Surah: AN-FAL 

Ayah : 1

يَسۡـَٔلُونَكَ عَنِ ٱلۡأَنفَالِۖ قُلِ ٱلۡأَنفَالُ لِلَّهِ وَٱلرَّسُولِۖ فَٱتَّقُواْ ٱللَّهَ وَأَصۡلِحُواْ ذَاتَ بَيۡنِكُمۡۖ وَأَطِيعُواْ ٱللَّهَ وَرَسُولَهُۥٓ إِن كُنتُم مُّؤۡمِنِينَ

(Ewe Nabii) Wanakuuliza kuhusu (utaratibu wa ugawaji wa) Ngawira. Sema: Ngawira ni za Allah na Mtume (wao ndio watoaji wa utaratibu wa mgao wake). Basi mcheni Allah (kwa kutekeleza amri zake na kujiepusha na makatazo yake) na tatueni migogoro baina yenu, na mtiini Allah na Mtume wake ikiwa nyinyi ni Waumini



Surah: AN-FAL 

Ayah : 2

إِنَّمَا ٱلۡمُؤۡمِنُونَ ٱلَّذِينَ إِذَا ذُكِرَ ٱللَّهُ وَجِلَتۡ قُلُوبُهُمۡ وَإِذَا تُلِيَتۡ عَلَيۡهِمۡ ءَايَٰتُهُۥ زَادَتۡهُمۡ إِيمَٰنٗا وَعَلَىٰ رَبِّهِمۡ يَتَوَكَّلُونَ

Kwa hakika kabisa, Waumini (kamili) ni wale ambao anapotajwa Allah nyoyo zao hujaa hofu, na wanaposomewa Aya zake huwaongezea imani, na wanamtegemea Mola wao Mlezi tu



Surah: AN-FAL 

Ayah : 3

ٱلَّذِينَ يُقِيمُونَ ٱلصَّلَوٰةَ وَمِمَّا رَزَقۡنَٰهُمۡ يُنفِقُونَ

(Waumini) Ambao wanasi-mamisha Swala (wanadumu katika kuswali kwa kukidhi vigezo na masharti ya Swala) na katika vile tulivyowaruzuku wanavitoa (katika njia za heri)



Surah: AN-FAL 

Ayah : 4

أُوْلَـٰٓئِكَ هُمُ ٱلۡمُؤۡمِنُونَ حَقّٗاۚ لَّهُمۡ دَرَجَٰتٌ عِندَ رَبِّهِمۡ وَمَغۡفِرَةٞ وَرِزۡقٞ كَرِيمٞ

Hao (wenye sifa tajwa) ndio Waumini kweli kweli. Wana daraja (za juu ambazo ni makazi mazuri) kwa Mola wao Mlezi na msamaha na riziki bora mno (huko Peponi)



Surah: AN-FAL 

Ayah : 5

كَمَآ أَخۡرَجَكَ رَبُّكَ مِنۢ بَيۡتِكَ بِٱلۡحَقِّ وَإِنَّ فَرِيقٗا مِّنَ ٱلۡمُؤۡمِنِينَ لَكَٰرِهُونَ

Kama Mola wako Mlezi alivyokutoa nyumbani kwako (Madina) kwa haki (kwenda vitani na Swahaba wanachukia kwa kuwa wachache na hawakuwa na maandalizi ya vita), na kwa hakika kabisa kundi moja miongoni mwa Waumini lilikereka sana



Surah: AN-FAL 

Ayah : 6

يُجَٰدِلُونَكَ فِي ٱلۡحَقِّ بَعۡدَ مَا تَبَيَّنَ كَأَنَّمَا يُسَاقُونَ إِلَى ٱلۡمَوۡتِ وَهُمۡ يَنظُرُونَ

Wanajadiliana nawe katika jambo la haki (vita) baada ya kuwa limeshakuwa bayana (na kwa kuogopa kwao vita ilikuwa) kama kwamba wanaswagwa kupelekwa kwenye kifo huku wanatazama



Surah: AN-FAL 

Ayah : 7

وَإِذۡ يَعِدُكُمُ ٱللَّهُ إِحۡدَى ٱلطَّآئِفَتَيۡنِ أَنَّهَا لَكُمۡ وَتَوَدُّونَ أَنَّ غَيۡرَ ذَاتِ ٱلشَّوۡكَةِ تَكُونُ لَكُمۡ وَيُرِيدُ ٱللَّهُ أَن يُحِقَّ ٱلۡحَقَّ بِكَلِمَٰتِهِۦ وَيَقۡطَعَ دَابِرَ ٱلۡكَٰفِرِينَ

