٖ

Kwa hakika kabisa, tulimpeleka Nuhu kwa watu wake, akasema: Enyi watu wangu, muabuduni Allah (tu). Nyinyi hamna Mola mwingine zaidi yake. Hakika, mimi nakuhofieni (kupata) adhabu ya siku kubwa sana



Surah: AL-AARAAF 

Ayah : 60

قَالَ ٱلۡمَلَأُ مِن قَوۡمِهِۦٓ إِنَّا لَنَرَىٰكَ فِي ضَلَٰلٖ مُّبِينٖ

Kundi la mamwinyi katika watu wake lilisema kuwa: Hakika, sisi tunakuona umo katika upotevu uliodhahiri sana