وَإِذۡ قَالَ مُوسَىٰ لِقَوۡمِهِ ٱذۡكُرُواْ نِعۡمَةَ ٱللَّهِ عَلَيۡكُمۡ إِذۡ أَنجَىٰكُم مِّنۡ ءَالِ فِرۡعَوۡنَ يَسُومُونَكُمۡ سُوٓءَ ٱلۡعَذَابِ وَيُذَبِّحُونَ أَبۡنَآءَكُمۡ وَيَسۡتَحۡيُونَ نِسَآءَكُمۡۚ وَفِي ذَٰلِكُم بَلَآءٞ مِّن رَّبِّكُمۡ عَظِيمٞ
Na (kumbuka) Mussa alipo-waambia watu wake: Kumbukeni neema ya Allah aliyokujaalieni, pale alipokuokoeni kutokana na watu wa Firauni waliokupeni adhabu mbaya kabisa, wakiwachinja watoto wenu wanaume, na wakiwaacha hai wanawake. Na katika hayo ulikuwa mtihani mkubwa unaotoka kwa Mola wenu Mlezi
وَإِذۡ تَأَذَّنَ رَبُّكُمۡ لَئِن شَكَرۡتُمۡ لَأَزِيدَنَّكُمۡۖ وَلَئِن كَفَرۡتُمۡ إِنَّ عَذَابِي لَشَدِيدٞ
Na alipotangaza Mola wenu Mlezi (kwamba): iwapo mtani-shukuru nitakuzidishieni; na iwapo mtanikufuru, basi adhabu yangu ni kali mno
وَقَالَ مُوسَىٰٓ إِن تَكۡفُرُوٓاْ أَنتُمۡ وَمَن فِي ٱلۡأَرۡضِ جَمِيعٗا فَإِنَّ ٱللَّهَ لَغَنِيٌّ حَمِيدٌ
Na Mussa alisema: Iwapo nyinyi mtakufuru na wote waliomo duniani, hakika Allah ni Mkwasi mno, Msifiwa
أَلَمۡ يَأۡتِكُمۡ نَبَؤُاْ ٱلَّذِينَ مِن قَبۡلِكُمۡ قَوۡمِ نُوحٖ وَعَادٖ وَثَمُودَ وَٱلَّذِينَ مِنۢ بَعۡدِهِمۡ لَا يَعۡلَمُهُمۡ إِلَّا ٱللَّهُۚ جَآءَتۡهُمۡ رُسُلُهُم بِٱلۡبَيِّنَٰتِ فَرَدُّوٓاْ أَيۡدِيَهُمۡ فِيٓ أَفۡوَٰهِهِمۡ وَقَالُوٓاْ إِنَّا كَفَرۡنَا بِمَآ أُرۡسِلۡتُم بِهِۦ وَإِنَّا لَفِي شَكّٖ مِّمَّا تَدۡعُونَنَآ إِلَيۡهِ مُرِيبٖ
Je, hazikukufikieni habari za baadhi ya waliokuwa kabla yenu? Kaumu ya Nuhu, na A’adi, na Thamud, na waliofuata baada yao, ambao hapana awajuaye ila Allah? Mitume wao waliwajia kwa hoja zilizo wazi, na wao wakarudisha mikono yao kwenye vinywa vyao, wakasema: Hakika sisi hatuyataki hayo mliyotumwa kwayo, na hakika sisi tuna shaka kubwa na mnayotuitia
۞قَالَتۡ رُسُلُهُمۡ أَفِي ٱللَّهِ شَكّٞ فَاطِرِ ٱلسَّمَٰوَٰتِ وَٱلۡأَرۡضِۖ يَدۡعُوكُمۡ لِيَغۡفِرَ لَكُم مِّن ذُنُوبِكُمۡ وَيُؤَخِّرَكُمۡ إِلَىٰٓ أَجَلٖ مُّسَمّٗىۚ قَالُوٓاْ إِنۡ أَنتُمۡ إِلَّا بَشَرٞ مِّثۡلُنَا تُرِيدُونَ أَن تَصُدُّونَا عَمَّا كَانَ يَعۡبُدُ ءَابَآؤُنَا فَأۡتُونَا بِسُلۡطَٰنٖ مُّبِينٖ
Mitume wao walisema: Je, kuna shaka na Allah, Muumba mbingu na ardhi? Yeye anakuiteni ili apate kukufutieni madhambi yenu, na akupeni muhula (wa adhabu angamizi) mpaka muda uliowekwa (ufike). Walisema: Nyinyi si chochote ila ni wanadamu tu kama sisi. Mnataka kutuzuia na waliyokuwa wanayaabudu Baba zetu. Basi tuleteeni hoja ilio wazi