Na (kumbukeni) wakati Allah anakuahidini kuwa, moja ya makundi mawili ni lenu. Nanyi mkapenda kundi lisilokuwa na silaha ndio liwe lenu. Na Allah anataka aisimamishe haki kwa maneno yake, na aukate mzizi wa makafiri (awaangamize)



Surah: AN-FAL 

Ayah : 8

لِيُحِقَّ ٱلۡحَقَّ وَيُبۡطِلَ ٱلۡبَٰطِلَ وَلَوۡ كَرِهَ ٱلۡمُجۡرِمُونَ

(Allah ameyafanya hayo) Ili aisimamishe haki na ateketeze batili (ukafiri) na hata kama waovu watachukia



Surah: AN-FAL 

Ayah : 9

إِذۡ تَسۡتَغِيثُونَ رَبَّكُمۡ فَٱسۡتَجَابَ لَكُمۡ أَنِّي مُمِدُّكُم بِأَلۡفٖ مِّنَ ٱلۡمَلَـٰٓئِكَةِ مُرۡدِفِينَ

(Kumbukeni) Wakati mna-muomba msaada Mola wenu Mlezi akuokoeni (dhidi ya maadui zenu), akakujibuni kuwa: Kwa yakini Mimi nitakusaidieni kwa (kuleta vikosi vya) Malaika elfu moja wanaofuatana mfululizo



Surah: AN-FAL 

Ayah : 10

وَمَا جَعَلَهُ ٱللَّهُ إِلَّا بُشۡرَىٰ وَلِتَطۡمَئِنَّ بِهِۦ قُلُوبُكُمۡۚ وَمَا ٱلنَّصۡرُ إِلَّا مِنۡ عِندِ ٱللَّهِۚ إِنَّ ٱللَّهَ عَزِيزٌ حَكِيمٌ

Na Allah hakulifanya (hili la kuleta vikosi vya Malaika) ila liwe bishara na ili kwalo nyoyo zenu zituwe (zitulizane). Na (ili hatimae mjue kwamba,) haupatikani ushindi ila kutoka kwa Allah tu. Hakika Allah ni Mwenye nguvu, Mwenye hekima



Surah: AN-FAL 

Ayah : 11

إِذۡ يُغَشِّيكُمُ ٱلنُّعَاسَ أَمَنَةٗ مِّنۡهُ وَيُنَزِّلُ عَلَيۡكُم مِّنَ ٱلسَّمَآءِ مَآءٗ لِّيُطَهِّرَكُم بِهِۦ وَيُذۡهِبَ عَنكُمۡ رِجۡزَ ٱلشَّيۡطَٰنِ وَلِيَرۡبِطَ عَلَىٰ قُلُوبِكُمۡ وَيُثَبِّتَ بِهِ ٱلۡأَقۡدَامَ

(Kumbukeni) Wakati (Allah) anakugubikeni kwa lepe la usingizi (kwenye usiku wa kuamkia vita) kwa ajili ya amani na utulivu kutoka kwake, na anakuteremshieni maji (mvua) kutoka mawinguni ili kwayo akusafisheni (Hadathi na Janaba) na kukuondoleeni wasiwasi wa Shetani (hofu), na ili azipe nguvu nyoyo zenu, na kwa (yote) hayo aiimarishe miguu yenu (isitetereke kwenye medani ya vita)



Surah: AN-FAL 

Ayah : 12

إِذۡ يُوحِي رَبُّكَ إِلَى ٱلۡمَلَـٰٓئِكَةِ أَنِّي مَعَكُمۡ فَثَبِّتُواْ ٱلَّذِينَ ءَامَنُواْۚ سَأُلۡقِي فِي قُلُوبِ ٱلَّذِينَ كَفَرُواْ ٱلرُّعۡبَ فَٱضۡرِبُواْ فَوۡقَ ٱلۡأَعۡنَاقِ وَٱضۡرِبُواْ مِنۡهُمۡ كُلَّ بَنَانٖ

(Kumbuka) Wakati Mola wako Mlezi alipowapa Wahyi (vikosi vya) Malaika kwamba: Hakika Mimi nipo pamoja nanyi (kwa kukusaidieni na kukupeni ushindi), basi watieni nguvu walioamini (kwa kuwapa bishara njema). Nitatia woga kwenye nyoyo za waliokufuru (hadi washindwe). Basi wapigeni juu ya shingo (vichwani) na wapigeni kwenye kila ncha za vidole (vya mikono na miguu)