قَالَتۡ لَهُمۡ رُسُلُهُمۡ إِن نَّحۡنُ إِلَّا بَشَرٞ مِّثۡلُكُمۡ وَلَٰكِنَّ ٱللَّهَ يَمُنُّ عَلَىٰ مَن يَشَآءُ مِنۡ عِبَادِهِۦۖ وَمَا كَانَ لَنَآ أَن نَّأۡتِيَكُم بِسُلۡطَٰنٍ إِلَّا بِإِذۡنِ ٱللَّهِۚ وَعَلَى ٱللَّهِ فَلۡيَتَوَكَّلِ ٱلۡمُؤۡمِنُونَ
Mitume wao waliwaambia: Sisi kweli si chochote (kimaumbo) ila ni wanadamu kama nyinyi. Lakini Allah humfanyia hisani amtakaye katika waja wake. Wala sisi hatuwezi kuleta uthibitisho ila kwa idhini ya Allah. Na kwa Allah tu ndio wategemee Waumini
وَمَا لَنَآ أَلَّا نَتَوَكَّلَ عَلَى ٱللَّهِ وَقَدۡ هَدَىٰنَا سُبُلَنَاۚ وَلَنَصۡبِرَنَّ عَلَىٰ مَآ ءَاذَيۡتُمُونَاۚ وَعَلَى ٱللَّهِ فَلۡيَتَوَكَّلِ ٱلۡمُتَوَكِّلُونَ
Na wala hatuna udhuru (wa kwa) nini tusimtegemee Allah, na hali Yeye ametuongoa kwenye Njia zetu. Na hapana shaka sisi tutavumilia hizo kero mlizotuudhi kwazo. Na kwa Allah tu wategemee wanaotegemea
وَقَالَ ٱلَّذِينَ كَفَرُواْ لِرُسُلِهِمۡ لَنُخۡرِجَنَّكُم مِّنۡ أَرۡضِنَآ أَوۡ لَتَعُودُنَّ فِي مِلَّتِنَاۖ فَأَوۡحَىٰٓ إِلَيۡهِمۡ رَبُّهُمۡ لَنُهۡلِكَنَّ ٱلظَّـٰلِمِينَ
Na walisema waliokufuru (kuwaambia) Mitume wao: Tutakutoeni mkuku katika nchi yetu, au mrudi katika dini yetu. Basi Mola wao Mlezi aliwaletea wahyi: Hakika tutawaangamiza madhalimu
وَلَنُسۡكِنَنَّكُمُ ٱلۡأَرۡضَ مِنۢ بَعۡدِهِمۡۚ ذَٰلِكَ لِمَنۡ خَافَ مَقَامِي وَخَافَ وَعِيدِ
Na tutakuwekeni katika ardhi baada yao. Haya ni kwa anayeogopa kusimamishwa mbele yangu, na akaogopa maonyo yangu (ya adhabu)
وَٱسۡتَفۡتَحُواْ وَخَابَ كُلُّ جَبَّارٍ عَنِيدٖ
Na (Mitume) waliomba nusra (kwa Allah dhidi ya mahasimu wao), na alishindwa kila jabari mkaidi
مِّن وَرَآئِهِۦ جَهَنَّمُ وَيُسۡقَىٰ مِن مَّآءٖ صَدِيدٖ
(Kila mkaidi ajue) Usoni (mbele) yake ipo Jahanamu (inamngoja), na atanyweshwa maji ya usaha (na damu itiririkayo kutoka kwenye mili ya watu wa Motoni)
يَتَجَرَّعُهُۥ وَلَا يَكَادُ يُسِيغُهُۥ وَيَأۡتِيهِ ٱلۡمَوۡتُ مِن كُلِّ مَكَانٖ وَمَا هُوَ بِمَيِّتٖۖ وَمِن وَرَآئِهِۦ عَذَابٌ غَلِيظٞ
Ataugugumia usaha (na damu ili akate kiu), wala hawezi kuumeza (kutokana na kinyaa na kuunguza kwake). Na (sababu za) mauti zitamjia kutoka kila upande (wa kiungo, lakini), wala hafi. Na zaidi ya hayo ipo adhabu nyingine kali zaidi