Surah: AN-FAL 

Ayah : 13

ذَٰلِكَ بِأَنَّهُمۡ شَآقُّواْ ٱللَّهَ وَرَسُولَهُۥۚ وَمَن يُشَاقِقِ ٱللَّهَ وَرَسُولَهُۥ فَإِنَّ ٱللَّهَ شَدِيدُ ٱلۡعِقَابِ

Hilo (la kuwapiga Washirikina) ni kwasababu wamemuasi Allah na Mtume wake (na kuwafurusha waumini kwenye miji yao). Na mwenye kumuasi Allah na Mtume wake basi (ajue) Allah ni Mkali wa kuadhibu



Surah: AN-FAL 

Ayah : 14

ذَٰلِكُمۡ فَذُوقُوهُ وَأَنَّ لِلۡكَٰفِرِينَ عَذَابَ ٱلنَّارِ

Hiyo (adhabu ya awali mliyoipata enyi makafiri ya kukatwa shingo na vidole vitani) basi ionjeni. Na bila ya shaka makafiri wana adhabu ya Moto (Akhera)



Surah: AN-FAL 

Ayah : 15

يَـٰٓأَيُّهَا ٱلَّذِينَ ءَامَنُوٓاْ إِذَا لَقِيتُمُ ٱلَّذِينَ كَفَرُواْ زَحۡفٗا فَلَا تُوَلُّوهُمُ ٱلۡأَدۡبَارَ

Enyi Mlioamini, mkikutana na (kundi la majeshi ya) waliokufuru uso kwa uso (vitani) msiwageuzie mgongo (msiwakimbie)



Surah: AN-FAL 

Ayah : 16

وَمَن يُوَلِّهِمۡ يَوۡمَئِذٖ دُبُرَهُۥٓ إِلَّا مُتَحَرِّفٗا لِّقِتَالٍ أَوۡ مُتَحَيِّزًا إِلَىٰ فِئَةٖ فَقَدۡ بَآءَ بِغَضَبٖ مِّنَ ٱللَّهِ وَمَأۡوَىٰهُ جَهَنَّمُۖ وَبِئۡسَ ٱلۡمَصِيرُ

Na yeyote atakayewageuzia mgongo wake siku hiyo (atakayewakimbia) isipokuwa kama (amefanya hivyo kama) mbinu za vita (geresha) au kuungana na kikosi (cha wapiganaji wenzake), basi atakuwa amestahiki ghadhabu kutoka kwa Allah na makazi yake ni Jahanamu, na huo ni mwisho mbaya mno



Surah: AN-FAL 

Ayah : 17

فَلَمۡ تَقۡتُلُوهُمۡ وَلَٰكِنَّ ٱللَّهَ قَتَلَهُمۡۚ وَمَا رَمَيۡتَ إِذۡ رَمَيۡتَ وَلَٰكِنَّ ٱللَّهَ رَمَىٰ وَلِيُبۡلِيَ ٱلۡمُؤۡمِنِينَ مِنۡهُ بَلَآءً حَسَنًاۚ إِنَّ ٱللَّهَ سَمِيعٌ عَلِيمٞ

Basi (Kwenye Siku ya Badri) hamkuwaua nyinyi (hao makafiri kwa nguvu na uhodari wenu) lakini Allah ndiye aliyewaua. Na wewe (Muhammad) hukutupa (na kuufikisha mchanga kwenye nyuso za makafiri), lakini Allah ndiye aliyetupa (aliyeufikisha mchanga na ukawapata makafiri), na ili awajaribu Waumini kutokana na hayo majaribio mazuri (kwa kuwapa neema ya ngawira walio hai na waliouawa wakiwa mashahidi). Hakika Allah ni Msikivu, Mjuzi sana



Surah: AN-FAL 

Ayah : 18

ذَٰلِكُمۡ وَأَنَّ ٱللَّهَ مُوهِنُ كَيۡدِ ٱلۡكَٰفِرِينَ

(Tukio hilo la vita vya Badri lililenga kuwatahini waumini), na hakika Allah ni Mwenye kudhoofisha njama za makafiri