مَّثَلُ ٱلَّذِينَ كَفَرُواْ بِرَبِّهِمۡۖ أَعۡمَٰلُهُمۡ كَرَمَادٍ ٱشۡتَدَّتۡ بِهِ ٱلرِّيحُ فِي يَوۡمٍ عَاصِفٖۖ لَّا يَقۡدِرُونَ مِمَّا كَسَبُواْ عَلَىٰ شَيۡءٖۚ ذَٰلِكَ هُوَ ٱلضَّلَٰلُ ٱلۡبَعِيدُ
Mfano (wa kutisha wa) waliomkufuru Mola wao Mlezi, vitendo vyao (vyema ikiwemo kuunga udugu n.k Siku ya Kiyama havitawafaa) ni kama jivu linalopeperushwa kwa nguvu za upepo katika siku ya dhoruba. Hawawezi kupata chochote katika waliyoyachuma. Huo ndio upotevu wa mbali
أَلَمۡ تَرَ أَنَّ ٱللَّهَ خَلَقَ ٱلسَّمَٰوَٰتِ وَٱلۡأَرۡضَ بِٱلۡحَقِّۚ إِن يَشَأۡ يُذۡهِبۡكُمۡ وَيَأۡتِ بِخَلۡقٖ جَدِيدٖ
(Ewe unaeambiwa habari hii) Hivi uoni kuwa Allah ameziumba mbingu na ardhi kwa Haki? Akitaka atakuondoeni na ataleta viumbe wapya kabisa (watiifu zaidi kuliko nyinyi)
وَمَا ذَٰلِكَ عَلَى ٱللَّهِ بِعَزِيزٖ
Na hilo (la kuwaondoeni na kuleta viumbe wapya) kwa Allah si jambo gumu
وَبَرَزُواْ لِلَّهِ جَمِيعٗا فَقَالَ ٱلضُّعَفَـٰٓؤُاْ لِلَّذِينَ ٱسۡتَكۡبَرُوٓاْ إِنَّا كُنَّا لَكُمۡ تَبَعٗا فَهَلۡ أَنتُم مُّغۡنُونَ عَنَّا مِنۡ عَذَابِ ٱللَّهِ مِن شَيۡءٖۚ قَالُواْ لَوۡ هَدَىٰنَا ٱللَّهُ لَهَدَيۡنَٰكُمۡۖ سَوَآءٌ عَلَيۡنَآ أَجَزِعۡنَآ أَمۡ صَبَرۡنَا مَا لَنَا مِن مَّحِيصٖ
Na (viumbe) wote watatoka (makaburini na) kuhudhuria mbele ya Allah. Basi (wale wafuasi waliokuwa wanafuata mkumbo) wanyonge watawaambia (wakubwa wao) waliotakabari: Sisi tulikuwa wafuasi wenu; basi hamuwezi kutuondolea adhabu ya Allah japo kidogo? Watasema: Lau Allah angelituongoa (tukawa waumini) basi hapana shaka nasi tungelikuongoeni. Ni mamoja kwetu (kama) tutapapatika au tutasubiri; hatuna pa kukimbilia
وَقَالَ ٱلشَّيۡطَٰنُ لَمَّا قُضِيَ ٱلۡأَمۡرُ إِنَّ ٱللَّهَ وَعَدَكُمۡ وَعۡدَ ٱلۡحَقِّ وَوَعَدتُّكُمۡ فَأَخۡلَفۡتُكُمۡۖ وَمَا كَانَ لِيَ عَلَيۡكُم مِّن سُلۡطَٰنٍ إِلَّآ أَن دَعَوۡتُكُمۡ فَٱسۡتَجَبۡتُمۡ لِيۖ فَلَا تَلُومُونِي وَلُومُوٓاْ أَنفُسَكُمۖ مَّآ أَنَا۠ بِمُصۡرِخِكُمۡ وَمَآ أَنتُم بِمُصۡرِخِيَّ إِنِّي كَفَرۡتُ بِمَآ أَشۡرَكۡتُمُونِ مِن قَبۡلُۗ إِنَّ ٱلظَّـٰلِمِينَ لَهُمۡ عَذَابٌ أَلِيمٞ