Surah: AN-FAL 

Ayah : 19

إِن تَسۡتَفۡتِحُواْ فَقَدۡ جَآءَكُمُ ٱلۡفَتۡحُۖ وَإِن تَنتَهُواْ فَهُوَ خَيۡرٞ لَّكُمۡۖ وَإِن تَعُودُواْ نَعُدۡ وَلَن تُغۡنِيَ عَنكُمۡ فِئَتُكُمۡ شَيۡـٔٗا وَلَوۡ كَثُرَتۡ وَأَنَّ ٱللَّهَ مَعَ ٱلۡمُؤۡمِنِينَ

Kama mnataka ushindi (kwenye vita) basi ushindi ume-kwishakujieni[1]. Na mkiacha (kupigana na Mtume na Waislamu) itakuwa ndio heri kwenu (duniani na Akhera). Na mkirejea (kupigana na Mtume na Waislamu) sisi pia tutarejea (kuwapa kichapo na kipigo) na katu kundi (jeshi) lenu halitakufaeni kitu chochote, hata kama litakuwa kubwa, na kwa hakika Allah yupo pamoja na waumini


1- - Hapa wanaambiwa makafiri kwa lugha ya kuwakejeli kwamba mnataka kuwashinda Waislamu basi mmekwishaupata kwa kichapo mlichokipata katika vita vya Badri! Walichokipata ni kipigo na sio ushindi!


Surah: AN-FAL 

Ayah : 20

يَـٰٓأَيُّهَا ٱلَّذِينَ ءَامَنُوٓاْ أَطِيعُواْ ٱللَّهَ وَرَسُولَهُۥ وَلَا تَوَلَّوۡاْ عَنۡهُ وَأَنتُمۡ تَسۡمَعُونَ

Enyi mlioamini, mtiini Allah na Mtume wake (kwa wanayo kuamrisheni au kukukatazeni), na msiigeuke (msiipinge) amri hiyo (ya kumtii Allah na Mtume wake) na ilhali mnasikia (wanayokuambieni)



Surah: AN-FAL 

Ayah : 21

وَلَا تَكُونُواْ كَٱلَّذِينَ قَالُواْ سَمِعۡنَا وَهُمۡ لَا يَسۡمَعُونَ

Na msiwe kama wale waliosema: Tumesikia, na kumbe hawasikii.[1]


1- - Hawa ni wanafiki, Wayahudi na washirikishaji waliokuwa wanadai kuwa wanaisikia Qur’an, mawaidha na kuizingatia kumbe hawako hivyo. Waislamu tunakatazwa tusiwe kama hao.


Surah: AN-FAL 

Ayah : 22

۞إِنَّ شَرَّ ٱلدَّوَآبِّ عِندَ ٱللَّهِ ٱلصُّمُّ ٱلۡبُكۡمُ ٱلَّذِينَ لَا يَعۡقِلُونَ

Hakika viumbe waovu sana mbele ya Allah ni hawa (wanaojifanya) viziwi (wa kuisikia haki), mabubu (wa kutosema kweli) ambao hawatumii akili (katika kupambanua haki na batili)



Surah: AN-FAL 

Ayah : 23

وَلَوۡ عَلِمَ ٱللَّهُ فِيهِمۡ خَيۡرٗا لَّأَسۡمَعَهُمۡۖ وَلَوۡ أَسۡمَعَهُمۡ لَتَوَلَّواْ وَّهُم مُّعۡرِضُونَ

Na laiti Allah angejua kwamba kwenye nafsi zao kuna kheri yoyote, kwa yakini kabisa angewasikilizisha. Na lau angewasikilizisha wangeligeuka na huku wakipuuza (kwa ukaidi)



Surah: AN-FAL 

Ayah : 24

يَـٰٓأَيُّهَا ٱلَّذِينَ ءَامَنُواْ ٱسۡتَجِيبُواْ لِلَّهِ وَلِلرَّسُولِ إِذَا دَعَاكُمۡ لِمَا يُحۡيِيكُمۡۖ وَٱعۡلَمُوٓاْ أَنَّ ٱللَّهَ يَحُولُ بَيۡنَ ٱلۡمَرۡءِ وَقَلۡبِهِۦ وَأَنَّهُۥٓ إِلَيۡهِ تُحۡشَرُونَ

Enyi mlioamini, muitikeni Allah na Mtume wanapokuiteni kwenye jambo linalokupeni uzima. Na jueni kuwa Allah huingia kati (na kujua yanayojiri) kati ya mtu na moyo wake, na kwamba kwake Yeye tu mtakusanywa (na kulipwa)