Na Shetani atawaambia wafuasi (wake huko Akhera) mara itapokatwa hukumu (na watu wa Peponi kuingia Peponi na wa Motoni kuingia Motoni): Hakika Allah alikuahidini ahadi ya kweli. Nami nilikuahidini (uongo); lakini sikukutimizieni. Na sikuwa na mamlaka juu yenu, isipokuwa nilikuiteni (katika ukafiri na maasi), nanyi mkaniitikia. Basi msinilaumu mimi, bali jilaumuni wenyewe. Mimi siwezi kuwa msaidizi wenu, wala nyinyi hamuwezi kuwa wasaidizi wangu. Hakika mimi nilikataa tangu zamani kunishirikisha na Allah. Hakika madhalimu watakuwa na adhabu chungu mno
وَأُدۡخِلَ ٱلَّذِينَ ءَامَنُواْ وَعَمِلُواْ ٱلصَّـٰلِحَٰتِ جَنَّـٰتٖ تَجۡرِي مِن تَحۡتِهَا ٱلۡأَنۡهَٰرُ خَٰلِدِينَ فِيهَا بِإِذۡنِ رَبِّهِمۡۖ تَحِيَّتُهُمۡ فِيهَا سَلَٰمٌ
Na (Allah) atawaingiza walioamini na waliotenda mema katika Pepo ipitayo mito mbele yake, watadumu humo kwa idhini ya Mola wao Mlezi. Maamkizi yao humo (kutoka kwa Allah na Malaika) yatakuwa: Salaam[1]
1- - Rejea Sura ArRa’d 13: 24 “Amani iwe kwenu, kwa sababu mlisubiri, basi ni mema yaliyoje matokeo ya
nyumba ya Akhera
أَلَمۡ تَرَ كَيۡفَ ضَرَبَ ٱللَّهُ مَثَلٗا كَلِمَةٗ طَيِّبَةٗ كَشَجَرَةٖ طَيِّبَةٍ أَصۡلُهَا ثَابِتٞ وَفَرۡعُهَا فِي ٱلسَّمَآءِ
(Ewe unayeambiwa) Kwani hukuona vipi Allah alivyopiga mfano wa neno zuri (ambapo amelilinganisha neno Lailaha illa LLah)? Ni kama mti mzuri, mizizi yake ni imara, na matawi yake (yamechanua) kuelekea mbinguni
تُؤۡتِيٓ أُكُلَهَا كُلَّ حِينِۭ بِإِذۡنِ رَبِّهَاۗ وَيَضۡرِبُ ٱللَّهُ ٱلۡأَمۡثَالَ لِلنَّاسِ لَعَلَّهُمۡ يَتَذَكَّرُونَ
Hutoa matunda yake kila wakati kwa idhini ya Mola wake Mlezi. Na Allah huwapigia watu mifano ili wapate kukumbuka
وَمَثَلُ كَلِمَةٍ خَبِيثَةٖ كَشَجَرَةٍ خَبِيثَةٍ ٱجۡتُثَّتۡ مِن فَوۡقِ ٱلۡأَرۡضِ مَا لَهَا مِن قَرَارٖ
Na mfano wa neno ovu (neno la ukafiri) ni kama mti muovu, uliong’olewa juu ya ardhi. Hauna uimara
يُثَبِّتُ ٱللَّهُ ٱلَّذِينَ ءَامَنُواْ بِٱلۡقَوۡلِ ٱلثَّابِتِ فِي ٱلۡحَيَوٰةِ ٱلدُّنۡيَا وَفِي ٱلۡأٓخِرَةِۖ وَيُضِلُّ ٱللَّهُ ٱلظَّـٰلِمِينَۚ وَيَفۡعَلُ ٱللَّهُ مَا يَشَآءُ
Allah anawathibitisha wale walioamini kwa kauli thabiti[1] katika maisha ya dunia (kaburini)[2] na katika Akhera. Na Allah huwapoteza madhalimu. Na Allah anafanya analolitaka
1- - Neno madhubuti na imara ni Lailaha illa llah na kila neno la haki na kweli
2- - Wakati watakapokuwa wanaulizwa na Malaika wawili kuhusu Mola wao, Dini yao na Mtume wao?
۞أَلَمۡ تَرَ إِلَى ٱلَّذِينَ بَدَّلُواْ نِعۡمَتَ ٱللَّهِ كُفۡرٗا وَأَحَلُّواْ قَوۡمَهُمۡ دَارَ ٱلۡبَوَارِ
Kwani hukuwaona wale (maka-firi) waliobadilisha neema za Allah kuwa kufuru, na wakawafikisha watu wao kwenye nyumba ya maangamivu?
جَهَنَّمَ يَصۡلَوۡنَهَاۖ وَبِئۡسَ ٱلۡقَرَارُ
(Nao wataingia) Jahanamu, maovu yaliyoje makazi hayo!?
وَجَعَلُواْ لِلَّهِ أَندَادٗا لِّيُضِلُّواْ عَن سَبِيلِهِۦۗ قُلۡ تَمَتَّعُواْ فَإِنَّ مَصِيرَكُمۡ إِلَى ٱلنَّارِ
Na walimfanyia Allah washirika ili wapoteze watu kwenye Njia yake. Sema: Stareheni, kwani marejeo yenu ni Motoni
قُل لِّعِبَادِيَ ٱلَّذِينَ ءَامَنُواْ يُقِيمُواْ ٱلصَّلَوٰةَ وَيُنفِقُواْ مِمَّا رَزَقۡنَٰهُمۡ سِرّٗا وَعَلَانِيَةٗ مِّن قَبۡلِ أَن يَأۡتِيَ يَوۡمٞ لَّا بَيۡعٞ فِيهِ وَلَا خِلَٰلٌ
Waambie waja wangu walioa-mini, wasimamishe Swala, na watoe katika tulivyowaruzuku, kwa siri na dhahiri, kabla haijafika Siku isiyofaa kitu fidia wala urafiki
ٱللَّهُ ٱلَّذِي خَلَقَ ٱلسَّمَٰوَٰتِ وَٱلۡأَرۡضَ وَأَنزَلَ مِنَ ٱلسَّمَآءِ مَآءٗ فَأَخۡرَجَ بِهِۦ مِنَ ٱلثَّمَرَٰتِ رِزۡقٗا لَّكُمۡۖ وَسَخَّرَ لَكُمُ ٱلۡفُلۡكَ لِتَجۡرِيَ فِي ٱلۡبَحۡرِ بِأَمۡرِهِۦۖ وَسَخَّرَ لَكُمُ ٱلۡأَنۡهَٰرَ
Allah ndiye aliyeziumba mbingu na ardhi, na akateremsha maji kutoka mawinguni. Na kwa hayo akatoa matunda kuwa ni riziki yenu. Na akayatiisha majahazi yanayopita baharini kwa amri yake, na akaitiisha mito ikutumikieni (kwa manufaa yenu mbalimbali)
وَسَخَّرَ لَكُمُ ٱلشَّمۡسَ وَٱلۡقَمَرَ دَآئِبَيۡنِۖ وَسَخَّرَ لَكُمُ ٱلَّيۡلَ وَٱلنَّهَارَ
Na akalitiisha jua na mwezi kwa manufaa yenu daima dawamu (ili mjue miaka na hesabu), na akautiisha usiku (ili mpumzike) na mchana kwa manufaa yenu (ili mfanye kazi)
وَءَاتَىٰكُم مِّن كُلِّ مَا سَأَلۡتُمُوهُۚ وَإِن تَعُدُّواْ نِعۡمَتَ ٱللَّهِ لَا تُحۡصُوهَآۗ إِنَّ ٱلۡإِنسَٰنَ لَظَلُومٞ كَفَّارٞ
Na akakupeni kila mlicho-muomba. Na mkizihesabu neema za Allah hamuwezi kuzidhibiti. Hakika mwanadamu ni dhalimu mkubwa, mwenye kuzikufuru sana neema
وَإِذۡ قَالَ إِبۡرَٰهِيمُ رَبِّ ٱجۡعَلۡ هَٰذَا ٱلۡبَلَدَ ءَامِنٗا وَٱجۡنُبۡنِي وَبَنِيَّ أَن نَّعۡبُدَ ٱلۡأَصۡنَامَ
Na (kumbuka) Ibrahim alipo-sema: Ewe Mola wangu Mlezi, ujaalie mji huu uwe wa amani (kwa watu, mimea na wanyama) na uniepushe mimi na wanangu kuabudu masanamu