Surah: AN-FAL 

Ayah : 25

وَٱتَّقُواْ فِتۡنَةٗ لَّا تُصِيبَنَّ ٱلَّذِينَ ظَلَمُواْ مِنكُمۡ خَآصَّةٗۖ وَٱعۡلَمُوٓاْ أَنَّ ٱللَّهَ شَدِيدُ ٱلۡعِقَابِ

Na (enyi waumini) jihadharini na fitina (kujiingiza kwenye majanga) ambayo hayatowasibu waliodhulumu (waliofanya uovu) tu miongoni mwenu. Na jueni kuwa Allah ni Mkali wa kuadhibu



Surah: AN-FAL 

Ayah : 26

وَٱذۡكُرُوٓاْ إِذۡ أَنتُمۡ قَلِيلٞ مُّسۡتَضۡعَفُونَ فِي ٱلۡأَرۡضِ تَخَافُونَ أَن يَتَخَطَّفَكُمُ ٱلنَّاسُ فَـَٔاوَىٰكُمۡ وَأَيَّدَكُم بِنَصۡرِهِۦ وَرَزَقَكُم مِّنَ ٱلطَّيِّبَٰتِ لَعَلَّكُمۡ تَشۡكُرُونَ

Na kumbukeni (Enyi Muhajirina) mlipokuwa wachache mnaonyanyaswa katika ardhi (ya Makkah), mnaogopa watu wasikunyakueni (na kukuteseni), basi (Allah) akakupeni hifadhi (mahali pazuri pa kuishi ambapo ni mji wa Madina), na akakutieni nguvu kwa nusra yake, na akakupeni riziki nzuri ili mpate kushukuru



Surah: AN-FAL 

Ayah : 27

يَـٰٓأَيُّهَا ٱلَّذِينَ ءَامَنُواْ لَا تَخُونُواْ ٱللَّهَ وَٱلرَّسُولَ وَتَخُونُوٓاْ أَمَٰنَٰتِكُمۡ وَأَنتُمۡ تَعۡلَمُونَ

Enyi mlioamini, msimfanyie hiana Allah na Mtume (kwa kuvunja ahadi na makubaliano ya imani zenu), wala msifanyie khiyana amana zenu (mnazoaminiana), na ilhali mnajua



Surah: AN-FAL 

Ayah : 28

وَٱعۡلَمُوٓاْ أَنَّمَآ أَمۡوَٰلُكُمۡ وَأَوۡلَٰدُكُمۡ فِتۡنَةٞ وَأَنَّ ٱللَّهَ عِندَهُۥٓ أَجۡرٌ عَظِيمٞ

Na jueni ya kwamba, hakika mali zenu na watoto ni mtihani[1], na kwamba kwa Allah kuna ujira mkubwa mno


1- - Mali na watoto ni mtihani unaoweza kumuingiza mtu katika mitihani kwa kuwa na kiburi au kufanya mambo ya haramu kwa sababu ya mali au watoto.


Surah: AN-FAL 

Ayah : 29

يَـٰٓأَيُّهَا ٱلَّذِينَ ءَامَنُوٓاْ إِن تَتَّقُواْ ٱللَّهَ يَجۡعَل لَّكُمۡ فُرۡقَانٗا وَيُكَفِّرۡ عَنكُمۡ سَيِّـَٔاتِكُمۡ وَيَغۡفِرۡ لَكُمۡۗ وَٱللَّهُ ذُو ٱلۡفَضۡلِ ٱلۡعَظِيمِ

Enyi mlioamini, mkimcha Allah atakufanyieni kipambanuzi (kinachokuwezesheni kupambanua kati ya haki na batili), na atakusameheni na kukufutieni makosa yenu. Na Allah ni Mwenye fadhila kubwa mno



Surah: AN-FAL 

Ayah : 30

وَإِذۡ يَمۡكُرُ بِكَ ٱلَّذِينَ كَفَرُواْ لِيُثۡبِتُوكَ أَوۡ يَقۡتُلُوكَ أَوۡ يُخۡرِجُوكَۚ وَيَمۡكُرُونَ وَيَمۡكُرُ ٱللَّهُۖ وَٱللَّهُ خَيۡرُ ٱلۡمَٰكِرِينَ

Na (kumbuka) wakati waliokufuru wanakupangia njama (pale Makkah kwenye Darun Nad’wa ima) wakufunge (wakuweke kizuizini) au wakuue au wakutoe (wakufukuze). Na wanapanga njama (hiyo kwa siri) na Allah anapanga njama (zake). Na Allah ndiye Mbora wa wanaopindua njama